WAKATI mgomo wa walimu ukiingia siku ya tano leo, Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa madai yao hayatekelezeki.
Rais aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Madai ambayo walimu wamekuwa wakiitaka serikali kuyatafutia ufumbuzi ni pamoja na ongezeko la mishahara kwa asilimia 100, posho ya kufundishia kwa walimu wa Sayansi asilimia 55, asilimia 50 kwa walimu wa masomo ya Sanaa na asilimia 30 posho kwa walimu wanaoishi katika mazingira magumu.
Katika hilo rais alisema: “Mgomo si jambo zuri na linanisononesha lakini sitaki kuzungumzia sana hili kwa sababu kesho (leo) mahakama itatoa uamuzi juu ya kesi hiyo.
“Lakini napenda kuwahakikishia walimu kuwa tunawajali sana, tunawathamini, tunatambua mchango wao hata mimi ninayeongea hapa ni kazi ya walimu… kwa hiyo hatuwezi kuwapuuza,” alisema Kikwete.
Akifafanua kwa nini madai hayo ya walimu hayatekelezeki, Rais Kikwete alisema ni makubwa na yanazidi uwezo wa serikali.
Alisema endapo watakubali kuyatekeleza madai ya walimu, serikali itatumia shilingi trilioni 6.574 (karibu trilioni 7) kwa ajili ya kulipana mishahara wakati uwezo wa serikali kukusanya mapato ni trilioni nane.
Hivyo alisema haiwezekani mapato yote ambayo serikali inakusanya yakatumika kwenye kulipana mishahara.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, endapo serikali itaamua kulipa mishahara kwa kiwango hicho kuna hatari ya mapato yote yakatumika huko na kuacha miradi mingine ya maendeleo pamoja na huduma za kijamii.
“Tukifanya hivyo, utatokea mgomo wa wananchi…hawatapata maji, dawa, barabara na huduma nyingine…tufike mahali tuseme kuna ukomo wa kulipana,” alisema Kikwete.
Kikwete alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa walimu walio tayari kufundisha kuendelea kufanya hivyo na kuonya baadhi ya walimu wanaowatisha wenzao walio radhi kufanya kazi.
Mbali na hilo, Rais Kikwete alionekana kukerwa na tabia ya walimu waliogoma kuwatumia watoto wadogo kuandamana na kusema kuwa: “ Jamani hakuna mtoto mdogo hapa sote tuna akili, hivi ni mtoto gani anaweza kuandamana na kwenda kulala barabarani yeye mwenyewe, hili si jambo jema, wadai haki yao lakini watoto wawaache”.
Rais Kikwete pia alisema wakati wote wamekuwa wakiyafanyia kazi madai ya walimu pamoja na kutekeleza haki zao ikiwa ni pamoja na kukaa pamoja katika meza ya mazungumzo.
Hata hivyo alionekana kusikitishwa na kitendo cha Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kumuandikia barua siku ya Ijumaa na kuikabidhi kwa Katibu Kiongozi wakati wakijua kwamba Jumamosi na Jumapili hakuna kazi.
“Jamani hii ni sawa na yule mtu ambaye anakupeleka polisi siku ya Ijumaa wakati anajua Jumamosi na Jumapili huwezi kutoka mpaka Jumatatu wakati wa siku ya kazi,” alitania na kuongeza kuwa: “Narudia kusema tena hatuwapuuzi walimu ila madai haya ni magumu, tuendelee kuzungumza, turudi kwenye meza ya mazungumzo.”
Julai 29, mwaka huu, CWT walitangaza kuanza mgomo usio na kikomo, hatua ambayo ilikuja ikiwa ni siku moja baada ya serikali kutangaza kuwa mgomo huo ni batili.
Tayari mgomo huo umesababisha athari kubwa nchi nzima, baada ya wanafunzi kukosa masomo kwa takriban siku tano sasa.
Leo Mahakama Kuu kitengo cha Kazi itatoa uamuzi kuhusu kesi iliyofunguliwa na serikali kuzuia mgomo huo wa walimu.
Serikali ilifungua kesi hiyo kupinga mgomo huo ulioitishwa na CWT, kwa madai kuwa ni batili kwa sababu ulikiuka sheria.
Katika kesi hiyo, serikali inadai kuwa CWT ilitumia sheria ya utatuzi wa migogoro ya wafanyakazi wa serikali namba sita, kifungu cha 26, inayotumiwa na wafanyakazi wote wa umma na wengine badala ya kutumia sheria ya majadiliano ya pamoja ya utumishi wa umma ya mwaka 2003.
Pia inadai kuwa katika sheria waliyotumia inataka kutoa notisi ya saa 48 badala ya ile ya watumishi wa umma ambayo inawahusu walimu ambao ni kundi maalumu, ambayo ingetoa notisi ya siku 60.
Mgogoro mwingine kati ya CWT na serikali umedumu kwa zaidi ya miaka mitano sasa, ambapo licha ya ahadi ya kulipwa madai hayo, fedha zimekuwa hazikidhi ukubwa wa tatizo na kusababisha madeni kurundikana.