Friday, July 13, 2012

Ndugulile atimuliwa bungeni

  Agoma kufuta tuhuma zake kwa madiwani 
MBUNGE wa Kigambo, Dk. Faustine Ndungulile (CCM), jana alifukuzwa bungeni na kutakiwa kutohudhuria vikao vitatu, kutokana na kugoma kufuta kauli yake ya kuwatuhumu madiwani wanne wa jimboni kwake kuwa walihongwa na Waziri wa Ardhi ili kuunga mkono ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni.
Hatua hiyo ilikuja baada ya madiwani hao kumwandikia Spika wa Bunge wakilalamika kudhalilishwa na mbunge huyo juzi wakati akichangia hotuba ya wizara hiyo.
Naibu Spika, Job Ndugai, alilieza Bunge jana baada ya kipindi cha maswali na majibu kuwa madiwani hao walitumia kanuni ya 71 ambayo inampa fursa mtu yeyote kuwasilisha bungeni jambo lolote lililomkwaza ambalo limetolewa na mbunge husika.
Ndugai alimtaka Dk. Ndugulile kuthibitisha tuhuma hizo kama atakuwa na ushahidi vinginevyo aifute kauli hiyo na kuwaomba radhi wahusika, jambo ambalo hata hivyo hakufanya baada ya kupewa fursa hiyo jioni.
Katika utetezi wake, Dk. Ndungulile alianza kwa kusema kuwa anaungana na wananchi wake kupinga ujenzi huo wa mji mpya wa Kigamboni kwa kuwa inakiuka sheria ya ardhi inayotamka kuwa ardhi ni mali ya wananchi.
Alisema kuwa sheria inayotumika kwenye mpango wa mji mpya wa Kigamboni ni ya Mipango Miji no. 8 (3) (a) ya Mwaka 2007 ambapo kabla ya kutangaza eneo la uendelezaji, ni lazima mkutano wa hadhara ufanyike kwenye eneo la mradi ili kuomba ridhaa.
“Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nachangia jana niliwataja baadhi ya madiwani wa Manispaa ya Temeke kuwa walipewa rushwa kukubali ujenzi wa mji mpa lakini sikuwataja kwa majina, sasa naomba kujua hao wanaolalamika ni kina nani?” alihoji mbunge huyo.
Alifafanua kuwa mazingira ya madiwani watatu, Suleiman Mathew (Vijibweni), Albert Luambano (Tungi), Doto Msawa (Kigamboni) na Juma Nkumbi (Kibada) waliotambulishwa juzi mbungeni kama wageni wa Waziri wa Ardhi, uwepo wao unatia shaka.
“Waziri anatoka Muleba Kusini, mbona hakualika madiwani wa kutoka huko badala yake anawaalika wa Kigamboni kwenye mgogoro? Hata hivyo madiwani hawa nashangaa kwa nini wako hapa wakati walipaswa kuwa na wenzao kwenye ziara ya mafunzo huko Kilimanjaro. Mazingira haya ndiyo nilisema yanatia shaka,” alihitimisha Ndugulile.
Katika uamuzi wake Ndugai alitumia kanuni ya 74 ikisema kuwa kwa vile mbunge huyo alipewa nafasi ya kudhibitisha tuhuma zake ama kufuta kauli lakini hakufanya hivyo, anamtoa nje ya Bunge asihudhurie vikao vitatu.
Hata hivyo, akizungumza nje ya Bunge, Dk. Ndungulile alidai kuwa ameonewa kwa kufukuzwa kwa vile alichokifanya ni kuwatetea wapiga kura wake wanaopinga mradi huo.
Nao madiwani hao walisema hawatafanya kazi na mbunge huyo aliyewatuhumu kuwa wamehongwa hadi hapo atakapoomba radhi kwa kauli.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, diwani wa kata ya Vijibweni, Mathew, alisema kauli ya Ndungulile inawachonganisha na wananchi wa Kigamboni ambao wanapenda mradi huo isipokuwa wanataka walipwe vizuri.
“Sisi tumekuja hapa kama wanavyokuja wengine, hatujahongwa, hatujanunuliwa…atuombe radhi,” alisema.