Tuesday, August 7, 2012

Ufisadi fedha za JK watikisa Bunge

UFISADI wa fedha za Serikali zaidi ya sh bilioni tatu zilizotengwa kwa ajili ya safari za nje za Rais Jakaya Kikwete, zimelitikisa Bunge.

Mjadala wa wizi wa fedha hizo ulioibuliwa na baadhi ya vyombo vya habari mwezi uliopita, uliibuka jana Bungeni baada ya kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kumtaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG), kufanya uchunguzi wa kina kuhusu kashfa ya fedha za posho za safari ya rais.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ezekia Wenje alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara hiyo.

Alisema, suala hilo lina utata kwani hivi karibuni Waziri Benard Membe alijitokeza na kusema suala hilo litafanyiwa uchunguzi, lakini baada ya siku chache akasema uchunguzi wa awali umebaini fedha hizo sh bilioni 3.5 zilizotengwa kwa ajili ya safari za rais ndani na nje ya nchi, zipo salama na hazijaibwa, kilichojitoeza ni kasoro na taratibu za fedha zilizokiukwa na hakuna dalili zote za wizi.

“Kamabi ya Upinzani inataka kusikia kauli ya serikali juu ya tuhuma hizi za ufisadi ambazo sasa unaonekana kukithiri hadi kwenye fedha za rais za safari, kwa sababu inaonekana dhahiri kauli za waziri zinajichanganya, hatujui lengo lake, hivyo tunataka uchunguzi wa kina,” alisema.

Hata hivyo, Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Ulinzi na Usalama, imesema kuwa suala hilo limeshaundiwa tume ya uchunguzi kwa lengo la kuchukua hatua stahiki.

Akisoma hotuba ya kamati hiyo, Mjumbe Betty Machangu aliipongeza serikali kwa hatua hiyo.

Aidha, alisema kutokana na kuwepo kwa tuhuma za wizi wa fedha kwa ajili ya viongozi, kamati inaishauri wizara kuongeza umakini katika usimamizi wa fedha za umma kudhibiti matukio ya wizi.