Monday, August 27, 2012

Baadhi ya Waislamu wagomea sensa

SENSA ya watu na makazi iliyoanza jana nchini kote, imegubikwa na kasoro kadhaa katika maeneo mbalimbali, huku suala la uhaba wa vifaa kwa makarani likionekana kuwa kubwa.

Tanzania Daima ilifanikiwa kupita kwenye mitaa kadhaa ya mikoa mbalimbali na kuzungumza na wananchi, makarani wa sensa na viongozi wa serikali na kubaini dosari hizo.

Hata hivyo, mbali ya uhaba wa vifaa kwa makarani, pia tishio la baadhi ya viongozi wa Kiislamu kuwashawishi waumini wao kususia, nalo lilileta mkanganyiko kwa baadhi ya maeneo.

Katika maeneo kadhaa, vilionekana vipeperushi kwenye baadhi ya nyumba vyenye ujumbe wa kuwakataza Waislamu wasishiriki shughuli hiyo, jambo lililowalazimu polisi kusambaa mitaani na kuwatia mbaroni baadhi ya watu waliodaiwa kuvisambaza.

Pia, uelewa mdogo wa baadhi ya makarani nao ulilalamikiwa na wananchi wengi, kwani walitumia muda mrefu kuandikisha taarifa zao na huku wakidai kuwa maswali mengine yanayoulizwa kwenye dodoso hizo hayana maana yoyote.

Waislamu wasusia Dar

Jijini Dar es Salaam, makarani katika baadhi ya maeneo walikwama kupata takwimu za baadhi ya wakazi kutokana na kushikilia msimamo wa viongozi wao wa kiroho wa kususia sensa hiyo.

Tanzania Daima ilifika kwenye maeneo tofauti ukiwemo Mtaa wa Kibondemaji wilayani Temeke na kubaini changamoto hizo za baadhi ya waumini wa Kiislamu kupinga kuhesabiwa.

Akizungumza na Tanzania Daima Mwenyekiti wa Mtaa huo, Rashidi Mrisho, alisema hadi sasa kumekuwa na upinzani kutoka dhehebu hilo ambapo katika mtaa huo, nyumba zaidi ya 13 zimepinga kuhesabiwa.

Alisema waumini hao, wamedai kuwa shughuli hiyo imekiuka kipengele namba 2.109 hadi 2.111 cha Umoja wa Mataifa, kinachosema takwimu ni lazima ioneshe kila dhehebu kama sehemu inayounda jamii nzima kwa ujumla wake, maelezo mafupi ya waumini wa dini au dhehebu.

Aliongeza kuwa, kitendo cha kutowalipa wajumbe wa mitaa, pia ni moja ya changamoto ambayo imeifanya kazi hiyo kukosa msisimko wa kutosha.

Hata hivyo, alisema kwa wajumbe waliopinga kutoa ushirikiano, majina yao yatafikishwa ngazi za mbele zaidi kwa ajili ya hatua za kinidhamu.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Miembeni wilayani Ilala, Saburi Sabur, alisema pamoja na watu wengi kutoa ushirikiano, bado baadhi ya Waislamu wameendeleza msimamo wao wa kupinga kwa madai kuwa wanatii maelekezo ya viongozi wao.

Alisema kuwa, katika mtaa huo inaonesha nyumba zipatazo 30 wakazi wake walipinga mpango huo wa sensa, kwa kutotoa ushirikiano kwa makarani.

Akizungumzia kuhusu malipo ya wajumbe wa mtaa, Saburi alisema tatizo hilo kwake halikuwapo kwa kuwa kila mjumbe alilipwa sh 20,000 ambapo mwenyekiti alilipwa sh 100,000.

Katika hatua nyingine, Saburi alisema iwapo upizani kama huo ukiendelea, kuna hatari kazi hiyo ikashindwa kukamilika katika muda uliopangwa wa siku saba.

Alifafanua kuwa, katika mtaa huo shughuli hiyo ilichelewa kuanza kutokana na vifaa kuchelewa kufika ambapo makarani ilibidi wakae kwa muda mrefu bila kazi hadi vilipoletwa.

