Saturday, July 21, 2012

Zitto ahofia ukoloni kurejea

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, ameitahadharisha serikali kuepuka kuurejesha ukoloni ambao utalifanya taifa lisiwe na uhakika wa chakula na mbegu.
Alitoa tahadhari hiyo jana bungeni alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa mwaka 2012/2013 ambapo alipinga matumizi ya teknolojia ya uhandisi jeni (GMO).
Alisema matumizi ya teknolojia hiyo inawarejesha Watanzania katika ukoloni mkongwe na kuwa mikono ya mabeberu watakaokuwa na uwezo wa kuamua wakati gani wataipatia Tanzania mbegu mbalimbali.
Alisema anapinga nchi na wakulima kutegemea mbegu kutoka nje katika kampuni kubwa hususan ya Monsanto ambayo inapigiwa ‘debe’ bila woga na serikali.
“GMO inaturudisha katika ukoloni, itatufanya tuwe tegemezi, serikali haioni aibu wala woga kulizungumzia jambo hili…, mimi sikubaliani nalo na ninawaomba wabunge na wananchi tusiikubali,” alisema.
Alibainisha kuwa anapata wasiwasi jinsi kampuni ya kuzalisha mbegu ya Monsanto inavyoshiriki katika kila hatua katika kilimo kwanza ambacho hivi sasa kimekuwa kikiimbwa kila kona na serikali.
Awali akisoma hotuba yake ya bajeti, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alisema GMO katika kilimo inaweza kuongeza ubora na uzalishaji wa mazao ya kilimo, kupunguza gharama za uzalishaji, kuhifadhi mazingira na kwa kupunguza matumizi ya dawa na mbolea, kusafirisha mazingira na uzalishaji wa nishati mbadala.
Aliongeza kuwa kuna madhara yanayoweza kutokea kama hakutakuwa na utafiti wa kutosha katika teknolojia ya uhandisi jeni.