MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM), Kata ya Ndago wilayani Iramba katika Mkoa wa Singida, Yohana
Mpinga (30), ameuawa kwa kupigwa kwa mawe katika vurugu zilizotokea
katika mkutano wa hadhara wa Chadema, uliokuwa ukihutubiwa na Mbunge wa
Ubungo, John Mnyika.
Mkutano huo ulikuwa umeandaliwa na
Chadema na kufanyika katika Kijiji cha Ndago katika Jimbo la Iramba
Magharibi. Mbali na Mnyika, viongozi wengine wa Chadema waliokuwapo ni
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk Kitila Mkumbo na Mkurugenzi wa
Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Mwita Waitara.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida,
Linus Sinzumwa, alisema katika fujo hizo zilizotokea juzi, Mpinga
alikufa baada ya kutokea fujo na kurushiana mawe kati ya wanachama wa
Chadema na CCM.
Katika mkutano huo kwa mujibu wa madai
ya Kamanda Sinzumwa, viongozi wa Chadema walipokuwa wakihutubia walianza
kumkashifu Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba, hali
iliyosababisha wanachama wa CCM kushindwa kuvumilia hali hiyo na kutokea
fujo.
Sinzumwa alidai katika fujo hizo Mpinga
alipigwa kwa mawe na kupoteza maisha katika nyumba ya Mwalimu Shume
Manase alipokimbilia kuhami maisha yake.
Kutokana na mauaji hayo, watu 18
wanashikiliwa na Polisi kwa ajili ya mahojiano na baada ya upelelezi
kukamilika watu hao watafikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma
zinazowakabili.
Juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya ya Iramba ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Yahaya
Nawanda, alikiri kutokea kwa mauaji hayo. Hata hivyo, Chadema wamedai
hawahusiki na fujo hizo na kudai kushangazwa kusikia habari za
kuhusishwa na fujo hizo wakati uchunguzi haujafanyika ili kuwabaini
waliohusika na fujo hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari,
Mwita alidai mbali na mkutano huo kuwa na baraka za Polisi, lakini pia
walikuwa na taarifa juu ya mpango wa kuvurugwa mkutano huo. Alidai
waliwatahadharisha askari waliokuwapo kwenye eneo hilo kuwa kuna vijana
ambao walikuwa wameandaliwa kufanya fujo ili kuhakikisha kuwa mkutano
huo haufanyiki.
Kwa mujibu wa madai ya Mwita, taarifa
hizo zilieleza kuwa kuna kikundi cha vijana kilichokuwa kimeandaliwa na
kununuliwa pombe pamoja na kukodiwa gari ili kiharibu mkutano huo kwa
kuhakikisha haufanyiki.
Alidai pamoja kutoa taarifa hizo, hakuna
hatua yoyote ya makusudi iliyochukuliwa na Polisi waliokuwapo karibu na
eneo la mkutano, hali iliyosababisha fujo kutokea mara tatu kabla ya
mkutano huo kuendelea na kukamilika salama na wao kuondoka katika eneo
hilo.
“Lakini kutokana na vurugu zilizokuwa
zikisababishwa na kikundi cha vijana ambao tayari walishatolewa taarifa
yao kwenye mkutano huo mbele ya Polisi, askari waliokuwapo hawakuthubutu
kuchukua hatua kwa vijana wale,” alidai Mwita.
Alidai wakati wakiendelea na mkutano huo
na baada ya kutoa taarifa kwa OCD na RPC, askari waliokuwa tayari
kuzuia fujo walifika, lakini tayari fujo zilishatulia na mkutano
uliendelea kama kawaida.
Kutokana na fujo hizo ambazo Mwita
alidai zilitokea mara tatu, waliamua kufungua jalada Polisi lenye namba
NDG/RB/190/2012 na katika jalada hilo walitaja majina ya watu waliokuwa
wakifanya fujo mbele ya mkutano huo kwa lengo la kufanya mkutano huo
usifanyike.
Aliwataja watu aliodai waliohusishwa na
fujo hizo na walionaswa na kamera zilizokuwa zikitumiwa kuchukua
kumbukumbu ya mkutano huo kuwa ni Daniel Sima, Tito Nitwa, Bakili Ayubu,
Yohana Makala Mpande, Ernest Kadege, Abel John, Athumani Ntimbu, Martin
Manase, James Ernest, Simon Makacha, Anthon John na Frank Yesaya.
“Kwa hakika askari wa Ndago waliokuwepo
mkutanoni mbali ya kutochukua hatua yoyote, fujo za sisi kupondwa mawe
zilizidi, askari wote walikimbia akabaki OCS pekee ambaye naye
alionekana dhahiri kutochukua hatua stahili,” alidai Mwita.
Alisema mpaka wanaondoka katike eneo la
mkutano hakukuwa na taarifa yoyote juu ya fujo zilizosababisha mtu
kupoteza maisha na waliendelea na mkutano mwingine katika Kijiji cha
Kinampanda na waliporudi hotelini walipofikia jioni mjini Singida
walianza kusikia taarifa zinazoeleza kuwa kuna mtu au watu wamepoteza
maisha katika mkutano wao wa kwanza.
Mwita alidai Chadema inalaani taarifa
zilizosambazwa kuwa chama hicho kinahusika katika kupoteza maisha ya mtu
huyo kwani hakikujihusisha kwa aina yoyote katika kufanya fujo na muda
wote kilikuwa kikiomba msaada kutoka kwa askari ili kutuliza fujo hizo.
Alisema kutokana na habari
zinazosambazwa kwa kuihusisha Chadema, kuwa kinahusika katika kupoteza
maisha ya mtu huyo, chama hicho kimebaini kuwepo mbinu chafu ya
kuvihusisha vyombo vya Dola katika kuwatisha wananchi ili wasikiunge
mkono katika kuleta mabadiliko ya kweli ndani ya jamii.
Alisema tayari chama chake kimeshapokea
taarifa kutoka Jeshi la Polisi ya kusitishwa kwa ziara yake ambayo kwa
jana ingefanya mikutano miwili katika kijiji cha Shelui na Kiomboi na
wanatii amri hiyo.