Monday, July 23, 2012

Wabunge wamsafishia Zitto njia ya Urais 2015


Mbunge Zitto Kabwe

NI JOSHUA NASSARI WA CHADEMA, DEO FILIKUNJOMBE WA CCM, WASEMA KIGOMA WAJIANDAE KUTOA RAIS
IKIWA imebaki miaka mitatu kabla ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini mwaka 2015, wabunge wawili vijana wamewataka wakazi wa Mkoa wa Kigoma kujiandaa kumpata kutoka eneo hilo.

Kauli za Wabunge hao zimekuja kipindi ambacho mchakato wa Katiba unaendelea huku kukiwa na uwezekano wa umri wakugombea urais kushuka hivyo kuwawezesha wanasiasa wengi vijana akiwamo Zitto, kugombea nafasi hiyo.

Wakizungumza katika tamasha kubwa lililokutanisha mamia ya wakazi wa Mkoa wa Kigoma, Deo Filikunjombe ambaye ni mbunge wa Ludewa (CCM), Joshua Nasari wa Arumeru Mashariki (Chadema) na Halima Mdee, Kawe (Chadema), walisema wanaamini Rais wa 2015 atakuwa Mbunge wa Kigoma kaskazini na ambaye ni mzaliwa wa mkoa huo.

Katika kauli yao hiyo, wabunge hao walisema Mbunge huyo ameonyesha umahiri mkubwa katika kusimamia mambo ya kitaifa bila upendeleo, jambo linalomfanya kujijengea umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi, hivyo kuonekana wazi kulibeba vema kundi la Vijana wa Taifa hili.

Akimzungumzia kuhusu rais ajaye kutoka Kigoma, Filikunjombe alisema kundi la vijana lazima liungane kuhakikisha kuwa linatoa viongozi watakaopigania maslahi yao na Taifa kwa jumla ili kuleta ukombozi wa kifikra na kimaendeleo kwa maslahi ya jamii.

"Lazima mtambue kuwa, Tanzania ni nchi yetu sisi wote na lazima vijana wote bila kujali itikadi zetu za kisiasa tunatakiwa kujipa moyo kwamba tunaweza kufanya makubwa katika kuleta maendeleo ya jamii katika nchi yetu," alisema Filikunjombe na kuongeza:

"Vijana wa Kigoma mnabahati ya kuwa na Wabunge wazuri na ninaamini miaka michache ijayo lazima mkoa huu utoe Rais wa Tanzania."

Huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu waliokusanyika katika uwanja wa Lake Tanganyika mjini hapa kuhudhuria tamasha hilo lililopambwa na wasanii nyota wa kizazi kipya kutoka Mkoa wa Kigoma, Filikunjombe alisema; "Zitto anastahili kuwa rais".

Mbunge huyo wa CCM ambaye katika siku za karibuni ameonekana kuwa mshirika mkubwa wa kisiasa wa Zitto na Chadema, alisema Zitto anafaa kuwa Rais kwani amefanikiwa kuwaunganisha watu na kuleta umoja miongoni mwao, jambo ambalo linadumisha umoja wa kitaifa.

Kauli ya Nassari
Kwa upande wake Nasari, alisema Mkoa wa Kigoma umejitokeza wazi kuwa na wanasiasa mahiri na wenye vipaji vya hali ya juu katika kupigania maslahi ya wananchi pamoja na kupambana na ufisadi unaodidimiza uchumi wa taifa letu na kuwanufaisha wachache kwa kutumia nafasi zao.

‘Leo, ni mara yangu ya kwanza kufika Kigoma, lakini kwa jinsi ninavyoona mpangilio mzuri wa shughuli hii, naamini kabisa kuwa, Zitto Kabwe aliyeandaa hafla hii na kuwakusanya wasanii wa Kigoma kuwa kitu kimoja anafaa kabisa kuwa rais ajaye wa Taifa letu. Na haya ninayasema kwa uhakika bila hata chembe ya mzaha," alisema Nasari.

