Tuesday, July 17, 2012

Kova ampuuza Askofu Gwajima

SIKU moja baada ya Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Dar es Salaam, Josephat Gwajima kuibuka na kukana taarifa zilizotolewa na Jeshi la Polisi kuhusiana na mtuhumiwa Gitu Mhindi kuhusika na tukio la kumteka na kumdhuru Dk. Steven Ulimboka, jeshi hilo limeibuka na kusema litasimamia ukweli kwa kuwa lina uhakika na taarifa dhidi ya mtuhumiwa huyo na zipo kimaandishi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema kamwe hawezi kukanusha taarifa zilizotolewa na jeshi hilo Julai 13, mwaka huu, kwa kuwa walijiridhisha na kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo.

Alisema kamwe jeshi lake halitaki malumbano na viongozi wa dini, kwa kuwa jeshi linafanya doria mchana na usiku kimwili na viongozi wa dini wanafanya doria za kiroho.

“Sisi tupo sambamba na viongozi wa dini wote, tunafanya kazi kwa pamoja, hivyo sihitaji kufanya malumbano na viongozi hawa, ila cha msingi mtuhumiwa amefikishwa mahakamani na tuiachie mahakama ifanye kazi yake,” alisema Kova.

Kuhusu madai kuwa mtuhumiwa huyo ambaye ni raia wa Kenya ana matatizo ya akili, alisema si rahisi kuzungumzia hilo, kwa kuwa anayestahili kuelezea afya ya mtuhumiwa huyo ni daktari na hata kama ana matatizo hayo na amehusika kutenda kosa hilo atashitakiwa kwa mujibu wa sheria.

Alisema anafahamu mambo mengi, lakini amefungwa mdomo na sheria kwa kuwa mtuhumiwa yupo mahakamani, hivyo waache sheria ifanye kazi yake.

Alisema amefuatilia kwa undani kumbukumbu za kipolisi na ushahidi uliopo ndani ya jalada la kipolisi, hivyo kuna mengi lakini si vyema yakaibuliwa hadharani kwa kuwa itakuwa ni kuingilia uhuru wa mahakama.

Aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za kuwanasa watuhumiwa waliomvamia na kumdhuru Dk. Ulimboka.

Wiki iliyopita, Kova alisema wamemkamata mtuhumiwa Mhindi ambaye alikwenda kutubu kanisani kwa Mchungaji Gwajima na alijieleza kuhusika na tukio la kumteka Dk. Ulimboka.

Hata hivyo, mwishoni mwa wiki wakati wa ibada ya kila Jumapili, Mchungaji Gwajima alikanusha taarifa za polisi na kudai kanisa lake halina taarifa za mtuhumiwa huyo ambaye inadaiwa ni raia wa Kenya na hajawahi kuonana naye wala kutubu ndani ya kanisa lake.

Alisema taarifa hizo za polisi ni za kujikanganya na za kulichafua kanisa lake, huku akitoa ushauri polisi wasihusike katika Tume ya Uchunguzi wa sakata la Dk. Ulimboka kwa kuwa nao ni watu wa Serikali.