BARAZA la Madaktari Tanganyika limesema
madaktari 390 waliokuwa mafunzoni katika hospitali mbalimbali nchini na
kugoma kazi, wamepoteza sifa na kwa sababu hiyo, usajili wao
umesitishwa.
Kutokana na hali hiyo, usajili wao wa
muda umesitishwa kuanzia leo na madaktari wote wanaohusika, wametakiwa
kurejesha hati za usajili wa muda kwenye Ofisi ya Msajili wa Madaktari
kabla ya Julai 17.
Hatua hiyo imo katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Baraza la Madaktari Tanganyika, Dk Donan Mmbando.
Taarifa ya Dk Mmbando ilieleza kwamba
imechukua hatua hiyo baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, kumwandikia akilalamikia hatua ya madaktari hao kugoma.
Kwa mujibu wa Dk Mmbando, Katibu Mkuu
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii aliwasilisha malalamiko kwenye Baraza
la Madaktari Tanganyika kwamba madaktari waliogoma walikataa kutoa
huduma za kitaalamu, ikiwa ni wajibu wao na kwamba kitendo hicho
kilihatarisha maisha ya wagonjwa katika hospitali husika na pia ni
kinyume cha maadili ya taaluma ya udaktari.
Mwenyekiti huyo alieleza, kwamba
walipokea malalamiko kutoka kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, kwamba baadhi ya madaktari waliopata usajili wa muda ili
kuwawezesha kufanya mafunzo kwa vitendo, waligoma kutoa huduma kwa
wagonjwa kati ya Juni 23 na 29.
Ilieleza kuwa madaktari hao walipangiwa
kutoa huduma kwa wagonjwa katika hospitali za Muhimbili, K.C.M.C, Rufaa
Mbeya, Bugando, Amana, Temeke, St. Francis- Ifakara, Mwananyamala, Sekou
Toure, Hydom na Dodoma.
“Kutokana na malalamiko hayo, Msajili wa
Baraza la Madaktari Tanganyika, alimwandikia kila daktari
aliyelalamikiwa Taarifa ya Kusudio la Kufanya Uchunguzi dhidi yake, juu
ya malalamiko yaliyowasilishwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii.
“Baraza la Madaktari Tanganyika
limebaini kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 15(2) cha Sheria ya Madaktari,
Sura ya 152, madaktari waliokuwa kwenye mgomo na ambao kwa sasa
wameondolewa katika hospitali walizokuwa wakifanya mafunzo kwa vitendo,
wamepoteza sifa za usajili wa muda,” ilieleza taarifa ya Dk Mmbando.
“Kwa kuzingatia masharti ya sheria
kuhusu kupata usajili wa muda, Baraza la Madaktari Tanganyika
limeridhika, kwamba madaktari wote ambao majina yao yameorodheshwa
katika taarifa hii, wamepoteza sifa na kwa sababu hiyo, usajili wao
umesitishwa kuanzia Julai 11,” ilisema taarifa.
Alitaja idadi ya madaktari 390 na
hospitali walizotoka kuwa ni Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (103); KCMC
(66); Rufaa Mbeya (55); Rufaa Bugando (43); Amana (26); Temeke (17), St
Francis (17); Mwananyamala (26); Sekou Toure (14), Hydom (14) na Dodoma
(2).
Madaktari hao waligoma baada ya
kushindwa kuafikiana na Serikali katika nyongeza ya mshahara ambao
walikuwa wakitaka walipwe Sh milioni 3.5 kwa daktari anayeanza kazi
ambaye ikijumuishwa na posho nyingine, atakuwa na mshahara wa Sh milioni
7.7.
Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake
ya mwisho wa mwezi uliopita, aliwaeleza madaktari hao kwamba Serikali
haina uwezo wa kulipa kiwango hicho, na wako huru kutafuta mwajiri
mwingine anayeweza kuwalipa na hivyo hawana sababu ya kugoma.