Thursday, August 2, 2012

Zitto akana kuhongwa, adai ni mkakati wa CCM kujitakasa

NAIBU Katibu Mkuu wa CHADEMA na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, amesema tuhuma za rushwa zinazoelekezwa kwake ni mkakati wa makusudi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutaka kuaminisha wananchi kuwa ufisadi upo pia ndani ya upinzani.

Zitto amedai kuwa kwa bahati mbaya pasipo kujua wako baadhi ya wabunge wa upinzani nao wameingia kwenye mtego huo wa uzushi wa CCM bila tahadhari kuwa hiyo ni vita ya kisiasa ya kuisambaratisha CHADEMA.

Mbunge huyo alifichua mbinu hizo jana mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuelezea hatua ya tuhuma za rushwa zilizotolewa kwenye majadiliano ya Wizara ya Nishati na Madini.

“Nalazimika kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo la kisiasa zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi nimeshiriki katika vitendo vya rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC). Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi cha kuukanganya umma,” alisema.

Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema anawajibika kuwatoa hofu wananchi kutokana na hisia potofu kwa vile ana dhamana kubwa ya uongozi.

“Mkakati huo wa kuniunganisha na baadhi ya wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea rushwa unatekelezwa na watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakizieneza habari hizo na hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya kauli zangu zinatokana na ushawishi wa rushwa,” alisema.

Alisema kuwa watu mbalimbali wamefikia kuaminishwa habari hizo kiasi cha wengine kuuliza kwanini hakutajwa katika orodha iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, alipowataja wabunge sita wa CCM wanaotuhumiwa kwa rushwa.

Zitto ambaye aliongozana na wabunge 14 wa CHADEMA katika mkutano huo, alisema kuwa hiki ni kipindi cha pili cha ubunge na akiwa mwenyekiti wa POAC, ukiwa ni takriban mwaka wa saba sasa, kwamba kamati yake inasimamia mashirika 259 ya Umma na si TANESCO peke yake.

“Zipo hoja pandikizi za kutaka POAC ivunjwe na hasa zikinilenga mimi binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia mema nchi yetu kuiona POAC ikivunjwa au sura zikibadilishwa, kwa kuwa kamati hii imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi,” alisema.

“Mimi Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili ya uongozi bora katika maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya kunidhoofisha na kunivunja moyo,” alisema.

Aliweka bayana kuwa kwa maoni yake POAC isihusishwe na tuhuma hizo kwa vyovyote vile kwamba yuko tayari ahukumiwe yeye na si kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma hizo mbaya katika historia ya Bunge.

“Nitakuwa tayari kuinusuru POAC na masilahi ya taifa letu kwa kujiuzulu uenyekiti iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa nimehongwa. Kamati ya POAC ni muhimu zaidi kuliko mimi,” alisema mbunge huyo.

Zitto alisema anafahamu kwamba kuna wanasiasa hasa wa upinzani ambao wanautaka sana uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia kutaka kuidhoofisha, lakini wanashindwa kuelewa kuwa anayepanga wajumbe wa kamati ni Spika wa Bunge.

“Msishangae pia kuja baadaye kubaini kwamba baadhi ya wanasiasa wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa kupokea rushwa,” aliongeza.

Zitto alisema baada ya bodi ya wakurugenzi ya TANESCO chini ya uenyekiti wa Meja Jenerali mstaafu Robert Mboma, kutangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu, William Mhando, ili kupisha uchunguzi, POAC ilimuandikia Spika kumuomba aridhie kuwaita Bodi ya TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na pia Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa zifanyiwe uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa.

“Tulifanya hivyo kwani kulikuwa na tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa Mhando siku chache kabla ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kulikuwa na lengo la kufunika ‘madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa sana,” alisema.

Zitto alisema kuwa kitendo hicho cha halali na kwa mujibu wa kanuni kilichofanywa na kamati yake kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu kwamba ni ishara ya kuwa yeye ana masilahi binafsi na TANESCO na hususan Mhando.

“Baada ya tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa gazeti moja alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Waziri Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi, hapa bungeni na wamewaambia kuwa mimi nimepewa rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani na wala kwa lengo gani,” alitanabaisha.

Aliongeza kuwa alijaribu kumtafuta kwa simu Waziri Muhongo na Maswi ili wampe ufafanuzi juu ya yeye na kamati ya POAC kuhusishwa na tuhuma hizo bila mafanikio, hali ambayo alidai inamwondolea mashaka juu ya ushiriki wao katika kueneza au kuthibitisha uvumi huo.

“Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yoyote na uongozi wa TANESCO kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika,” alisema.

Alibainisha kuwa hakuna wakati wowote, popote ambapo yeye binafsi au kamati yao imekataa Mhando kuchunguzwa kwa tuhuma zozote kwamba wanachosisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria, jambo alilodai atalisimamia, iwe masika au kiangazi.

Zitto alisema ni kwa sababu hiyo, amekutana na Spika Anne Makinda na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, juzi na kwamba kwa kujiamini kabisa amewaomba suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa dhidi yake zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kina.

“Nimekwenda mbali zaidi kukiomba chama changu CHADEMA kifanye pia uchunguzi na tathmini yake kwa kina kujiridhisha na tuhuma hizo, natumia fursa hii pia kuomba vyombo vya dola vichunguze tuhuma hizo kwa nafasi yake ili kuweza kupata ukweli.

Zitto alisisitiza kuwa lazima wafike mahali kama viongozi kwamba utaratibu unapokiukwa na yeyote yule, au uongo unapotolewa hadharani waseme bila kuogopa.

Alisema kuwa kwa imani hiyo, hatasalimu amri mbele ya dhamira zao ovu hata atakapobaki peke yake katika mapambano hayo ya kulinda na kutetea rasilimali za taifa zinufaishe Watanzania wote.

Alimtaka Waziri Muhongo kuwaeleza ukweli wananchi kuwa ili mgawo wa umeme usiwepo tena nchini serikali itapaswa kulipa sh bilioni 42 kila mwezi kwa kampuni binafsi za kufua umeme za IPTL na Symbion, ukweli ambao alidai utakuja kujulikana wenyewe muda si mrefu.