Monday, July 23, 2012
Mbunge Chadema anusurika kwenda jela
MBUNGE wa Maswa Mashariki, Christopher Kasulumbai (62) amenusurika kwenda jela miezi minne kwa kosa la kumshambulia aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga, badala yake amelipa faini ya Sh 150,000.
Kasulumbai ambaye ni Mbunge kupitia tiketi ya Chadema, alinusurika kwenda jela miezi minne baada ya kulipa faini ya Sh 100,000 kwa kosa la shambulio na Sh 50,000 au kifungo cha miezi mitatu jela kwa kumtukana Mkuu huyo wa Wilaya.
Pamoja na Kasulumbai pia mahakama hiyo ilitoa adhabu kama hiyo kwa mwanachama wa Chadema aliyeshitakiwa pamoja na Mbunge huyo, Robert Magilani, ambaye alipatikana na hatia sawa na ya Mbunge huyo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, Thomas Simba alisema pamoja na kuwapa adhabu hiyo, pia washitakiwa hao watatakiwa kulipa fidia ya Sh milioni moja kila mmoja kwa Kimario.
Mbunge Kasulumbai, alifungwa pingu kwa saa kadhaa kabla ya kulipa faini hiyo hivyo kulazimika kusubiri katika chumba cha mahabusu na baada ya kulipa faini aliachiwa.
Mahakama hiyo pia iliwaachia huru washitakiwa wawili ambao ni Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Suzan Kiwanga na Katibu wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) Igunga, Annuar Kashaga baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yao.
Hakimu Simba alitaja mashitaka ambayo hayakuthibitika mbele ya Mahakama hiyo kuwa ni kumweka chini ya ulinzi Mkuu wa Wilaya na kumwibia simu mbili za mkononi aina ya Nokia.
Hakimu alitoa adhabu hiyo kwa washitakiwa na kubaini wazi kwamba washitakiwa hao au upande wa mashitaka wana haki ya kukata rufaa ndani ya siku 30 baada ya hukumu hiyo.