Tuesday, June 4, 2013

JIFUNZE MAMBO YA FEDHA NA UTAJIRI

 TUJIFUNZE UCHUMI/BIASHARA
ELEWA MAMBO YA FEDHA ILI UJENGE UTAJIRI

·       PESA
·       AKIBA
·       VITEGA UCHUMI
·       MIKOPO
·       UWEKEZAJI KATIKA HISA
·       UWEKEZAJI KATIKA HATI FUNGANI
·       MCHANGANUO WA MAZINGIRA (BUSINESS ENVIRONMENTS)
·       KUPANGA MIPANGO YA FEDHA
·       UWEKAJI HESABU ZA FEDHA
·       KUDHIBITI HATARI/MASHAKA KATIKA BIASHARA
·       WATOA HUDUMA ZA FEDHA
·       MPANGO KAZI


1.       PESA
·       Pesa inapotajwa, kitu gani kinakuja kwenye fikra zako?
·       Pesa ni nini?

Pesa ni chombo cha mabadilishano.,ni thamani inayolingana na bidhaa au huduma iliyobadilishwa na ni fedha halali inayokubalika kwa wananchi wan chi husika.Pesa inatumika kununulia bidhaa na kulipia matibabu,Ankara za simu na umeme au mishahara ya wafanyakazi.Pesa pia inatumika kama kiwango cha thamani cha kupimia thamani ya bidhaa na huduma mbali mbali.Idadi ya vipande vya pesa vinavyotakiwa kununua bidhaa ndio bei ya bidhaa yenyewe.

Pesa pia hutumika kama hifadhi ya thamani ya uzalishaji wa leo wa bidhaa na huduma kwa matumizi ya baadaye.Inawezekana kuwa usumbufu kuweka stoo uzalishaji wa ziada na mara nyingi watu huuza na kuweka pesa wanazopata benki au taasisi nyingine za fedha.Pia wanaweka akiba kwa kununua mali (kama ng’ombe,nyumba,hisa n.k.)

1.1    Chimbuko la pesa
·       Watu walikuwa wakibadilishana vipi bidhaa hapo kale?
·       Pesa imetokea wapi?

Historia ya pesa ni ya miaka maelfu nyuma.watu walizoea kubadilishana bidhaa kupitia biashara ya kubadilishana vitu. Katika uchumi wa kubadilishana mali, mtu mwenye kitu cha kuuza lazima kwanza atafute mtu mwenye kitu kinachokubalika kutolewa ili kibadilishwe.Kwa mfano, mtu angeweza kubadilishana mbuzi wawili kwa gunia moja la mahindi

Muda ulivyosogea, watu wakaanza kutumia vito, chumvi, viungo, pembe za ndovu na makombe kuwakilisha thamani ya vitu vinavyouzwa.Matumizi ya kauri au pembe za ndovu yalikuwa karibu kila mahali kabla binadamu hajagundua jinsi ya kufua madini ya thamani kama vile dhahabu na fedha kuwakilisha thamani ya bidhaa zinazouzwa.Madini haya baadaye yalitengenezwa sarafu na thamani ya sarafu iliamuliwa kwa ukubwa wake.

Katika uchumi wa pesa, mwenye bidhaa anaweza kuiuza kwa pesa, ambayo inakubalika kwa malipo ya bidhaa, kwa hiyo kuepuka muda na juhudi ambazo zingehitajika kumtafuta mtu ambaye atafanya biashara inayokubalika. Pesa ya kisasa iko kwenye mfumo wa sarafu au noti za benki.Pesa ya karatasi ndio mfumo unaotumika zaidi wa pesa halisi.Mfumo mwingine wa pesa ni pesa ya mkopo, ambayo mara nyingi iko kwenye mfumo wa kadi za plastiki (kama vile card za pesa,kadi za mashine za kutolea pesa (ATM)). Pesa ya mkopo inadhaminiwa na ahadi ya mtoaji (iwe ni serikali au taasisi yoyote ya kifedha) kulipa thamani inayolingana katika kiwango cha pesa ya chuma, kama vile dhahabu au fedha.Pesa ya karatasi haibadilishiki kwenye aina nyingine yoyote ya pesa na thamani yake hupangwa na mamlaka ya serikali.

