Monday, July 9, 2012

Ikulu yawajibu viongozi wa dini,Ni waliotaka kutanzua mgomo wa madaktari

SIKU moja baada ya viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu kujitosa katika sakata la mgogoro wa madaktari wakishauri Rais Jakaya Kikwete akutane na madaktari pamoja na viongozi hao ili kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wao unaoendelea, Ikulu imejibu ikisema kuwa hawana sababu ya kupitia kwa watu wengine kuomba kukutana na viongozi wa serikali.
Juzi viongozi hao walikutana na Jumuiya ya Madaktari na wanaharakati jijini Dar es Salaam jana katika harakati za kujaribu kuwasihi wasitishe mgomo ili kuwanusuru wananchi na hivyo kupendekeza kuwa iundwe kamati huru ya kuchunguza tukio la kupigwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, mapema iwezekanavyo ili kupata ukweli wa kilichotokea.
Dk. Steven Ulimboka, yuko nchini Afrika Kusini kwa matibabu baada ya kutekwa na kupigwa na watu wasiojulikana, tukio ambalo lilifanyika siku chache baada ya madaktari hao kuanza mgomo.
Akisoma tamko la viongozi hao, Mkurugenzi wa Baraza la Habari la Kiislamu (Bahakita), Hussein Msopa, kwa niaba ya viongozi hao, alisema kwamba kuundwa kwa kamati huru ya uchunguzi kutasaidia kupata ukweli wa tukio la kutekwa na kupigwa kwa Dk. Ulimboka na kuwezesha kubaini wahusika wa tukio hilo.
“Tukio la kutekwa, kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Pande Dk. Ulimboka ni la kusikitisha… na tunamuomba Rais Kikwete aunde tume huru itakayojumuisha madaktari wenyewe, viongozi wa dini, wanaharakati na wanasheria kubaini kiini cha tatizo hilo,” alisema Msopa.
Hata hivyo, akizungumza na Tanzania Daima jana jioni, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alisema kuwa viongozi hao wa dini mara zote walipoomba kukutana na viongozi wa serikali, akiwemo Rais, hawakupitia kwa mtu yeyote isipokuwa waliomba moja kwa moja na wakakubaliwa.
“Hivyo, hawana sababu ya kupitia kwa watu wengine kuomba kukutana na viongozi wa serikali,” alisema.
Salva aliongeza kuwa mgomo wa madaktari umeisha na walioamua kuendelea na kazi hii muhimu sana ya kutibu binadamu wamerudi kazini, jambo ambalo ni jema sana.
Alisema kuwa sasa si wakati wa kulumbana tena bali ni wakati wa kusonga mbele badala ya kurudi nyuma kwa sababu hakuna mgomo tena wa kujadiliwa.
“Tangu madaktari walipoanza kudai maslahi zaidi, serikali ilifanya jitihada kubwa za kukutana nao. Mbali na Kamati ya Majadiliano ya Serikali, madaktari pia wamekutana na Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kamwe serikali haijapata kukataa kukutana na viongozi wa madaktari,” aliongeza Salva.
Alifafanua kuwa mara ya mwisho madaktari hao walipoitwa kukutana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, walikataa wakidai kuwa waziri hakuwa na jambo jipya la kuwaambia.
Katika tamko lao hilo, pia viongozi hao pamoja na kudai tume huru waliomba serikali kufuta kesi iliyofunguliwa dhidi ya madaktari waliofukuzwa kutokana na mgomo na kuwarejesha kazini ili kumaliza mgomo huo waliodai unaathiri afya za Watanzania.
Kuhusu afya ya Dk. Ulimboka anayeendelea na matibabu katika hospitali moja nchini Afrika Kusini, mmoja wa wanafamilia hiyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema anapata nafuu.
Hata hivyo, ndugu huyo ambaye hakupenda kuzungumza kwa kirefu alionyesha kukerwa na taarifa za vyombo vya habari vinavyoripoti afya ya Dk. Ulimboka kuwa ni mbaya sana, akisema kuwa si kweli.