Thursday, July 19, 2012
Maiti 31 ajali ya meli Zanzibar zapatikana
JESHI la Polisi limesema, hadi sasa miili ya watu 31 waliokufa katika ajali ya kuzama kwa meli ya mv Skagit katika kisiwa cha Chumbe imepatikana na baadhi ya hiyo 21 wametambuliwa.
Ofisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi, Zanzibar, Mohammed Mhina, amesema, watu 145 wameokolewa, na kwamba, ilivyofika saa tatu usiku jana, meli hiyo ilizama kabisa. Kwa mujibu wa Mhina, miongoni mwa maiti hizo, 14 ni watoto, 15 wanawake, na wanaume wawili.
Amesema, maiti wamewekwa katika viwanja vya Maisara ili kutambuliwa, na wengi wa walionusurika wanapata tiba katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar Mhina amesema, meli hiyo imezama katika eneo lenye kina cha maji mita 30, na kwamba, jana kulikuwa na mawimbi makubwa, na upepo uliokuwa ukivuma kwa kasi ya kilomita 20 kwa saa.
Waziri Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi,amelieleza Bunge leo kuwa, meli ya Mv. Skagit ilikuwa na watu 290 wakiwemo watu wazima 250, watoto 31 na wafanyakazi wa meli 9.
“Watu 31 waliokufa miili yao imtumbuliwa na ndugu zao na waliookolewa ni 146 na wengine 113 wanatafutwa, “ amesema Waziri Lukuvi.
Lukuvi amesema meli hiyo ilikuwa na watalii 16, 14 kati ya hao wameokolewa, mmoja amekufa na mwingine hajulikani aliko.
“ Serikali zote mbili, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ya Muungano zimetangaza siku tatu za maombelezo. Mazishi ya waliokufa yatafanyika leo,” alisema.
Waziri Lukuvi alisema kituo cha mawasiliano kimefungiliwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya taarifa zinazohusiana na msiba huo.
Amesema, vikosi vya uokoaji vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na vya Jamhuri ya Muungano vinaendelea na juhudi za uokoaji .
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wametangaza siku tatu za maombolezo kuanzia leo, bendera zitapepea nusu mlingoti.
Serikali imesema leo bungeni kuwa, watu 113 waliokuwa kwenye meli iliyopinduka na kuzama jana katika Bahari ya Hindi hawajulikani walipo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi amesema bungeni leo kuwa, vikosi vya uokoaji vinaendelea kuwatafuta na inasadikiwa kuwa wapo kwenye meli iliyozama.
Spika wa Bunge ameahirisha kikao cha Bunge hadi kesho asubuhi ili wabunge na Serikali wapate muda wa kushughulikia ajali hiyo ya kuzama kwa meli ya mv Skagit.
“Hali ipo tete kila mahali, kila mahali kufuatia ndugu zao wapo wapi” amesema Makinda na kuwaeleza wabunge kuwa, idadi ya watu ambao hawajapatikana ni kubwa.
Kabla ya kuahirisha Bunge, Makinda alisema, wabunge 18 walikwenda Zanzibar jana, na kwamba, posho za wabunge wote za kikao cha leo zitapelekwa Zanzibar kushughulikia maafa hayo. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) jana ilisema, meli iliyozama katika kisiwa cha Chumbe, Zanzibar ilikuwa na abiria 248 wakiwemo watoto 31.
Taarifa ya mamlaka hiyo hiyo ilisema, meli hiyo, Mv Skagit iliondoka katika Bandari ya Dar es Salaam jana saa sita mchana, ikiwa na mabaharia tisa.
Kwa mujibu wa Sumatra, meli hiyo, inamilikiwa na Kampuni Seagul Transport, imasajiliwa na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) na kwamba, Cheti cha Ubora kimeanza tarehe 24 Agosti, 2011 na kinamalizika 23 Agosti, 2012. Imesema, meli hiyo ilikuwa imeruhusiwa kubeba abiria wanaoruhusiwa 300 na tani 26 za mizigo.
“SUMATRA kupitia Kituo cha Utafutaji na Uokoaji (MRCC) ilipata taarifa kuwa meli ya MV Skagit iliyokuwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Zanzibar ilikuwa inazama katika eneo la karibu na kisiwa cha Chumbe, Zanzibar, eneo ambalo lipo umbali wa Kilomita za Bahari 13.8 kutoka Bandari ya Zanzibar” imesema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Sumatra, baada ya kupata taarifa hizo, kituo cha MRCC kilitoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na vyombo vya usafiri wa majini vilivyokuwa karibu na eneo la tukio.
“ Zoezi la uokoaji linaendelea katika eneo la tukio kwa msaada wa vyombo vifuatavyo: Mv Flying Horse, Mv Kilimanjaro III, Tug Bandari ya Zanzibar, KMKM, Mv Zanzibar I, Police Patrol Boat, Navy” imesema taarifa hiyo.