Wednesday, July 11, 2012

TFF usagaji upo Twiga Stars

Na Tullo Chambo 
KABLA ya kujikita katika mada ya leo, kwanza nichukue nafasi hii kuitakia kila la kheri timu ya Olimpiki Tanzania, iliyoondoka nchini jana kwenda Uingereza kwa ajili kupeperusha bendera ya taifa katika michezo hiyo mikubwa kabisa na ya kihistoria duniani.
Ilianza kama utani, lakini ikaja kuwa mada kubwa miongoni mwa mashabiki wa michezo hususan soka na jamii kwa ujumla.
Ilianza mara tu baada ya timu ya taifa ya soka ya wanawake, ‘Twiga Stars’ ambayo ilikuwa tegemeo kubwa kwa mamilioni ya Watanzania wapenda michezo, kuondolewa katika kinyang’anyiro cha kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Wanawake (AWC).
Twiga Stars ambayo ilikuwa imejiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu fainali hizo, baada ya kuiondosha Namibia kwa jumla ya mabao 7-2, ikiwa imebakiza mechi moja tu dhidi ya Ethiopia, hapo ndipo upepo ulipobadilika.
Twiga, ilijikuta ikiporomoka utendaji wake ndani ya dimba na kujikuta ikiondoshwa na Wahabeshi hao kwa jumla ya mabao 3-1 na hapo ndipo yalipoanza kuibuka mambo.
Lilianza shinikizo la kutaka makocha na viongozi wabwage manyanga, hatimaye Kocha Mkuu, Charles Boniface Mkwasa akaachia ngazi huku akitoa sababu mbalimbali, ikiwamo uwezo wa timu hiyo ndipo ulipoishia na kubeba jukumu la kuwajibika kwa matokeo hayo.
Lakini siku chache baadaye, kocha huyo alinukuliwa na baadhi ya magazeti, ambayo nayo yalinukuu chanzo, ambacho kilikuwa runinga ya Star, kuwa katika timu hiyo kuna vitendo vya mapenzi ya jinsia moja (kusagana) na kuwa waliokuwa wakibainika waliondolewa.
Hapo ndipo mijadala ya kila aina ikaanza kuibuka na kupamba moto miongoni mwa wadau wa michezo.
Jambo la kushangaza na ambalo ni wazi lilitokana na shinikizo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likawaandalia mkutano na waandishi wa habari, viongozi wa Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA), Mwenyekiti wake, Lina Madina Mhando, Meneja wa timu, Furaha Francis, na kocha aliyebwaga manyanga, Mkwasa.
Katika mkutano huo, viongozi hao walipata wakati mgumu kujivua ‘shombo’ la usagaji, lakini kwa mioyo migumu wakajitahidi kuudanganya umma wa Watanzania kuwa hakuna kitu kama hicho katika soka la wanawake.
Kali zaidi ikawa ni kwa Mkwasa, ambaye ndiye chanzo cha kuibuka kwa skendo hiyo, alipita huku na kule kwa kina ndugu zetu flani, ambao hukimbilia kudai ‘nimenukuliwa vibaya’.
Mkwasa akadai amenukuliwa vibaya, hakutamka mambo hayo.
Ni vigumu kuingia akilini, tangu anukuliwe vibaya, takriban wiki na ushehe ipite ndipo asubiri kuandaliwa mkutano na TFF ili kuja kuweka mambo sawa! Alikuwa wapi?
Lakini yote kwa yote, si lengo la Uwanja wa Kuchonga, kumhukumu Mkwasa kama alitoa kauli hiyo au lah...! Lengo hapa ni kuweka wazi ukweli wa kashfa hiyo.
Sijui kama kitaalamu tendo hilo linachangia vipi kuzorotesha ufanisi dimbani au kuchochea ufanisi dimbani kwa wahusika, ila nililotaka kuiambia TFF, isikimbilie kukanusha kwa kujifurahisha tu na si kutibu tatizo.
Nikiwa na uzoefu na ‘ushahidi’ ambao ni vigumu kuuthibitisha kwa kalamu, vitendo vya usagaji vipo katika soka la wanawake, kuanzia ngazi ya klabu hadi timu ya taifa ‘Twiga Stars’.
Wahusika wakihitaji ushauri wa jinsi ya kufanya uchunguzi kuhusiana na hilo, tuko wazi kutoa ushauri, kuliko kukimbilia kulifukia.
Vitendo hivi vya usagaji, vimejenga chuki miongoni mwa wachezaji na hata kubomoa urafiki wa ‘damu’ waliokuwa nao awali, kisa: usagaji; chuki hiyo na kutopendana huenda hadi dimbani.
Haya ni mambo ya ndani katika soka la wanawake na wadau wanayafahamu haya, lakini kina Furaha, Lina na Mkwasa wanakuja kiwepesi na kutaka kuudanganya umma, huku wakidai wamedhalilishwa na kufadhaishwa.
Hapa TFF inapaswa kukaa chini, kuchekecha akili huku wakiongozwa na busara, waunde chombo huru kuchunguza mambo haya na hatimaye kutoa suluhisho kwa manufaa ya michezo hususan soka la wanawake, badala ya kukimbilia kujisafisha.
Namaliza kwa kusisitiza tena, usagaji upo Twiga Stars. TFF chukua hatua.

Source: Tanzania Daima.