Wakati gazeti hili linakwenda mitamboni, kulikuwa na taarifa kuwa kituo cha polisi wilayani Temeke kimevamiwa na baadhi ya wananchi waliokuwa wakidai kupinga kitendo cha wenzao kukamatwa baada ya kugomea sensa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Davis Misime licha ya kukanusha taarifa hizo, lakini alikiri kuwa watu 17 walikamatwa kwa ajili ya mahojiano kwa kugoma kuhesabiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Alisema watu hao ni kutoka maeneo ya Kindungulile kata ya Mianzini, Yombo Kilakala-Barabara ya Mwinyi, Kiburugwa, Kigamboni na Kibada.

Kagera wakosa vifaa

Kutoka mkoani Kagera katika Wilaya ya Biharamulo, makarani 1,999 wameilalamikia kamati ya sensa kwa kuchelewa kuwagawia vifaa vya kazi katika vituo vyao.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya makarani hao walisema hadi kufikia saa tatu asubuhi, walikuwa hawajagawiwa vifaa hivyo.

Walisema, kamati ya sensa wilayani humo, ilishindwa kutoa ushirikiano kwao hali inayoweza kuchangia kutofanikiwa kwa shughuli hiyo licha ya kukaa kwenye vituo vyao kwa muda wa siku tatu kama walivyoagizwa na wasimamizi wao wakisubiri vifaa.

Mmoja wa makarani hao, Paulo Kamihanda kutoka Kata ya Nyarubungo, alisema kuwa vifaa vya kazi zikiwemo sare, kofia pamoja na malipo ya siku ya kwanza na nauli bado hawajapewa.

“Kulingana na jiografia ya Biharamulo ilivyo, mpaka kufikia muda huu hatujakabidhiwa vifaa, unategemea nini? Kama si kukwamisha sensa ni nini?” alihoji.

Aidha, aliyataja baadhi ya maeneo ambayo yamecheleweshewa vifaa hivyo ni pamoja na kata za Nyarubungo, Nemba, Nyantakala na Kalenge.

Mratibu wa sensa wilayani humo, Richard Kalulu alikiri kuwepo kwa ucheleweshaji wa vifaa, akisema vilipokelewa saa 6 usiku wa kuamkia jana kutoka Bukoba, hivyo kusababisha uchelewaji huo.

Wakesha msikitini Arusha

Mkoani Arusha, baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu juzi waliamua kukesha msikitini kutimiza azima yao ya kutokuhesabiwa kama walivyohamasishwa na viongozi wao.

Wanaodaiwa kukesha msikitini, ni baadhi ya waumini wa Msikiti Mkuu wa Bondeni, ambao waliondoka hapo jana baada ya swala ya alfajiri.

Hata hivyo, mwenyekiti wa msikiti huo, Abdulazizi Mkindi, alikanusha madai hayo kwa kile alichowaeleza waandishi wa habari kuwa, awali walipanga kufanya mkesha msikitini hapo kwa ajili ya kuiombea nchi amani, lakini waliahirisha baada ya vifaa vya maandalizi kutotimia.

“Ni kweli ilikuwa tufanye mkesha wa kuiombea nchi amani, kwani inapita kwenye kipindi kigumu, kuna mambo ya sensa na mambo mengine, lakini ilibidi tuahirishe kwani vifaa havikutimia… tulikuwa tumepata mbuzi saba na ng’ombe mmoja, lakini swala hiyo ya mkesha itafanyika leo,” alisema.

Alisema kuwa hao wanaodaiwa kulala msikitini hapo inaweza kuwa ni wageni ambao ni utaratibu wa kawaida endapo Muislamu atafika mahali na kukosa pa kulala, basi huenda msikitini.

Mkindi alisema kuwa, msimamo wa kugomea sensa uliisha baada ya viongozi wa dini hiyo kukutana na Rais Jakaya Kikwete Ikulu na kuahidi kufanyia kazi malalamiko yao.

Hata hivyo, Katibu wa Baraza la Waislamu (BAKWATA) mkoani hapa, Abudulkareem Jonjo, alikiri kupata taarifa za baadhi ya waumini kulala msikitini hapo, hivyo kuwahimiza kuacha msimamo wa kutohesabiwa.

Mratibu wa sensa mkoani hapa, Magreth Martin, alisema kuwa mpaka jana saa kumi jioni, shughuli hiyo ilikuwa ikiendelea vizuri licha ya kuwepo kwa kasoro za upungufu wa vifaa kama vizibao vinavyopaswa kuvaliwa na makarani wa sensa.

