Wednesday, August 22, 2012

Lowassa: Enzi ya Mkapa tuliyaona maisha bora

ALIYEKUA Waziri Mkuu, Edward Lowassa amempongeza Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kwa kusimamia maamuzi yake hali iliyosaidia kuboresha uchumi wa nchi.

Lowassa ambaye ni mbunge wa Monduli, alisema licha ya kulaumiwa wakati wa utawala wake, Mkapa alisimamia uamuzi wake na wananchi waliyaona maisha bora kwa kuwa mfumuko wa bei ulikua ‘dijiti’ moja, lakini sasa umepanda hadi asilimia 17.9.

Akizungumza juzi kwenye kipindi cha dakika 45, kinachorushwa hewani na kituo cha ITV, mbunge huyo alisema tatizo lililopo serikalini hivi sasa ni viongozi kushindwa kuchukua uamuzi na kuusimamia bila kuogopa lawama kama alivyofanya Rais Mkapa.

“Lazima tufanye maamuzi na kuyasimamia… Rais Mkapa wakati wake alifanikiwa kwenye hilo, aliyasimamia, watu walimlaumu wakamwita Ukapa, lakini uchumi ulisimama na wote tulishuhudia.

“Bila serikali kupunguza matumizi na kujikita kwenye kilimo cha mashamba makubwa, tutaendelea kuwa maskini… jembe la mkono haliwezi kututoa. Hata wakati wa Yesu watu walitumia wanyamakazi,” alisema Lowassa aliyetakiwa kutoa tathimini yake kuhusu uchumi wa nchi hivi sasa.

Awali, alikiri kukua kwa uchumi kutokana na ujenzi wa barabara za lami kwa sehemu kubwa ya nchi, huku akisisitiza kwamba haujafika kwenye mifuko ya wananchi kwa vile mfumuko wa bei upo juu.

Muda mwingi wa mahojiano yake, Lowassa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia mambo ya nje, ulinzi na usalama aliitaka serikali kuhamasisha kilimo cha mashamba makubwa na matumizi ya zana za kisasa za kilimo.

“Serikali isimbane mkulima mdogo, imwache auze mazao yake popote alipo kwa ghamara nzuri, hii itamhamasisha na kuongeza bidii kwenye uzalishaji wake akiamua hata kuuzia Kenya,” alisema mbunge huyo.

Mafuta na Gesi

Kuhusu kugundulika kwa rasilimali ya mafuta na gesi hapa nchini, mwenyekiti huyo ambaye hivi karibuni aliunga mkono kauli ya serikali kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi, alisema isiposimamiwa vema uwepo wake utakuwa laana kwa Watanzania.

“Hii ni rasilimali nzuri kwetu, tukiisimamia vema itakuwa neema na tukiisimamia vibaya itakuwa laana… hatuna haraka ya kugawa vitalu vyote vyenye gesi.

“Tungojee tusiwe na haraka kama alivyofanya Mwalimu Nyerere baada ya kugundua kwamba kuna madini aliyaacha kwanza na leo yanatusaidia, wapo watakaoniona mjinga, lakini ‘am not a fool’ (mimi si mjinga),” alisema Lowassa kabla ya kuhitimisha mazungumzo yake.

Kuhusu balozi zetu

Lowassa alisema, tatizo la fedha linazikabili balozi za Tanzania nje ya nchi na watendaji wake ambao wakati mwingine hukaa hadi miezi mitatu au sita bila kupata mshahara.

“Nirudie kusema ucheleweshaji wa maamuzi ni kikwazo mfano pale New York jengo la ubalozi wetu linatakiwa kukarabatiwa, fedha inayotakiwa ni dola milioni moja ambapo likiwa zuri tuna uwezo wa kulipangisha kila mwezi tutapata dola 400,000, lakini hadi sasa lipo tu linazidi kuharibika.

“Pale London, pia kuna kiwanja chetu kinavamiwa na vibaka ambao wakikaa pale kwa wiki mbili, kuwaondoa lazima uende mahakamani, hizi zote ni mali ambazo zinahitaji maamuzi tu zifanyiwe kazi.

“Tunao uwezo wa kuwaambia NSSF wajenge balozi zetu huko nje tuwalipe taratibu, lakini maombi yalipelekwa wizara ikakataa kwa kutumia sheria fulani fulani, lakini si sahihi kutegemea fedha za bajeti kuu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za serikali,” alisema.

Kuhusu afya yake

Lowassa alianza kwa kuwalaumu waandishi wa habari wanaopotosha kuhusu afya yake kwamba amepata kiharusi huku akikanusha kwamba alikwenda nchini Ujerumani kwa kutizama afya yake na kufanyiwa uchunguzi wa jicho.

“Nashangazwa na ‘speed’ ya kuandika uongo kuhusu afya za watu, siumwi na wala sijapata kiharusi, nipo fiti kwa jambo lolote,” alisisitiza Lowassa ambaye Machi mwaka huu safari yake ya Ujerumani ilizusha hofu juu ya afya yake.

SOURCE: TANZANIA DAIMA

Kama umeipenda SHARE NA WENZAKO