1.2             Sifa bainifu za pesa za kisasa

·       Ni ndogo na inabebeka kiurahisi
·       Inaweza kugawanywa kwenye sehemu ndogo ndogo
·       Inadumu
·       Inakubalika na wote
·       Inarahisisha biashara

1.3             Kwa nini tunahitaji pesa?
Hatuwezi kuzalisha kila kitu tunachohitaji au kufanya kila kitu.Tunahitaji watu wengine wazalishe baadhi ya vitu na kutupatia baadhi ya huduma.Kwa hiyo, tunahitaji pesa ya kununulia bidhaa hizo na kulipia huduma hizo.

Tunahitaji pesa kwa kubadilishana na kile tunachohitaji.tunahitaji pesa inayoendana na mfumo wa maisha yetu

1.4             Tunaipataje pesa?
Tunaweza kupata pesa kupitia njia zifuatazo:
·       Kufanya kazi kwa mshahara au ujira
·       Kuwapatia watu wengine huduma zetu
·       Kilimo na kuuza bidhaa mbali mbali
·       Kufanya biashara
·       Michango au ruzuku kutoka kwa ndugu,marafiki na wengine
·       Pensheni,bonasi na aina nyingine ya fidia
·       Gawio kutokana na akiba kwenye chama cha kuweka na kukopa (SACCOS) au hisa kwenye kampuni zilizomo kwenye soko la hisa la Dar es salaam


1.5             Tunatumiaje pesa
Tunatumia pesa kwa:
·       Matumizi ya kawaida
·       Kuweka akiba
·       Kitega uchumi

1.6             Ni kwa namna gani matumizi ya fedha huleta tofauti?
Pesa kama chombo cha kubadilishana,kinaweza kutumika kuongeza uzalishaji au matumizi.pesa inayotumika kununulia matumizi ya kawaida haiongezi mapato ya baadaye.pesa iliyowekezwa au akiba kwa kitega uchumi cha baadaye inaweza kuleta mapato zaidi.

2.    Akiba
2.1             Akiba ni nini?
Akiba ni pesa au mali za thamani zinazowekwa pembeni au kutunzwa kwa ajili ya matumizi ya baadaye.zinaweza kuwa kwenye mfumo wa pesa taslim, mifugo,chakula n.k. Akiba hutumika nyakati za upungufu au dharura ikitokea.
Kuweka akiba ni kitendo cha makusudi cha kuacha kutumia pesa kwa sasa na kuiweka pembeni kwa matumizi ya baadaye
2.2           Tunawekaje akiba?
        Tunaweza kuweka akiba kwa kuweka pesa kwenye akaunti ya benki ya biashara,akiba na hisa kwenye chama         
         cha kuweka na kukopa (SACCOS) au benki imani au VICOBA au michango ya kupokezana kwa jina lingine
         mchezo (ingawa kisheria sio rasmi).watu wengine wanaweka pesa zao kwenye mifuko ya plastiki (tena ndo  
         wengi kwa sasa hasa wafanyabiashara wa kihindi) na kuificha chini ya kitanda,kwenye mto,nyufa za nyumba
         au kwenye mti.tunaweza pia kuhifadhi mazao kwa matumizi ya baadaye wakati mahitaji yanapokuwa ni
         makubwa.
2.3           kwa nini tunahitaji kuweka akiba?
Vyanzo vya mapato havitabiriki au ni vya msimu hasa kwa watu wanaotegemea ajira au kilimo au hata wafanyabiashara.inatubidi tutarajie matatizo na dharura kiasi fulani kwenye maisha yetu.Akiba inatukinga kutokana na kutumia tukiwa tuna kipato kidogo au hatuna kabisa.tunaweka akiba kwa ajili ya mahitaji ya mzunguko wa maisha kama vile kuzaliwa kwa mtoto na kukidhi mahitaji ya mahali pa kuishi na dharura nyingine kama ugonjwa au kwa mahitaji ya kuwekeza.

