Monday, July 16, 2012

Wabunge wa aina hii hawafai

MKUTANO wa Bunge la Bajeti unaoendelea sasa mjini Dodoma, umetajwa kuwa wa aina yake kutokana na vituko vinavyofanywa na baadhi ya wabunge.
Tangu kuanza kwake Juni 11, mwaka huu, vikao vya Bunge kadhaa vimegeuka kuwa uwanja wa mipasho, jukwaa la siasa, na kumbi za matusi na kashifa.
Kinyume kabisa cha matarajio ya Watanzania, Bunge ambalo lilitakiwa kuwa kisima cha hekima, heshima na kielelezo sahihi cha nidhamu na haki, limejishusha hadhi kiasi cha kusemwa hata na watoto wa shule za msingi.
Hatupendi kabisa kurudia kile kilichokwisha kusemwa na gazeti hili, iwe ni kihabari, makala au maeneo mengine, leo tuweke wazi jinsi wabunge wengi wanavyotumia vibaya Bunge hili kwa kujadili kisichoeleweka.
Kwa miaka mingi, na hasa baada ya kuingia kwa wabunge wengi vijana na wasiojua kuficha uozo, wasema kweli, wazalendo wa dhati na wasio na chembe ya woga, Watanzania wameshuhudia aina ya wabunge wanaoshindwa kutofautisha wajibu wao kama wabunge na pale wanapokuwa wanahutubia katika majukwaa ya siasa.
Kazi ya mbunge na wajibu wake ni kuisimamia serikali ili itimize wajibu wake kikamilifu ya kiutendaji. Mbunge bila kujali itikadi ya vyama, anawajibika kutambua kuwa pale bungeni hawakilishi chama chake tu, bali wananchi wote waliompa imani na wakamchagua.
Watanzania wanategemea mbunge anayesimama, ama anazungumzia mambo ya msingi ya maendeleo na kuikosoa waziwazi na hata kuiwajibisha serikali pale inapofanya uzembe.
Badala yake, wabunge wengi hasa wa CCM, wamegeuka kuwa wasemaji wakuu wa serikali kuliko hata mawaziri wenyewe wa wizara. Wamekuwa daima wakifanya kazi za chama na kusahau kwamba wao ni walinzi na wasimamizi wakubwa wa kazi za serikali.
Kana kwamba hilo halitoshi, na kwa sababu ya kuwa viziwi na ushabiki wa kushangaza na usiotarajiwa, baadhi ya wabunge wa CCM wamekuwa ‘ndumila kuwili’ na wasiojua wanachotaka, baada ya kuzishambulia baadhi ya hotuba za bajeti, lakini mwisho wa siku wakiishia kuunga mkono hotuba hiyo mia kwa mia na wengine mia mbili kwa mia!
Mbunge ambaye katika jimbo lake, wanawake wameota vibiyongo kwa sababu ya kuchota maji ya tope maili nyingi, wasichana wamefeli shule kwa sababu ya kutumia muda wao mwingi kutafuta maji, na wanawake wajawazito wanaojifungua porini kwa kukosa zahanati, anawezaje kuwa na ujasiri wa kuwaponda wabunge wa upinzani wanaoishambulia serikali kwa kuzembea kuwafikishia Watanzania hao huduma za afya na maji?
Mbunge wa aina hiyo anayeanza kujipendekeza kusifia uongozi wa spika, waziri mkuu na rais na kushusha ‘tusi’ kwa wapinzani, anapata akili za aina gani za kuanza kuunga mkono hoja mia kwa mia na kupigiwa makofi, halafu analalama hadi povu linamtoka mdomoni? Je, dharau kwa wapinzani ilikuwa ya nini? Kule kujitapa kote kulitoka wapi?
Hivi wabunge wa aina hii, nani bado anawadanganya kuwa watu wana haja ya kusikia CCM dume, wakati maisha yao ni dhiki tupu?
Tunataka wabunge wa aina hii wabadilike. Wajue kuwa hawalipwi na CCM, bali ni fedha za Watanzania wote. Wala wasijidanganye kwamba eti, serikali ya CCM ndiyo inajenga hiki ama kile, bali wajue kuwa wao na serikali yao wamepewa dhamana tu ya kuwa watumishi wa watu na kwamba, kama ni barabara ama chochote kile kinajengwa na Watanzania wenyewe kwa fedha yao!