Huku akishangiliwa na mamia hayo ya wakazi wa Kigoma, alifafanua kwamba wanasiasa vijana wamejipanga kuwatetea wananchi na hususani kundi la vijana katika kuondoa matatizo mbalimbali yanayowasibu katika maisha kwa kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya kazi zao za uzalishaji mali.

Mdee amliza Zitto
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kawe Halima Mdee (Chadema) alimliza Zitto jukwaani baada ya kumuelezea kuwa ni ‘jembe’ katika mambo mbalimbali na mtu mwenye uchungu na maendeleo ya taifa.

Mdee aliyepewa nafasi ya kuwasalimia Wananchi alisema amekuwa na Zitto tangu Chuo kikuu cha Dar es Salaam na kwamba kutokana na ujasiri na umahiri wake katuika kutetea masilahi ya wanyonge na taifa, anafaa kuwa mmoja wa viongozi wa juu katika Taifa.

‘Ndugu zangu watu wa Kigoma, kwa kweli mna bahati sana, achilia mbali kuwa na vipaji katika sanaa ya muziki na michezo hasa mpira wa miguu, lakini mna wanasiasa wakali ambao ni tishio hapa nchini. Mimi namkubali sana Zitto Kabwe na ninaamini kuna siku atakuwa kiongozi wa juu katika nchi yetu," alisema Mdee.

Mdee alipongeza ushirikiano wa wananchi wa Kigoma na kusisitiza kuwa unatakiwa kuenziwa na kuigwa na mikoa mingine.

Zitto akiri kutoa machozi

Zitto alipulizwa na gazeti hili alikiri kudondosha machozi jukwaani kutokana na Mdee kuzungumza kwa hisia kali na hivyo maneno yake kumchoma na kushindwa kujizuia jukwaani.

" Kwa weli Halima Mdee aluzumgumza maneno mazito sana na alinikumbusha mbali enzi za Chuo kikuu tukiwa kwenye harakati za kutetea maslahi ya wanachuo na pia nimekuwa naye kwenye harakati za kisiasa ndani ya Chadema, ndiyo maana nilishindwa kujizuia na kuanza kutoa machozi," alisema Zitto.

Alisema amefarijika kuwaona wabunge wenzake kutoka vyama vya CCM, NCCR Mageuzi, Chadema na CUF wamefika Kigoma kumuunga mkono katika uzinduzi wa wimbo wa 'Leka dutigite' ulioimbwa kwa pamoja na wasanii wa muziki wenye asili ya Kigoma.

Zitto alisema Mkoa wa Kigoma kwa muda mrefu umekuwa nyuma kimaendeleo hivyo, kuufanya kudharauliwa na watu wengi hata kama hawajui lolote juu ya eneo hilo.

‘Wapo watu wanaotubeza kwamba mkoa wetu ni masikini na haufai kuishi, na kasumba hii imejengeka hadi kwa baadhi ya watumishi wa Serikali. Ndiyo maana sishangai ninaposikia kwamba kuna watumishi wa Serikali wanakataa kuhamia Kigoma. Lakini hii dhana sasa itaisha," alifafanua Zitto.

Wabunge waliohudhuria

Wabunge waliofika Kigoma kwenye hafla hiyo ni Mdee , Amina Mwidau wa viti maalumu (CUF), Esta Bulaya ( Viti maalumu (CCM), Filikunjombe (CCM), Kangi Lugola wa Mwibara, David Kafulila (Kigoma Kusini, NCCR-Mageuzi), Nasari (Arumeru Mashariki Chadema) na Raya Ibrahim Khamis wa viti maalumu kutoka Pemba.

Kauli ya Nape
Alipoulizwa Katibu Mwenezi wa CCM Nape Nnauye kuhusu Filikunjombe kumtabiria Zitto kuwa Rais wakati anatoka upinzani, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hajasikia wala kulisoma popote.

“Nyie andikeni kwanza halafu ndiyo nitaweza kusema, kwa sasa siwezi kusema chochote kwa sababu sijasikia kitu chochote ama kusoma popote pale jambo hilo,” alisema Nape.