Monday, August 13, 2012

Dk. Ulimboka arejea kwa kishindo

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Steven Ulimboka akisindikizwa na baadhi ya wananchi baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam jana akitokea Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu. (Na Mpigapicha Wetu).Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Steven Ulimboka akisindikizwa na baadhi ya wananchi baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam jana akitokea Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu.
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka, amerejea kwa kishindo nchini kutoka Afrika Kusini alikokuwa anatibiwa, na kusema yupo tayari kendeleza mapambano na kazi baada ya kupona kabisa.
Dk. Ulimboka alikwenda Afrika Kusini Juni 30 mwaka huu kwa ajili ya matibabu bora zaidi baada ya kutekwa, kupigwa na kutelekezwa kwenye msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na watu wasiojulikana.
Mwenyekiti huyo aliwasili jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Kambarage Nyerere (JKN) saa 8:15 alasiri kwa ndege ya Shirika la Afrika Kusini na kupokelewa na mamia ya madaktari, ndugu, rafiki, wanaharakati na jamaa zake.
Dk. Ulimboka aliondoka nchini akiwa kwenye kitanda cha wagonjwa kwa vile alikuwa kwenye hali mbaya kiafya, lakini jana alirejea akitembea kwa miguu na kuonekana mwenye afya njema.
“Nawashukuru Watanzania, madaktari, ndugu na jamaa zangu kwa kuniombea na kunisaidia kupata matibabu bora hadi leo hii narudi nyumbani nikitembea mwenyewe… nimepona kabisa, nipo tayari kwa mapambano na kufanya kazi yoyote, hakuna kilichoharibika mwilini mwangu,” alisema.
Vurugu uwanjani
Vurugu zilitokea kati ya ndugu na waandishi wa habari waliotaka kufahamu mambo kadhaa kutoka kwa Dk. Ulimboka mwenyewe, lakini baadhi ya ndugu zake waliwazuia wanahabari wasimwone.
Lengo la waandishi lilikuwa ni kumtaka Dk. Ulimboka aliyekuwa tayari kujibu maswali yao, kuwaeleza alikuwa akipata matibabu hospitali gani na chini ya daktari gani huko Afrika Kusini.
Licha ya ndugu kuwazuia wanahabari hususan wapiga picha, baadhi ya madaktari, wakiwemo viongozi wa jumuiya na Chama cha Madaktari (MAT) walijaribu kudhibiti hali hiyo na hatimaye waandishi japo kwa shida walipata kumwona na kumpiga picha.
Hata hivyo, muda wote baada ya kuwasili kwake, madaktari wenzake na wanaharakati walikuwa wakiimba nyimbo za kuhamasishana, ukiwemo wimbo wa taifa, huku wakimsindikiza kupanda gari walilolizunguka na kulisukuma hadi kwenye lango la kutokea uwanjani hapo.
Kwa mujibu wa ndugu wa karibu wa Dk. Ulimboka, kwa sasa atakuwa kwa wazazi wake Ubungo jijini Dar es Salaam kwa vile alikuwa mbali na familia yake kwa zaidi ya miezi miwili.
“Kwa sasa anakwenda nyumbani kwa baba…mke na mtoto wake watakuwa pale, unajua alikuwa mbali na familia, tena kwa matatizo,” alisema ndugu huyo aliyeomba jina lake lisichapishwe gazetini.
Akizungumzia kurejea kwa mwenyekiti wake, Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk. Edwin Chitage alisema kupona kwa Dk. Ulimboka kulitokana na huduma bora alizopata akiwa nje ya nchi.
“Ni Watanzania wachache wanaopata bahati kama ya Dk. Ulimboka, wengi wanakufa kwa sababu ya mazingira mabaya na huduma duni za matibabu… ndiyo maana madaktari tunataka kuboreshewa mazingira ya kazi zetu.
“…Kwa sababu madai yetu hayajatekelezwa, tutaendelea kupigania suala hilo ili kuwaokoa Watanzania maskini wasio na uwezo wa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu bora,” alisema.
Dk. Chitage aliongeza kuwa, hivi sasa Dk. Ulimboka atakuwa nyumbani kwa wazazi wake, kwa sababu alitengana nao kwa muda mrefu, na kwamba baada ya kupumzika kwa siku kadhaa, atazungumza na waandishi wa habari na kueleza yaliyo moyoni mwake.
Wanaharakati
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya na Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Malya walikuwa miongoni mwa waliofika kumpokea daktari huyo.
Wanaharakati hao walikuwa na mabango yaliyoandikwa; “Dk. Ulimboka karibu nyumbani, uliumizwa kikatili ukitetea afya bora kwa Watanzania”, “Dk. Ulimboka damu yako ilimwagika na kuamsha ari kwa wananchi kudai huduma bora za afya”, “Dk. Ulimboka wewe ni mpigania haki na afya bora kwa wananchi wote, Mungu na Watanzania wote tuko nawe”.
Akizungumza na waandishi wa habari, Malya alisema kupona kwa Dk. Ulimboka na kurejea nchini ni uthibitisho kwamba Mungu amesikia sauti za wanyonge.
“Dk. Ulimboka alisimamia haki za madaktari na za Watanzania wote, akitaka huduma bora zipatikane kwenye hospitali za umma kwa ajili ya wote,” alisema Malya.
Naye Nkya alifurahia kurejea kwa daktari huyo akimwita mpambanaji wa afya za Watanzania, na kusema lengo la kipigo alichopata lilikuwa kumtoa roho, lakini Mungu amempigania ili kuiumbua serikali dhalimu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Usiku wa kuamkia Juni 27, 2012 watu wasiofahamika walimteka, kumpiga, kumng’oa kucha na meno kisha kumtelekeza kwenye msitu wa pande Dk. Ulimboka.
Akiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) chini ya jopo la madaktari saba wakiongozwa na Profesa Joseph Kahamba, alishindwa kupatiwa baadhi ya vipimo ili kubaini iwapo damu yake ilikuwa na sumu ama la, kwa sababu baadhi ya dawa zilishindwa kufanya kazi.
Profesa Kahamba alikaririwa akisema hapa nchini hakuna kipimo kinachoweza kubaini sumu iliyopo kwenye damu ya mgonjwa huyo, hali inayowawia vigumu kumpatia matibabu sahihi, hivyo kumlazimu kwenda nje ya nchi.
Kabla ya kuondoka, madaktari hao walijichangisha fedha kwa lengo la kupata sh milioni 40 za matibabu ya mwenzao, jambo lililofanikiwa huku mmoja wa madaktari waliokuwa karibu na kamati ya kumsaidia Dk. Ulimboka, akisema zaidi ya sh milioni 60 zimetumika kuhakikisha mwenyekiti huyo wa jumuiya yao anapona.