JESHI la Polisi mkoani Singida, limemkamata na kumfikisha katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida, Mkurugenzi wa Sera na Utafiti
wa Chadema, Waitara Mwita kwa tuhuma za kutoa lugha ya matusi dhidi ya
Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), katika mkutano ambao ulisababisha
mauaji ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)
wa Kata ya Ndago, Yohana Mpinga (30).
Waitara alikamatwa juzi
asubuhi muda mfupi baada ya kumaliza kutoa tamko la chama hicho
kutohusika na mauaji ya kijana huyo na mchana wake alipandishwa
kizimbani, huku vijana wengine sita, wakituhumiwa kwa mauaji ya Mpinga.
Awali,
Mwanasheria wa Serikali, Seif Ahmed alidai mbele ya Hakimu wa mahakama
hiyo, Ruth Masssamu kuwa mnamo Julai 14, mwaka huu saa 10:00 alasiri
huko katika Kijiji cha Nguvumali, Kata ya Ndago wilayani Iramba,
mshtakiwa bila uhalali, alimtusi Mbunge Mwigulu kuwa ni malaya, mzinzi
na mpumbavu, huku akijua kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
Seif
alisema mshtakiwa bila uhalali, alitenda kosa hilo kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nguvumali kwa lengo la viongozi wa
Chadema kuzungumza na wananchi.
Hata hivyo, Waitara alikana kutenda kosa hilo na yupo nje kwa dhamana hadi Julai 30, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Mbali
na Waitara, vijana hao sita wakazi wa Kijiji cha Nguvumali wamefikishwa
mahakamani hapo wakituhumiwa kuhusika katika mauaji ya Mpinga.
Mwanasheria
wa Serikali Mwandamizi, Neema Mwanda aliwataja washtakiwa hao kuwa ni
Manase Daudi (40), William Elia (33), Frank Stanley (20), Charles
Leonard (36), Tito Nintwa na Fillipo Edward (30).
Alidai mbele
ya Hakimu Massamu, kuwa mnamo Julai 14, mwaka huu saa 10:00 alasiri huko
katika Kijiji cha Nguvumali, washtakiwa wote kwa pamoja bila uhalali,
walimpiga kwa kutumia fimbo na mawe mwenyekiti huyo wa UVCCM na
kusababisha kifo chake.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote
kwa vile mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji na
wamepelekwa rumande hadi Julai 30, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.
Wadau walaani
Vyama vya siasa nchini vimetakiwa kufanya
shughuli za kisiasa bila ya vurugu ili kupunguza matukio ya hatari
ambayo yanahatarisha amani kwa wananchi wasio na hatia.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, CCM Tawi la Vyuo Vikuu, Assenga Abubakari alisema
siasa zinazoendelea nchini hazina mwelekeo mzuri.
“Tunapoelekea kama
nchi sipo. Nchi haiwezi kufikia siasa ya kupiga propaganda mpaka watu
wengine wanapoteza maisha, sisi kama wanafunzi wa vyuo vikuu tunawataka
wanasiasa wabadilike waanze kufanya siasa safi,” alisema Abubakari.
Makinda akemea
ugaidi bungeni
Spika
wa Bunge, Anne Makinda jana alilazimika kutumia dakika kadhaa kukemea
kile alichosema kuwa ni vitendo vya ugaidi miongoni mwa wabunge.
Makinda
aliwataka wabunge waache tabia za kigaidi walizozianzisha kwa kutumiana
ujumbe wa vitisho kwa kuwa hiyo ni “tabia mbaya na inaliaibisha Bunge.”
Alisema
wabunge wanalindwa kwa Sheria ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge,
hivyo mtu akisema chochote bungeni kinatakiwa kuishia hapohapo na siyo
kujengeana uhasama na kuanza kupeana vitisho.
Makinda alitoa
maelezo hayo kutokana na ombi lililotolewa na Nchemba kwa kutumia Kanuni
ya 47 akitaka kutoa hoja maalumu ya kujadiliwa kwa dharura vurugu
zilizotokea jimboni kwake na kusababisha kifo cha mtu mmoja.
Spika Makinda alisema suala hilo haliwezi kujadiliwa kwani ameelezwa kuwa polisi wanafanya uchunguzi wa kina.
Alisema
ni muhimu wabunge wakaacha tabia mbaya kwa kuwa wameanzisha tabia za
kigaidi. Alisema wabunge wote ambao wamekuwa wakituma ujumbe wa vitisho
namba zao anazo na kwamba zitawasilishwa polisi kwa ajili ya uchunguzi.
Awali,
Nchemba alisema kutokana na vurugu hizo ambazo zimesababisha kifo cha
msaidizi wake, amekuwa akipokea vitisho vya ujumbe wa simu kutoka kwa
wabunge wa Chadema.
Nchemba alitaka kuwataja wabunge hao na
kusoma ujumbe ambao ametumiwa lakini Spika Makinda alimzuia kwa
kumweleza kuwa polisi wanalifanyia uchunguzi suala hilo.
“Mheshimiwa
Spika ningependa nisome meseji za vitisho ambazo nimetumiwa na wabunge
wa Chadema kutokana na vurugu zilizotokea Singida,” alisema Nchemba.