2.4            changamoto za aina mbali mbali za akiba
Ni nini faida na madhara ya kuweka pesa nyumbani, benki,SACCOS,mzunguko au kitega uchumi?
2.4.1     kuweka nyumbani
ni hatari sana kuweka nyumbani pesa kwani inaweza kuibwa haraka na kwa urahisi sana.inaweza pia kuliwa na panya,wadudu kama mende au hata kuungua.pia inaweza kutumika kwa matumizi yasiyo ya lazima.katika mifumo ya kifamilia inaweza kutumika vibaya na wanandoa walevi,watoto au hata ndugu wengine wa familia
2.4.2   akaunti za akiba kwenye benki
mabenki yana masharti magumu hasa kwa wale wanaotaka kukopa pesa.aidha, masharti na vigezo vinaweza kuwazuia watu wengi.pia,gharama za huduma za kibenki  ni za juu sana

2.4.3   SACCOS
Ili kuendesha SACCOS mtu anahitaji kuwa na mtiririko thabiti wa mapato kwani michango hufanyika mara kwa mara.uzalishaji kipato miongoni mwa watu hautabiriki na unaweza kukwamisha juhudi za kuweka akiba
2.4.4   Mzunguko (mchezo)
Katika utaratibu wa mzunguko,mwanachama mmoja wa zamu yake na baadaye akakataa kutoa michango kwa wengine.kikundi pia kinaweza kuvunjika kabla ya mzunguko kukamilika.

 
3.       vitega uchumi
watu wana mahitaji mengi zaidi kuliko ambavyo rasilimali zao finyu zinavyoweza kukidhi.wanataka kununua au kujenga nyumba,kununua kipande cha ardhi,kununua chakula,kulipa karo za shule au kuweka pesa kidogo kwa matumizi ya baadaye.pesa huwa haitoshi kufanikisha matakwa yote haya.kutumia pesa kwenye kipengele kimoja ina maana hakuna itakayopatikana kwa ajili ya kingine
tofauti katika utajiri wa watu ,hata kama wanaingiza kipato sawa,kunategemea maamuzi yao ya kutumia pesa.wengine wanapendelea kutumia pesa kwa ajili ya vitu vya anasa vya kila siku kuliko kujipatia mali ili kuzalisha kipato zaidi hapo baadaye.uchaguzi wa kutumia pesa ambao hufanywa na mtu sasa hivi ndio utakaoamua hali ya kifedha hapo baadaye.mtu anayeweka pesa kwenye shughuli inayozalisha atakuwa na kipato zaidi hapo baadaye.

3.1                 uwekezaji ni nini?
Uwekezaji ni kuacha matumizi ya leo kwa ajili ya shughuli ambayo itakuingizia kipato zaidi hapo baadaye.hii ina maana kwamba unachagua kutokutumia pesa yako kwenye chakula,nguo,starehe badala yake unanunua mali ambayo itakuingizia kipato zaidi.uwekezaji maana yake ni kutumia pesa yako katika njia ambazo zitaongeza uwezo wako wa kuingiza kipato.hii inajumuisha kuanzisha au kupanua biashara,kununua mifugo,kununua shamba,kujenga nyumba kwa ajili ya kupangisha,kuwaelimisha watoto n.k.
3.2             tofauti kati ya uwekezaji na akiba
akiba unaweka pesa pembeni kwa matumizi ya baadaye.unaweza kuweka kidogo kidogo hadi kufikia kiasi cha limbikizo kuu
uwekezaji ni kuweka pesa kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.madhumuni ni kuzidisha ulichokuwa nacho leo kwa siku zijazo
3.3             aina za vitega uchumi
3.3.1        vitega uchumi vya muda mfupi
pesa inayowekezwa inatarajiwa kurudisha matokeo (kipato) karibuni.muda unaochukua kabla ya matokeo yanayotarajiwa kupokelewa kawaida ni chini ya miaka miwili.vitega uchumi vinajumuisha kuanzisha biashara n.k
3.3.2     vitega uchumi vya muda wa kati
hivi ni vitega uchumi vinavyochukua miaka kadhaa kabla ya kuanza kupata kipato kutokana navyo.pesa inatarajiwa kuanza kutiririka baada ya miaka miwili;inaweza yote kuja kwa mkupuo au mtiririko wa pesa wa mara kwa mara.mifano, inajumuisha ununuzi wa hisa za kampeni kwenye soko la hisa (stock exchange market) ili kupata gawio au kuendeleza shamba lako kuongeza uzalishaji
3.3.3     vitega uchumi vya muda mrefu
hivi ni vitega uchumi ambavyo vinahitaji pesa nyingi zaidi na kuchukua muda mrefu kukamilisha mradi.mapato yake yanaweza kuanza kutiririka baada ya kukamilika kwa mradi lakini itachukua muda mrefu kabla ya kupata pesa uliyowekeza kwenye mradi.muda utakaochukua kupata pesa yako ni mrefu.vitega uchumi hivi hujumuisha uwekezaji kwenye majengo,kuwapatia watoto elimu,ununuzi wa shamba n.k.
faida ya vitega uchumi vya muda mrefu ni kwamba baada ya muda huongezeka thamani.hii ina maana kwamba ukiwa na kitega uchumi sahihi,utajiri wako utaongezeka wakati ujao.

