• Mgomo waanza, watikisa kila kona ya nchi
WAKATI walimu wakianza mgomo wa kutoingia madarasani jana, serikali imesema kuwa walimu watakaobainika kujihusisha na mgomo huo hawatalipwa mishahara.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema hayo jana wakati akitoa tamko la serikali kuhusu mgomo huo kwa waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, licha ya mwajiri kutowalipa mshahara walimu wote waliogoma watachukuliwa hatua kali huku wale wanaowatisha wenzao na kuwashirikisha wanafunzi kwenye mgomo, watawajibishwa.
Serikali pia imevitaka vyombo vya habari kuacha kuchochea mgomo huo kwa aina ya habari inazopeleka kwa umma, huku akisema kwamba si kazi ya vyombo hivyo kulibomoa taifa.
“Kwa mujibu wa sheria namba sita ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 ambayo mchakato wake ni mfupi, kifungu cha 83(4)g cha sheria hiyo, mwajiri hatalazimika kulipa mshahara kwa mtumishi aliyeshiriki katika mgomo kwa kipindi chote cha mgomo huo.
“Sheria ipo wazi, tutafanya hivyo kwa kipindi chote watakachokuwa kwenye mgomo… lakini pia kesi ipo mahakamani tayari na kesho mchana itatolewa hukumu,” alisema Dk. Kawambwa na kuongeza kwamba Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimefuata taratibu zote za mgomo huo.
Awali waziri huyo alisema serikali inaithamini elimu na walimu pia, haina sababu ya kushindwa kutatua kero zao ikiwemo ya kuwaongezea mishahara kwa asilimia 100; posho ya kufundishia kwa asilimia 55 ya mshahara walimu wa sayansi na asilimua 50 walimu wa sanaa.
“Walimu wanadai pia posho ya mazingira magumu ya kazi kwa asilimia 30 ya mshahara wao,” tunayo nia ya kufanya hayo lakini uwezo wa serikali ni mdogo ndiyo maana Juni 30 mwaka huu tuliweza kulipa sh bilioni 56 madai yao kwenye malimbikizo ya likizo na madai mengine ya walimu.
Dk. Kawambwa aliyepata kuwa waziri kwenye wizara nne tofauti katika utawala wa Awamu ya Nne, alisema juhudi za usuluhishi wa mgogoro huo zimekwama baada ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kushindwa kufanya hivyo, hali iliyoilazimu serikali kukimbilia Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
“Baada ya CMA kushindwa pale walimu walipokataa nyongeza ya asilimia 14 ya mishahara yao tofauti na watumishi wengine wa serikali, ikasema itatoa cheti cha kushindwa kuleta suluhu kwenye mgogoro ule (Certificate of Deadlock).
“Julai 26 serikali iliwasilisha ombi la kuzuia mgomo uliotangazwa na CWT nchi nzima, Julai 27 serikali na CWT tulitakiwa kupeleka maelezo yetu kwa maandishi ambapo serikali iliamriwa kupeleka maelezo yake leo (Julai 30) na wenzetu wapeleke maelezo yao kesho (Julai 31) kabla ya kuanza kwa mgomo huo,” alisema Dk. Kawambwa ambaye ni Mbunge wa Bagamoyo.
Bila kueleza iwapo mahakama hiyo ilitoa amri ya kuzuia mgomo ama la, waziri huyo aliwataka waandishi wa habari kusubiri uamuzi wa mahakama utakaotolewa leo mchana.
Hali ya mgomo nchini
Licha ya serikali kutangaza kuwa mgomo wa walimu ni batili, walimu wa mikoa mbalimbali nchini wameanza rasmi mgomo huo.
Jijini Dar es Salaam, mwitiko wa mgomo huo ulikuwa mkubwa wakati katika mikoa ya Mbeya na Arusha Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walilazimika kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi waliokuwa wakiandamana kupinga mgomo wa walimu wao.
Jijini Dar es Salaam, wanafunzi wa shule mbalimbali walikuwa nje wakicheza wakati walimu wao walijikusanya kwenye vikundi kujadili mgomo huo bila kuingia madarasani.
Miongoni mwa shule hizo ni Shule ya Msingi Nzasa na Charambe wilayani Temeke, ambapo katika Shule ya Nzasa walifika walimu wawili licha ya shule hiyo kuwa na walimu 63 na katika Shule ya Msingi Charambe mwalimu aliyefika ni mmoja kati ya walimu 48.
Shule nyingine ambazo walimu wake waliingia kwenye mgomo kuanzia jana ni Shule ya Msingi na Sekondari ya Makumbusho Wilaya ya Kinondoni, ambapo mkuu wa Shule ya Sekondari Makumbusho alikataa kuzungumzia hali hiyo na kutaka atafutwe ofisa elimu ili atolee maelezo mgomo huo.
Wakizungumza na gazeti hili jana, baadhi ya wanafunzi katika shule hizo walisema mgomo huo una waathiri kwani baadhi yao wapo katika maandalizi ya mitihani ya taifa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa baadhi ya shule kulikuwa na walimu wachache.
Hali ilikuwa tofauti kwenye shule za Msingi Mnazi Mmoja, Buruguni, Bunge na nyingine zilizopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, ambapo walimu walikuwa wakiendelea kufundisha.
“Hatuoni sababu ya sisi kugoma ikizingatiwa kuwa madai ya mgomo huu hatuyajui, pia hatujashirikishwa,” walisema baadhi ya walimu hao walipozungumza na gazeti hili.
Shule nyingine zilizoguswa na mgomo huo ni Shule ya Msingi Malamba Mawili Mbezi, ambapo mwalimu mkuu wa shule hiyo, Leah Sanga, alieleza kushangazwa na baadhi ya walimu wake kutofika kabisa eneo lao la kazi.
“Shule ina wanafunzi zaidi ya 3,000 lakini nimefika peke yangu, kutokana na hali hiyo imenilazimu nikae nao kwa maelewano hadi saa 5 asubuhi ndipo nilipowaruhusu kurudi nyumbani,” alisema Mwalimu Sanga.
Shule za msingi Mbagala Kuu, Bwawani na Kijichi walimu wake pia hawakuingia madarasani.
Kutoka Mbeya, Mwandishi Gordon Kalulunga, anaripoti kuwa mgomo wa walimu jana ulitikisa baadhi ya shule za mjini humo.
Kwa mujibu wa habari hizo, wanafunzi wa shule nyingi mjini hapa walionekana wakicheza muda wote wa masomo, huku walimu wao wakiwa nje wakibadilishana mawazo.
Katika baadhi ya mitaa ya katikati ya Jiji la Mbeya, FFU walilazimika kutumia nguvu kuwatawanya wanafunzi waliokuwa wakiandamana kupinga mgomo huo.
Kutoka mjini Arusha, inaripotiwa kuwa baadhi ya shule zimeingia katika mgomo huo kwa walimu wao kugoma kuingia darasani.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika mikoa ya Iringa, Mwanza, Shinyanga na mikoa mingine, walimu wengi walifika mashuleni na kusaini kitabu cha mahudhurio, lakini hakuna aliyeingia darasani kufundisha.