Baadhi ya wananchi wilayani hapa nao waligoma kuhesabiwa, hivyo kuwafanya makarani wa sensa kuwa katika wakati mgumu kupata takwimu zao.

Hali hiyo ililazimu mratibu wa sensa kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa sensa, Mkuu wa Wilaya, John Mongela na kuitisha kikao cha dharura kushughulikia tatizo hilo haraka.

Akizungumza na gazeti hili, mratibu wa sensa, Palangyo, alisema maeneo yaliyokutwa na changamoto hiyo ya mgomo ni kata za Elerai, Ngarenaro, Oysterbay, Engutoto, Sombetini na Unga Limited ambapo wahusika walikataa kuandikishwa bila kutoa sababu zozote.

Iringa shwari

Mkoani Iringa, shughuli ya sensa ya watu na makazi ilianza katika hali ya utulivu katika maeneo mbalimbali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alisema kuwa tangu kuanza shughuli hiyo saa 6 usiku wa kuamkia jana, hakuna tukio lolote la uvunjifu wa amani ambalo limetokea.

Alisema kuwa, jeshi hilo linaendelea kujipanga kuona kila Mtanzania anatumia haki yake ya msingi katika kuhesabiwa bila kuzuiwa na mtu ama kikundi chochote.

Vifaa adimu Dodoma

Uhaba wa vifaa kwa makarani umeukumba pia Mkoa wa Dodoma jana wakati shughuli ya sensa ya watu na makazi ikianza rasmi nchini nzima, hivyo kuleta usumbufu.

Mkuu wa mkoa huo, Dk. Rehema Nchimbi, alithibitisha uwepo wa kasoro hiyo akisema ilitokana na upungufu wa vifaa kama majaketi kwa ajili ya makarani.

Alisema kuwa majaketi hayo ambayo hutumika kuwatambulisha makarani hayakuweza kufika kwa wakati na kusababisha baadhi yao kutumia vitambulisho kwa kuvaa shingoni badala ya makusudio ya awali.

Alipoulizwa ni kwanini vifaa hivyo vimechelewa kufika wakati maandalizi ni ya muda mrefu, alisema kuwa jambo hilo lipo nje ya uwezo wake kwani vifaa vyote vilikuwa vinapakiwa kutoka jijini Dar es Salaam kupelekwa katika mikoa mbalimbali.

Hata hivyo, alisema kutokana na kukosekana kwa vifaa hivyo, bado hakuzuii shughuli ya sensa kuendelea.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili, walisema pamoja na siku hiyo kuwa ya Jumapili, lakini wamepoteza muda wao mwingi kuwasubiria makarani bila mafanikio.

Geita utata mtupu

Mkoani Geita, sensa ya watu na makazi imekuwa na utata mkubwa baada ya vifaa kuchelewa kukabidhiwa kwa makarani, baadhi ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji kususia kushiriki na kucheleweshwa kwa malipo ya makarani.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, walisema shughuli hiyo haiwezi kufanikiwa kwa asilimia 100 kutokana na maandalizi kuwabagua viongozi hao wa vijiji na vitongoji licha ya serikali kutambua wazi kuwa ndio wapo karibu zaidi na wananchi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Elimu, Khasan Mwibara na Khamisi Jagi ambaye ni mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyantorontoro, Kata ya Kalangalala, walisema wameshindwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa makarani hao kutokana na wao kutoshirikishwa katika mchakato mzima tangu awali.

Walidai kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakiwapigia simu tangu kuanza kwa sensa jana asubuhi baada ya kuwafananisha makarani na vibaka kutokana na kutokuwa na sare, vitambulisho wala kutembezwa na kiongozi yeyote wa kijiji au kitongoji.

Mratibu wa Sensa Mkoa wa Geita, Ersmus Lugarabamu, alikiri shughuli hiyo kukumbwa na changamoto mbalimbali na kudai kuwa hali hiyo ilitokana na serikali kuchelewesha vifaa vilivyohitajika kutoka jijini Dar es Salaam.

Mbali ya changamoto hizo, alisema tayari baadhi ya vifaa vimewasili japo kwa kuchelewa, na kwamba vimegawiwa na kazi inatarajiwa kuendelea vizuri kuanzia leo.


Source: Tanzania Daima.