Monday, July 16, 2012

Wabunge vijana kupata mafunzo JKT

WABUNGE vijana wa bunge la Tanzania wataanza kushiriki mafunzo maalum ya Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) ya miezi mitatu sambamba na mafunzo ya vijana kwa mujibu wa Sheria mwaka ujao.
Akiwasilisha bungeni hotuba ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Waziri wa wizara hiyo Shamsi Vuai Nahodha alisema wabunge hao vijana wataungana na kundi la kwanza la vijana 5000 katika mafunzo hayo yaliyopangwa kuanza i Machi 2013.
Waziri Nahodha alisema bungeni kuwa, wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara hiyo ya mwaka 2011/2012 wabunge hao waliomba kupata mafunzo hayo.
“ Ni imani yetu kuwa pamoja na waheshimwa wabunge kunufaika na mafunzo hayo watahamasisha zoezi la urejeshwaji wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria na kutoa taswira nzuri ya mafunzo hayo kwa jamii. Naomba waheshimiwa wabunge mjiorodheshe kwa maandalizi ya mafunzo haya,” amesema Nahodha.
Amesema, ingawa JKT lipo tayari kuchukua vijana 20,000 kwa wakati mmoja haitaweza kufanya hivyo kutokana na gharama za kuendeshea mafunzo hayo kuwa kubwa.
“Vijana hao ni miongoni mwa vijana 41,348 ambao watahitimu mafunzo ya Kidato cha Sita katika mwaka 2013. Kwa hivyo, Wizara imeweka vigezo maalumu vya kuwapata vijana hao kwa kuzingatia makundi. Makundi ya vijana hao yatatangazwa mwezi Januari 2013,” amesema.
Nahodha amesema, mafunzo hayo ya vijana kwa mujibu wa sheria yatafanyika kwa miezi sita katika kambi za Bulombora na Kanembwa (Kigoma), Mlale (Ruvuma), Mafinga (Iringa), Msange (Tabora) na Oljoro (Arusha).
Akizungumzia umuhimu wa matrekta katika kuendeleza Kilimo Kwanza, alisema Serikali imepunguza bei ya matrekta katika Shirika la SUMA-JKT ambapo matrekta yenye “horse power” 50 yaliyokuwa yakiuzwa shilingi milioni 25.6 sasa yanauzwa shilingi milioni 16.5 na matrekta yenye “horse power” 70 yaliyokuwa yanauzwa shilingi milioni 45.8 sasa yanauzwa shilingi milioni 38.8.
“Hivi sasa Shirika linawapunguzia wateja malipo ya awali (down payment) kutoka asilimia 50 ya bei ya trekta moja hadi asilimia 30. Vile vile Shirika linafikiria kupunguza zaidi malipo ya awali hadi asilimia 15 kwa wateja watakaonunua matrekta kuanzia 50 na kuendelea. Halikadhilika, Halmashauri za Wilaya ambazo zitakuwa tayari kuwadhamini wakulima wadogo wadogo imependekezwa zilipe malipo ya awali ya asilimia 10,” alisema.
Aidha alisema hadi kufikia tarehe 09 Julai, 2012 SUMAJKT ilikuwa imeuza matrekta 786 na kwamba katika kusogeza matrekta karibu na wateja wake, SUMAJKT imefungua vituo vya kuuzia matrekta hayo katika mikoa ya Dodoma, Mbeya, Mwanza na Arusha.
“Nimemwagiza wakala wa uuzaji wa matrekta kufanya mipango ya kuyahamishia matrekta yaliopo Mwenge Dar es Salaam na kuyapeleka Morogoro. Shirika la SUMAJKT linatarajia kufungua vituo zaidi vya mauzo ya matrekta kupitia kwa Wakuu wa Mikoa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kama vile ushauri na vipuri, alisisitiza.
Kuhusu kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa suala la migogoro ya ardhi ina ya jeshi na wanachi alisema Wizara imeanza kuchukua hatua mbalimbali.
“Katika baadhi ya maeneo tutalazimika kuwaondoa wavamizi mara moja ili kupisha shughuli za jeshi. Aidha, kwa maeneo ambayo uingiaji wa watu umezidi kiwango kiasi cha kufanya eneo husika kutokufaa tena kwa shughuli za Jeshi, tutashauriana na mamlaka zinazohusika kuangalia uwezekano wa kupewa maeneo mbadala,” Waziri Nahodha alisema.
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeliomba kuidhinisha jumla ya shilingi 1,086,550,058,000.00 ambazo kati yake shilingi 678,363,492,000.00 zitatumika kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na shilingi 408,186,566,000.00 ni bajeti ya matumizi ya maendeleo.