Saturday, July 21, 2012

Bosi NBC asimamishwa achunguzwe





BODI ya Wakurugenzi ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imemwomba Mkurugenzi wake Mwendeshaji, Lawrence Mafuru kwenda likizo na amekubali.

Taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Bodi hiyo ilisema, Mafuru anakwenda likizo ya lazima ili kupisha uchunguzi kuhusu matatizo mbalimbali yaliyotokea ndani ya benki hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya NBC, Dk Mussa Assad alisema jana: “Bodi ya Wakurugenzi imepokea tuhuma za ubadhirifu dhidi ya Menejimenti ya Benki hii.

“NBC ni benki inayoheshimiwa na kuaminiwa, hivyo kwa ajili ya utendaji mzuri na utawala bora uchunguzi umeitishwa juu ya suala hilo.” Alisema Bodi yake imeamua kumpeleka Mafuru likizo katika kipindi chote cha uchunguzi ambao unatazamiwa kuchukua muda mfupi.

Alihadharisha kuwa mpaka sasa hakuna hatia yoyote iliyokwishabainika dhidi ya Mafuru au mtendaji mwingine yeyote.

“Nikuhakikishieni, kwamba tuna timu yenye viongozi weledi ambayo inafanya kazi na kutimiza wajibu wake kwa kiwango cha juu cha uadilifu kwa lengo moja tu, la kuhudumia wateja wetu, wa ndani na nje na kufikia malengo ya kibiashara,” alisema Dk Assad.

Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Mafuru alisema: “Naunga mkono uchunguzi wa madai yaliyopo ambayo yametolewa dhidi yangu. Dhamiri yangu iko wazi na natumaini, kwamba baada ya uchunguzi huu, wateja, wadau na wafanyakazi wetu na umma kwa jumla, watathibitisha kwamba benki hii inasimamiwa na kuendeshwa kwa mujibu wa viwango bora vya kiutawala.”

Hatua hii ni mlolongo wa watendaji wakuu wa taasisi nchini kuondolewa au kusimamishwa nafasi zao za utendaji kutokana na tuhuma mbalimbali. Juni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi aliondolewa katika nafasi yake kwa madai ya ukiukaji wa sheria za utumishi wa umma.

Julai 14, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ilimsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Shirika hilo, William Mhando kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.