Friday, August 24, 2012

Nyumba 300 zabomolewa Mabwepande



NYUMBA takribani 300 zikiwemo za kifahari, zimebomolewa baada ya kubainika kujengwa katika maeneo mbalimbali yaliyovamiwa katika Kata ya Mabwepande na Madale wilayani Kinondoni, mkoani Dar es Salaam.

Operesheni ya kuwaondoa wavamizi wa mashamba iliyoanza jana saa 12 asubuhi, ilifanywa na Serikali ya Wilaya ya Kinondoni chini ya ulinzi mkali wa askari polisi waliokuwa na magari yapatayo 30 yakiwamo matingatinga manne na gari la wagonjwa.

Baada ya kuanza operesheni hiyo, kulitokea tafrani kidogo baada ya wananchi waliokuwa katika vikundi kutumia silaha za jadi kama mishale, mapanga kuwashambulia polisi, jambo lililolazimu jeshi hilo kutumia mabomu ya machozi katika kuwatawanya.

Katika operesheni hiyo iliyofanyika kwa awamu, wananchi ambao maeneo yao yalivamiwa, walikuwa wakiongoza kuonesha wavamizi na kisha kubomolewa nyumba na baadaye kuchoma moto nyumba hizo zilizokuwa zimejengwa kwenye eneo hilo ambalo lina vilima vingi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema wametumia nguvu ya wastani katika kusimamia operesheni hiyo na watu takribani 20 wanashikiliwa na jeshi hilo baada ya kuanzisha vurugu.

“Tulipata upinzani kidogo wakati tunaanza, jambo ambalo tulilazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya na kuendelea na kazi hiyo. Kazi imefanyika vizuri na hakuna askari wala raia yeyote aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa,” alisema Kamanda Kenyela ambaye katika awamu ya pili ya bomoabomoa, alitaka kusiwapo na uchomaji moyo nyumba zilizobomolewa.

Alisema katika operesheni hiyo, wamekamata mitambo ya pombe haramu ya gongo na walichobaini ni kuwa eneo hilo lilikuwa maficho ya wahalifu wa ubakaji, ukabaji na ujambazi uliokuwa ukifanyika hapo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema eneo hilo limekuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu na kuwa kazi waliyoifanya ni kuwaondoa wavamizi wapya katika eneo hilo lililovamiwa la kata za Mabwepande na Madale.

“Mgogoro wa hapa ni tofauti, zamani kulikuwa na tatizo la umilikaji wa watu zaidi ya mmoja katika eneo moja, lakini sasa kuna kundi la vijana ambao wanavamia maeneo ya watu na baadaye wanayauza, wengi wa waliobomolewa ni wale waliouziwa na wavamizi,” alisema Rugimbana.