Tuesday, July 17, 2012

Wabunge watishiana maisha

*Wabunge wa Chadema wadaiwa kumtisha Mwigulu
*Wamtumia meseji nzito kupitia simu za mkononi
*Yeye ahamaki, azipeleka meseji hizo polisi
*Spika awaonya wabunge, awataka wabadilike

MBUNGE wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), jana alitoa shutuma nzito dhidi ya wabunge Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akidai wanatishia maisha yake.
Mwigulu alisema kuwa baadhi ya wabunge wa chama hicho wanatishia uhai wake, kutokana na meseji alizotumiwa na wabunge hao.

Kutokana na hali hiyo, mbunge huyo alidai kuwa ameripoti suala hilo katika Jeshi la Polisi na kwamba tayari wabunge hao wanajulikana kwa majina.

Mwigulu aliyasema hayo bungeni jana, alipokuwa akiomba Mwongozo wa Spika kutaka Bunge lisitishe shughuli zake kwa ajili ya kujadili tukio la mauaji ya Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Yohana Mpinga (30), aliyeuawa juzi jimboni kwake.

Akiomba mwongozo huo, Mwigulu alisema: “Mheshimwa Spika, nimesimama kwa kutumia Kanuni ya 47 inayosema kwamba, baada ya muda wa maswali kwisha, mbunge yeyote anaweza kusimama na kuomba mwongozo wa kuahirishwa kwa shughuli zilizopo katika kitabu cha orodha cha shughuli za Bunge ili kujadili jambo analohisi ni la dharura, hata kama majadiliano yatakuwa yanaendelea.

“Kwa hiyo, Mheshimwa Spika, kutokana na tukio la kinyama lililotokea kwa kijana ambaye naweza kusema ni msaidizi wangu, yaani ni Katibu wa Umoja wa Vijana, UVCCM katika Kata ya Ndago, naomba Bunge lako liahirishe shughuli zake ili tujadili jambo hilo.

“Kijana huyu aliuawa kwa kufukuzwa kama kuku na kuuawa katika nyumba, naomba kutoa hoja Bunge lako liahirishe shughuli zilizopo kwenye orodha ya shughuli za leo.

“Nasema hivyo kwa sababu yaliyofanyika yanaonyesha yalikuwa yamepangwa, kwani kabla ya tukio hilo kutokea, nilipokea meseji za simu ambazo nimetumiwa na baadhi ya wabunge wa Chadema wakinitisha.

“Kwa hiyo, inaashiria kuwa, lililofanyika lilikuwa na uhusiano na hili la kunitisha, kwa ruhusa yako, naomba nizisome meseji hizo ambazo wabunge waliozituma nimezipeleka polisi na tayari wanajulikana,” alisema Mwigulu.

Hata hivyo, alipokuwa akijiandaa kusoma meseji hizo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimzuia mbunge huyo na kusema hakuna haja ya kufanya hivyo, kwa kuwa suala hilo liko polisi.

“Jambo hilo nimelisikia na kulisoma kwenye vyombo vya habari na bahati nzuri yule msemaji wa kamati amelaani tukio hilo na tumeambiwa polisi wanafanya uchunguzi wa kina.

“Lakini waheshimiwa wabunge, naomba msome vizuri kanuni katika kifungu cha masharti ambacho kinasema jambo lolote litahesabiwa kuwa la dharura na la maslahi kwa umma kama utatuzi wake unafanyika nje.

“Kwa sasa, jambo hilo alilosema Mheshimiwa Mbunge, tayari lipo polisi na siyo busara kama tukianza kulijadili hapa, kwa kuwa hata kama tukilijadili sijui tutafika wapi, tuwaachie polisi wafanye kazi yao.

“Pia nawataka polisi na Waziri wa Mambo ya Ndani, kulishughulikia jambo hili kwa kufanya utafiti wa kutosha ili kuwabaini wahusika na watakaoonekana wamefanya unyama huo, wachukuliwe hatua bila upendeleo,” alisema Spika Makinda.

Katika mazungumzo yake, Spika aliwataka wabunge kuacha tabia ambayo wameianzisha ya kuzungumzia masuala yanayotokea ndani ya Bunge wanapokuwa nje.

“Mnachukua maneno tena mnaanza kutishia wenzenu kuwa mnataka kuwaua, acheni tabia hiyo, yaani siku hizi mmeanzisha tabia ambayo haina heshima kwenu.

“Kila mtu anatakiwa kujadili jambo kwa heshima na kwa mujibu wa kanuni, yale unayojadili kwa heshima watu watakuunga mkono, lakini kama ukijadili na kuanza kutumia lugha zisizofaa kama kutishia kuua hatutakubali na mimi nayajua majina ya wabunge hao,” alisema Makinda.

Mwishoni mwa wiki, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), alihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Ndago kilichoko Jimbo la Iramba Magharibi. Katika mkutano huo, walikuwapo pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk. Kitila Mkumbo na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Mwita Waitara.

Wakati mkutano huo ukiendelea, kuna taarifa kuwa, viongozi wa Chadema walitoa maneno ya kashfa dhidi ya Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba na kwamba kauli hizo ziliwafanya wafuasi wa CCM waliokuwa eneo la mkutano, washindwe kuvumilia na kuanza kuwarushia mawe wafuasi wa Chadema.

Kutokana na hali hiyo, inadaiwa wafuasi wa Chadema nao walijibu mapigo na hatimaye kusababisha kifo cha Mpinga, aliyeuawa kwa kupigwa mawe akiwa katika nyumba moja ya mwalimu alikokuwa amekimbilia kunusuru maisha yake.