3.4             kwa nini tuwekeze?
Tunawekeza ili:
·       kujenga utajiri
·       kuongeza uwezo wa kupata kipato zaidi
·       kuanzisha fursa za kuzalisha kipato uzeeni
·       kutengeneza ajira kwetu wenyewe na familia
3.5              wapi na jinsi gani tunaweza kuwekeza?
Kwa kawaida watu wanawaiga wengine wakati wakiwekeza pesa zao.ninafungua biashara ya nguo kutoka uchina,na wewe pia unaamua kufungua biashara ya nguo kutoka uchinia.haya ni makosa.unahitji ufanye tathmini ya fursa mbadala zilizopo.fikiria kitahitajika kitu gani kutoka kwako na kama unaweza kumudu.
3.5.1        jinsi ya kufanya maamuzi ya kuwekeza
kuna njia nyingi unazoweza kuchagua za kuwekeza ambazo,hata hivyo,hazitaweza kukupa matokeo kama ambavyo ungependa.vifuatavyo ni baadhi ya vitega uchumi ambavyo unaweza kuwekeza pesa yako kutegemea na mahali ulipo:
·       kuwekeza kwenye mali ambazo zinapanda thamani kama vile ardhi
·       kuwekeza kwenye miradi/mitaji ya biashara ukitarajia itaongezeka thamani hapo baadaye – hisa.
·       Kuwekeza kwenye mali ambazo zinaanza kuingiza mapato mara moja, kama vile kuanzisha duka au hoteli
·       Kuwekeza kwenye mali ambazo hutoa huduma kwa watu wengine kama vile gari dogo au basi la kubebea abiria au mizigo
·       Kuwekeza pesa kwenye biashara za ubia,kama vile kuanzisha kampuni au ushirika.unapaswa kufanya kazi na watu unaowaamini
·       Kuwekeza kwenye zaidi ya mradi mmoja, kama vile kuwa na shamba na duka kutapunguza hatari ya kufilisika.
Ni muhimu kuzingatia kuwa pesa hupoteza thamani jinsi muda unavyokwenda hasa pesa yetu ya kitanzania.iwapo una shilingi leo unaweza kununua vitu vingi zaidi kuliko utakavyoweza baada ya mwaka mmoja.pesa inadumisha thamani yake ya uwiano inapowekezwa kwenye shughuli ya kuingiza kipato.pesa yako inapaswa ikuingizie kipato wakati wote.
Ili uweze kufanya tathmini ya uwekezaji wako inabidi ukokotoe uwiano wa pesa yako itakavyokuwa hapo kesho na mapato unayotaka kuingiza.kama pesa yako itapoteza kwa 10% kila mwaka hii ina maana kwamba shilingi 100 yako leo,itakuwa sawa na shilingi 110 mwaka kesho wakati huu.kwa hiyo kama unataka kuwekeza shilingi 100 kwa mwaka mmoja inapaswa iwe zaidi ya 110 kwa mwaka ujao,angalau kwa thamani yake kubaki vile vile.kiasi chochote chini ya hapo ni hasara kwako.