Friday, August 24, 2012

Watakaokuwa gesti kuhesabiwa usiku



OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imewatahadharisha wananchi kote nchini kuwa hakuna kaya zitakazohesabiwa usiku wakati wa Sensa ya Watu na Makazi.

Imesema kuwa sensa katika kaya zitafanyika Jumapili kuanzia saa moja asubuhi huku usiku wake ikifanyika katika sehemu zenye mikusanyiko ya watu kama nyumba za kulala wageni na hosteli.

Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu wa NBS, Radegunda Maro alibainisha hayo jana wakati akijibu maswali ya wananchi alipozungumza na Radio Tumaini inayorusha matangazo yake kutoka Dar es Salaam.

Hivyo mkurugenzi huyo aliwataka wananchi kutokubali kuwafungulia mlango katika kaya mtu yeyote atakayegonga usiku kwa kujifanya kuwa ni mtu wa sensa.

“Hii itasaidia kwa wale wanaoishi maeneo yasiyo salama ambayo baadhi ya watu wasio wema watataka kutumia siku hiyo kufanya vitendo vya ujambazi kwa kutaka wafunguliwe kwa madai ni watu wa sense,” alisema Maro akimjibu wananchi aliyeonesha wasiwasi kuhesabiwa usiku katika kaya.

Pia Maro alisema kwa asubuhi mawakala hao watakuwa wameambatana na wajumbe wa Nyumba Kumi watakaosaidia kuonesha nyumba ili kuepuka kuchanganya na kuhesabu mara mbili huku karani akiwa na kikoti chenye nembo ya Sensa ya Watu na Makazi 2012.

Alisema karani pia atakuwa na kitambulisho chenye picha yake na nembo ya sensa na watakaolala kwenye nyumba za kulala wageni, wahakikishe wamejaza fomu itakayokuwapo katika nyumba hizo.

Alisema kwa wajumbe wa Nyumba Kumi, watahusishwa kuanzia leo baada ya makarani kupewa vifaa na kuingia mitaani kwa ajili ya kutambua nyumba na sehemu zenye mchanganyiko wa watu.

Awali, Balozi mmoja wa Nyumba Kumi, Salum Rajab kutoka Kinyerezi alilalamika kutoshirikishwa kwao, ikiwa ni pamoja kutoelekezwa kazi zao watakazofanya katika tukio hilo muhimu kwa nchi.

Akizungumzia malipo kwa makarani, Maro alisema kuanzia jana walihakikisha makarani wote wanalipwa fedha zao zote zilizobaki pamoja na kuanza kuwalipa fedha kwa ajili ya sensa kama walivyosaini mikataba.

Alisema kwa mujibu wa mikataba yao, watalipwa nusu ya fedha yote halafu baada ya kumaliza kazi na kukabidhi watamaliziwa malipo yaliyobaki baada ya kukaguliwa na kuhakikisha wamefanya vizuri.