Friday, August 24, 2012
Madaktari wagoma kuhojiwa kuhusu Ulimboka
JUMUIYA ya Madaktari Tanzania, imesema hawako tayari kuhojiwa na tume iliyoundwa na Jeshi la Polisi nchini kuchunguza tukio la kutekwa, kupigwa na kutelekezwa kwa Mwenyekiti wao, Dk. Steven Ulimboka, kwa vile hawana imani nayo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu wa jumuiya hiyo, Dk. Edwin Chitage, alisema kuwa mazingira ya tukio lililompata mwenyekiti wao yanahusisha njama za makusudi zilizofanywa na polisi, hivyo wanahitaji tume nyingine huru zaidi watakayoweza kuipa ushirikiano.
“Tangu awali tulisema hatuna imani na tume ile, sasa hatuwezi kuipa ushirikiano… kisipoundwa chombo huru basi tutajua cha kufanya, tunataka hiyo tume iwe na wajumbe huru wanaoaminika ili waje na majibu sahihi, kwa sasa hapana.
“Hivi tume iliyoundwa na polisi walioteuliwa na serikali ambayo viongozi wake wanasema hawahusiki na kipigo cha mwenyekiti wetu unafikiri hao wajumbe wa tume wanaweza kuja na majibu ya kweli?” alihoji.
Chitage aliongeza kuwa katika mazingira hayo wajumbe wa tume hawawezi kuja na majibu ya kweli wakati wakuu wao serikalini wamekanusha kabla tume haijamaliza kazi.
Alibainisha kuwa msimamo wao kuhusu madai yao haujabadilika hivyo wataendelea kudai mazingira bora ya kazi na haki za watumishi wa sekta ya afya.
Alisema madaktari kwa sasa wamechoshwa na mazingira ya kukatisha tamaa wanayofanyia kazi, mrundikano wa wagonjwa, ufinyu wa vifaa tiba na dawa.
Usiku wa kuamikia Juni 27 mwaka huu, Dk. Ulimboka alitekwa na watu wasiojulikana, akapigwa na kutelekezwa msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na watu wanaodaiwa kuwa watumishi wa serikali.
Source:Tanzania Daima.