Tuesday, July 17, 2012

Spika akemea ‘ugaidi’ wa wabunge

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amekemea kile alichokiita ugaidi unaofanywa na baadhi ya wabunge dhidi ya wenzao wanaoonekana kuwadhibiti kwa hoja.
Kemeo hilo alilitoa jana bungeni mara baada ya kumzuia mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), aliyewatuhumu baadhi ya wabunge wa CHADEMA aliodai wamemtishia kumuua.
Makinda aliwataka wabunge kuacha tabia mbaya na ya kigaidi ya chuki dhidi ya wenzao wanaowazidi kwa hoja bungeni kwenye mijadala yao.
Alisema bungeni watu wanashindana kwa hoja hivyo yeyote anayezidiwa anapaswa kukubaliana na ukweli badala ya kujenga chuki na visasi visivyo na mantiki kwenye jamii.
“Tumeanzisha chuki na tabia mbaya za kigaidi, kinachojadiliwa hapa kinaachwa hapa lakini sasa wabunge wanafikia hatua ya kumtishia mtu kumuua, ni kweli habari za Nchemba ninazo na watu hao walimuandikia ujumbe wa kumtishia kumuua; nawajua, majina yao yamepelekwa polisi, tuwe na heshima jamani,” alisema.
Awali kabla ya Makinda kutoa kemeo hilo, Mwigulu aliomba mwongozo wa Spika akitumia kanuni ya Bunge ya 47 inayohusu kusitishwa kwa shughuli za Bunge ili kujadili jambo la dharura kwa maslahi ya taifa.
Mwigulu alisema kuwa juzi jimboni kwake lilitokea tukio la kinyama ambapo Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM kata ya Ndago kuuawa wakati akitoka kwenye mkuano wa CHADEMA.
“Naomba tuahirishe Bunge tujadili suala hili, kwa kuwa inaonyesha kilichotokea kilipangwa, nilipokea sms (ujumbe mfupi) katika simu yangu za kunitishia kuuawa kutokana na mijadala ninayochangia bungeni na namba za walionitumia sms hizo zimebainika kuwa ni za wabunge wa CHADEMA,” alisema Mwigulu.
Alisema namba za simu zilizokuwa zikitumika kumtumia ujumbe huo mfupi alizipeleka polisi na tayari wabunge hao waliomtishia maisha wa CHADEMA wamebainika majina yao na hatua zaidi zitachukuliwa.
Pamoja na kukataa kuwataja majina wabunge hao, Nchemba nje ya Bunge alionyesha ujumbe mfupi aliotumiwa ambao unasema: “Hivi wewe unajiamini nini? Kwa nini unatuzonga hivyo? Unadhani nchi hii ni ya CCM milele? Utajutia kimbelembele chako. Unadhani ni wewe tu unayejua sana? Ukabila kwenye chama chetu unakuhusu nini hata kama ni kweli kwa nini kututia aibu?”
Ujumbe huo uliendelea, “Hata ufanyeje 2015 tunaingia Ikulu na mjengoni tutajaa, Wangwe alijifanya kujua kama wewe leo yuko wapi?”
Ujumbe mwingine ulisomeka: “Bendera unayovaa kila siku shingoni itageuka sanda yako. Kila mtu ana haki ya kuvutia kwake lakini wewe umezidi. Hatuwezi kuitema keki tuliyokwishaionja.”
Na ujumbe mwingine wa mwisho ulisema, “Fahari yako leo itageuka kilio kwako. Utatutambua.”
Spika Makinda alimzuia Mwigulu kuwataja kwa majina wabunge hao waliomtumia ujumbe mfupi wa kumtishia kumuua na kumtaka aiachie polisi ishughulike na jambo hilo ambapo pia aliukataa mwongozo wa kuahirisha Bunge.
“Kanuni hizi kweli zipo lakini pia katika kifungu kinachoendelea kimetoa masharti yanayosema Bunge litaahirishwa iwapo tu suala litakalojadili utatuzi wake utakuwa mikononi mwake, lakini suala hili la kuuawa kwa Katibu wa CCM hata tukijadili sisi kama wabunge tutafika wapi?” alihoji Makinda.
Alisema taarifa alizonazo tayari polisi imeanza kulifanyia kazi suala hilo ambapo aliwataka kufanya uchunguzi wa kina na watakaobainika kuhusika na mauaji hayo wachukuliwe hatua bila kuonewa.