Friday, August 17, 2012

Mkuu wa shule ampa mimba mwanafunzi



MKUU wa Shule ya Sekondari ya Mgaga Wilaya ya Bahi, Dodoma, Daniel Mzula (30), anashikiliwa na Polisi kwa kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha nne shuleni hapo.

Kwa sasa mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 17 (jina linahifadhiwa) anadaiwa kuwa na ujauzito wa miezi sita.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa hatua ya kumkamata mtuhumiwa huyo ilitokana na taarifa zilizotolewa na baba wa mwanafunzi huyo aliyekuwa akitafuta msaada kwa mkuu huyo wa wilaya baada ya kutoa taarifa za mwanawe kupewa ujauzito na mwalimu, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya mwalimu huyo.

Mkwasa alisema kutokana na madai ya baba wa mwanafunzi huyo kuwa alipitia ngazi zote kuanzia Ofisi ya Kata na hatimaye kutoa taarifa shuleni, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

“Baba wa msichana aliomba msaada kwangu baada ya kuona kuwa hatendewi haki, licha ya kudai mkuu wa shule amempa mimba mtoto wake na alikuwa akiomba kama anaweza kusaidiwa mtoto wake angalau afanye mtihani kwani sasa mimba yake ilishafikisha miezi sita,” alisema Mkwasa.

Alisema kulingana na maelezo ya baba wa mwanafunzi Polisi walifanya uchunguzi baada ya kumhoji mwanafunzi huyo na ndipo alipomtaja mwalimu huyo kuwa alikuwa amempa ujauzito.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Bahi, ambaye hata hivyo hakutaka kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji wa Jeshi la Polisi, alikiri kushikiliwa kwa mwalimu huyo.

“Ndiyo anashikiliwa hapa kituoni, lakini siwezi kusema lolote juu ya hili kwa kuwa mimi si msemaji, wasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa Zelothe Stephen ndiye msemaji,” alisema OCD.