Thursday, July 19, 2012

Mbunge: Naweza kumpiga risasi baba

MBUNGE wa Donge, Sadifa Juma Khamis (CCM), amesema yupo tayari kumpiga risasi baba yake iwapo atashiriki kwenye maandamano yasiyo na kibali cha polisi.
Sadifa alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akichangia hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambapo alisema anaunga mkono polisi kutumia silaha za moto kwenye maandamano.
Alisema anapinga michango iliyotolewa na baadhi ya wabunge wenzake ambao walitaka polisi wasiwe wanakwenda kwenye maandamano na silaha za moto.
“Jamani mimi nipo tayari kumshoot (kumpiga risasi), baba yangu kama atakuwa amehudhuria maandamano yaliyokataliwa na polisi, nimepitia jeshini, najua ufanyaji kazi wa polisi.
“Ni lazima polisi apewe silaha za moto kwenye maandamano maana wengine hapa wanayafanya bila kibali, kama mnataka polisi wasiwapige risasi basi fuateni taratibu za kufanya maandamano,” alisema.
Awali kabla ya Sadifa kuchangia hotuba hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Naomi Kaihula (CHADEMA), alilitaka jeshi hilo kutokwenda na silaha za moto kwenye maandamano mbalimbali.
Alisema hivi sasa limekuwa jambo la kawaida kwa askari polisi kwenda katika maandamano wakiwa na silaha za moto ambazo wakati mwingine wamekuwa wakizitumia, jambo linalosababisha vifo na majeruhi kwa waliohudhuria.
Kaihula alibainisha kuwa polisi wanapaswa kutambua wajibu na dhamana yao kwa Watanzania kwa kutoegemea upande wa chama chochote katika utendaji wao.
“Hali ya sasa inaonyesha matumizi ya nguvu ya polisi ni makubwa, polisi wanaogopwa wanapokamata hata kibaka wanatumia silaha kali za moto, lakini pia kuna tatizo la polisi kujihusisha na siasa, vitu hivi viwili vinapaswa vitengane kwani ni tishio kwa usalama wa nchi,” alisema Kaihula.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Chiku Abwao (CHADEMA), aliwatahadharisha polisi kuwa kamwe wasitegemee CCM itaendelea kukaa madarakani milele, kwani ipo siku chama hicho kitang’oka, hivyo ni vema wao wakafanya kazi zao bila upendeleo.
Alisema watawala wa kibaguzi nchini Afrika Kusini walikuwa wakivitumia vyombo vya dola kuwaua wandamanaji na wale waliokuwa wakiupinga utawala huo lakini ulipofika mwisho waling’oka madarakani.