Tuesday, August 21, 2012
Jahazi lazama likienda Zanzibar
Jahazi
WATU wawili hawajulikani waliko huku 10 wakiwamo watalii watatu kutoka Uholanzi wakiokolewa baada ya jahazi lenye jina la mv Salwat kuzama likiwa njiani kutoka Tanga kwenda Zanzibar.
Polisi na Mamlaka ya Safari za Majini, walithibitisha jana, kutokea ajali hiyo Jumapili usiku katika bahari ya Hindi.
“Ajali hiyo ilitokea Jumapili jioni, lakini kwa bahati nzuri waokoaji kutoka Tanga na Zanzibar walifika eneo la ajali mapema na kuweza kuokoa watu 10. Wawili bado hawajaonekana. Jahazi hilo lilizama,” Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Safari za Majini Zanzibar (ZMA), Abdallah Kombo alisema jana.
Chombo hicho kiling’oa nanga katika bandari ya Tanga saa nane mchana Jumapili kikienda katika bandari ya Mkokotoni, Zanzibar, lakini kilipofika eneo la Maziwe karibu na Pangani mkoani Tanga, kilipigwa na wimbi kubwa na kupinduka.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, jahazi hilo lilikuwa na majaketi okozi ya kutosha ambayo yalitumiwa kuokoa maisha ya abiria hao wakiwamo raia wa Uholanzi, huku waliopotea wakiwa ni mwanamke na mwanamume.
“Utafutaji wa waliopotea unaendelea,” alisema Kombo huku Kamanda wa Polisi wa Kaskazini Unguja, Ahmad Khamis akisema manusura hao walikimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Miongoni mwa waliookolewa ni nahodha wa jahazi hilo Ahmada Haji Kombo ‘Gora’ na wafanyakazi wengine wa chombo hicho, Ali Haji, Khalid Haji, Mbwana Mshiraji na Khalfan.
Hali mbaya ya hewa ndiyo inayodaiwa kusababisha ajali hiyo ambayo imetokea siku chache baada ya nyingine ya Julai 18 ya boti ya mv Skagit iliyozama na kuua watu 136 wakiwamo raia wawili wa Uholanzi miongoni mwa wageni 15 waliokuwamo.
Timu ya wataalamu 10 iliundwa kufanya uchunguzi wa ajali ya mv Skagit, huku Rais Ali Mohamed Shein akiahidi kwenye sherehe za Idd el Fitri juzi Bwawani, kwamba Serikali yake iko kwenye mchakato wa kununua meli mpya ili kurahisisha usafiri na usafirishaji katika bahari ya Hindi.
Rais aliungana na viongozi wengine wa ZMA kuahidi mabadiliko makubwa katika safari za baharini.