Ni juu ya uteuzi wa Kadhi Mkuu
TAASISI ya Kiislamu ya Imam Bukhary iliyo chini ya Mwenyekiti, Sheikh Khamis Khalifa, imesema kuwa utaratibu uliotumiwa na Mufti wa Tanzania, Shaaban Simba, katika kumteua Kadhi Mkuu ni sahihi na hauna shaka yoyote kwa kuwa umezingatia na kutimiza matakwa ya sharia za Kiislamu.Tamko hilo limekuja ikiwa ni siku moja tangu jopo la masheikh 25 kutoka taasisi na jumuiya mbalimbali za Kiislamu Tanzania, kusambaza tamko la kupinga uteuzi wa Mufti hivi karibuni.
Sheikh Khalifa alisema ni jambo la kushangaza na kuhuzunisha kwa jopo la masheikh 25 kupinga utaratibu uliotumika katika uteuzi wa kadhi wakati ndiyo huo ambao wao wenyewe waliuelezea kuwa unaokubalika kwa mujibu wa madhehebu ya Imam Abu Hanifa na Imam Shafii, ambapo Waislamu wa Tanzania asilimia 99.9 ni wa madhehebu ya Shafii.
Alisema jopo hilo liliwahi kutoa tamko katika vyombo vya habari Agosti 13 na 16 mwaka huu kuwa mwenye mamlaka ya kumteua kadhi katika dola ya Kiislamu ni Khalifa, sultan au rais kwa vile ndiye mwenye haki kimsingi ya kufanya kazi anazostahili kufanya kadhi.
“Tamko la masheikh hao lilisema kwa mujibu wa Fik’hi (sheria) ya Kiislamu kwa kufuata madhehebu ya Imam Abu Hanifa na madhehebu ya Imam Shafii, iwapo Waislamu watahitaji kuwa na kadhi katika nchi ambayo haitawaliwi kwa misingi ya Kiislamu, basi kabla ya kumteua kadhi atachaguliwa Amiri, yaani kiongozi wa Waislamu wa nchi nzima na huyo ndiye atakayekuwa na uwezo wa kumteua kadhi akishauriana na wanazuoni (masheikh) na watu wenye busara, kwa nini sasa wampinge?” alihoji.
Sheikh Khalifa aliongeza kuwa kwa mujibu wa utararibu huo, kiongozi aliyechaguliwa kuwaongoza Waislamu wa Tanzania nzima kwa uwakilishi wao ni Mufti Sheikh Simba, ambaye alichaguliwa kwa uwakilishi wa masheikh kutoka mikoa na wilaya zote za Tanzania Bara na ndiye mwenye jukumu la kumteua kadhi pia.
Alisema ni jambo la fedheha na aibu kwa jopo hilo kujaribu kuwahadaa Waislamu kuwa utaratibu haukufuatwa huku wakiuficha ukweli kuwa sababu ya kupinga ni kutokana na aliyeteuliwa hatokani na kikundi chao cha Answar Sunna.
Alisema katika taarifa yao wamedanganya kwa kudai kuwa kadhi alistahili kuchaguliwa na taasisi, wakati tamko lao wenyewe linasema wazi kuwa anayestahili kumteua kadhi ni kiongozi mkuu aliyechaguliwa kuwaongoza Waislamu katika nchi husika.
”Hakuna mahala popote katika Sharia ya Kiislamu panapohusisha wingi wa taasisi katika uteuzi wa kadhi bali Sharia inaonesha mwenye uwezo huo ni mtawala wa dola au kiongozi mkuu wa Waislamu aliyechaguliwa katika nchi husika.
“Hata hivyo, ingawa sheria inampa uwezo wa kumteua kadhi japo na washauri wake wachache, Mufti Simba alimteua Kadhi Mkuu, Sheikh Abdallah Mnyasi, kwa ushauri wa tume ya dini nchini, ambayo inajumuisha wajumbe wa Baraza la Ulamaa taifa pamoja na masheikh wa mikoa na wilaya zote hapa nchini,” alisema Sheikh Khalifa.
Aidha, aliwataka Waislamu kote nchini kumtambua Kadhi Mkuu ambaye ni mwazuoni aliyebobea katika elimu ya Sharia ya Kiislamu, na kupeleka mashauri ya Kiislamu kwenye mahakama hiyo ili kupata uamuzi wa kisharia.
Sheikh Khalifa alisema ni vema kwa Waislamu kupuuza propaganda za kikundi hicho cha masheikh wa Kiwahhabiyya ‘Answar Sunna’ ambacho kinapinga uteuzi wake baada ya kuwatupa nje masheikh wao.
Alisema kuwa hapa nchini maanswar Sunna ni kikundi cha watu wachache kilichozuka siku za karibuni, ambacho kila wakati kinajihusisha na vurugu miongoni mwa Waislamu watulivu kila mahala walipo.
“Hivyo haiwezi kuwa busara kwa Kadhi Mkuu atokane na kikundi hiki ambacho hata utaratibu wao wa kidini unatofautiana na Waislamu asilimia 99 katika nchi hii,” alisema Sheikh Khalifa.
Aliongeza kuwa masheikh hao wanatakiwa wajitambulishe kwanza wao ni wafuasi wa madhehebu gani na wanataka kadhi ateuliwe kwa kufuata utaratibu upi kisha wakae kikao chao na wafuasi wao wamteue kadhi wao atakayehusika na mashauri yao kuliko kupoteza muda.