Friday, July 13, 2012

Mnyika apelekwa Kamati ya Maadili

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), atafikishwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge baada ya kushindwa kutoa ushahidi wa kuhusika kwa mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba, katika wizi wa Fedha za Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).
Naibu Spika, Job Ndugai, alitangaza hatua hiyo jana bungeni alipokuwa akitoa mwongozo alioombwa na Mwigulu ambaye alitaka kujua hatua zitakazochukuliwa dhidi ya Mnyika.
Mwigulu alisema wiki iliyopita Mnyika alimhusisha na wizi wa EPA uliofanyika wakati yeye (Mwigulu) akiwa chuoni na kiti cha Spika kilimpa Mnyika siku saba kutoa ushahidi dhidi ya tuhuma hizo.
Akitoa mwongozo wake, Ndugai alisema Mnyika alitakiwa apeleke ushahidi wa tuhuma hizo lakini amepeleka maandishi ya utangulizi ila si ushahidi.
“Kwa kuwa siku saba zimepita sasa mwongozo wangu ni…suala hili sasa ninalipeleka katika Kamati ya Haki Maadili na Madaraka ya Bunge, ataandikiwa barua na kamati hiyo ndiyo itakayoshughulikia ushahidi huo,” alisema.
Mapema katika madai yake Mwigulu alisema siku saba alizopewa Mnyika kuthibitisha tuhuma hizo ambazo zililenga kumvunjia heshima kwa chama chake, Watanzania na wapiga kura wake.
“Bunge lako linajua na Watanzania wanajua kwamba wakati tuhuma za EPA zinatokea mimi nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu, nilikuwa bado sijaajiriwa BoT,” alisema.
Baada ya kauli hiyo Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, aliomba kiti cha spika (Ndugai), kimwelekeze Nchemba matumizi halali ya mwongozo wa Spika kwa mujibu wa kanuni 68(7), inahusu jambo ambalo limetokea mapema kikao kinachoendelea.
“Sasa mheshimiwa Spika hili jambo ambalo mbunge analizungumzia lilitokea wiki iliyopita, pili kuna maelekezo tayari yaliyotolewa na kiti chako kwamba mheshimiwa Mnyika alete maelezo ya uthibitisho kwa kiti chako na maelekezo yalishatolewa ningefikiri ni jambo la busara kusubiri ofisi yako iseme kama imepata majibu ama haijapata sasa anachotaka huyu anataka mwongozo wa namna gani?” alihoji.
Hata hivyo, mwongozo wa Ndugai kwa Mwigulu, uliwashangaza baadhi ya wananchi wakihoji imekuwaje jambo hilo litolewe ufafanuzi mapema wakati kuna viporo vingi vya miongozo ya wabunge havijatolewa uamuzi.
Miongoni mwa miongozo iliyokaa kwa muda mrefu ni pamoja na madai ya aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kudai kuwa Waziri Mkuu alilidanganya Bunge kuhusu vurugu za Arusha Januari 5 mwaka jana.
Hadi Lema anavuliwa ubunge na Mahakama Aprili mwaka huu, suala hilo lilikuwa halijatolewa uamuzi, huku madai ya mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafuli ya Julai mwaka jana kuwa baadhi ya wabunge wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa waliomba rushwa kwenye halmashauri nayo hadi leo hayajatolea uamuzi.
Lakini pia vipo viporo vya Tundu Lissu dhidi ya William Ngeleja, Kabwe Zitto dhidi ya Mustafa Mkullo na wengine wengi.
Hata hivyo, Mnyika aliliambia gazeti hili kwamba alichokisema bungeni ni kuwa mbunge aliyemtaja ni mtuhumiwa na alikuwa na tuhuma nyingi ambazo alitakiwa kuzitaja.
Alisema kuwa pamoja na kuomba nafasi ili aweze kuzitaja tuhuma za mbunge huyo hakupewa na badala yake mwenyekiti ambaye alikuwa anaendesha shughuli za Bunge siku hiyo, Jenister Mhagama, akampa siku saba za kutoa ushahidi bungeni.
Mnyika alisema amewasilisha kwa Spika ushahidi wa awali kuhusu tuhuma ambazo alizitoa kwa mbunge mwenzake.
Alisema kuwa kauli ya Naibu Spika Job Ndugai ya kudai kuwa hajawasilisha ushahidi si ya kweli na inalenga kulitumia Bunge kama sehemu ya propaganda.
Hata hivyo, alisema kuwa inashangaza kuona kuwa kuna miongozo mbalimbali ambayo imetolewa siku za nyuma lakini haitolewi majibu mpaka sasa.