Tuesday, September 4, 2012

Wenje asema yupo tayari kutiwa lokapu


MBUNGE wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (Chadema)


MBUNGE wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (Chadema) amesema yuko tayari kukamatwa na Polisi mkoani Mwanza na kutiwa mahabusu kwa kukiuka sheria na kuitisha mkutano wa hadhara bila ya kupatiwa kibali na jeshi hilo.

Wenje alisema hayo juzi jijini hapa alipokuwa akiwahutubia wanachama na wafuasi wa Chadema kwenye uwanja wa Mbugani uliopo jijini hapa, ambapo alisema alifikia uamuzi huo mara baada ya kuahirishiwa mikutano yake mara mbili licha ya kwamba alikuwa akipewa vibali vya kuitisha mikutano hiyo.

“Ni kweli leo (juzi) ni siku ya kwanza kuvunja sheria, tunafanya mkutano bila ya kuwa na kibali cha Polisi na ninaomba iende kwenye kumbukumbu, endapo wataniita kesho niende kituoni sita kwenda, labda wanifuate wao wenyewe na wakinifuata naomba mniletee uji mahabusu,” alisema.

Alisema yeye hakuitisha mkutano kwa sababu ana ujasiri kuliko Polisi na Serikali, bali ameitisha mkutano huo kwa kuwa yeye ni mwakilishi wa wananchi ili awape mrejesho wa mambo yaliyozungumzwa bungeni na mipango iliyoainishwa na Serikali.

“Naomba ifahamike sikuja kuitisha mkutano huu kwa sababu mimi Wenje nina ujasiri kuliko Polisi, nataka niwaambie nimepokea simu zaidi ya kumi kutoka kwa OCD Nyamagana, lakini sikuzipokea. “Ninashangaa niliomba kibali tangu Agosti 21 nikaahirishiwa kwa sababu ya Sensa ya Makazi na Watu nikakubali, lakini baada ya muda huo nikaomba kibali nikaruhusiwa lakini tena mkutano huu nimeambiwa nisifanye,” alisema.

Alisema shughuli za utoaji wa burudani za fiesta zimeruhusiwa kufanya burudani zao na kuhoji yeye kama mwakilishi wa wananchi ni kwanini azuiliwe ilihali alikuwa akizungumza na wananchi juu ya mambo ya msingi ya maendeleo ya jimbo lake.

“Leo fiesta wanaendelea na burudani zao hapa Mwanza, mimi mkutano wangu unazuiliwa kwa sababu ya sensa, mbona huko kwenye fiesta watu wapo mbona wao hawazuiliwi”, alihoji Wenje na kuongeza kuwa kutokana na kuahirisha mikutano miwili kwa muda wa wiki mbili waliingia gharama na hivyo aliona ni vyema aitishe mkutano huo.