Friday, July 20, 2012

Vilio, simanzi Zanzibar.Walikufa wafikia 154, maiti zilizoopolewa zafikia 63

WAKATI vilio na simanzi vikiendelea kutawala kwa wananchi wa Zanzibar, kufuatia ajali mbaya ya kuzama kwa meli ya Mv Skagit juzi mchana katika eneo la Chumbe, serikali imetoa maelezo kuwa meli hiyo ilikuwa na abiria 290.
Hadi jana jioni maiti 63 zilikuwa zimeopolewa huku watu wengine 146 wakiokolewa hai na 81 wakiwa bado hawajapatikana licha ya juhudi za uokoaji kuendelea kwa msaada wa ndege ya Umoja wa Ulaya.
Hata hivyo, Msemaji wa Polisi visiwani Zanzibar, Mohamed Mhina, alisema juhudi za uokoaji zinaendelea lakini ni jambo lisilowezekana kabisa watu kupatikana wakiwa hai kutokana na kuzama kabisa kwa meli hiyo.
Kufuatia ajali hiyo, Rais Jakaya Kikwete, alifika visiwani humo jana jioni na kwenda moja kwa moja hadi viwanja vya Maisara ambako wananchi wamefurika wakitambua maiti za ndugu zao.
Rais Kikwete pia alimtumia salamu za rambirambi Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Mohamed Shein, na kutangaza siku tatu za maombolezo ambapo bendera itapepea nusu mlingoti.
Katika ufafanuzi huo wa serikali, ilielezwa kuwa meli hiyo ilitengenezwa nchini Marekani mwaka 1989 na kusajiliwa Zanzibar Oktoba 25 mwaka jana, na kupewa nambari ya usajili 100144 yenye uzito wa GRT96 chini ya umiliki wa Kampuni ya Seagul Sea Transport Limited ya Zanzibar.
“Meli hiyo kwa kawaida huwa inafanya safari zake Zanzibar–Pemba na Zanzibar-Dar es Salaam. Julai 18, 2012 meli hiyo iliondoka Dar es Salaam saa 5.30 asubuhi ikiwa na watu 290, kwa mujibu wa manifesti ya abiria iliyowasilishwa na wenye meli kwa mamlaka husika za Bandari (TPA) na ile ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra),” alisema.
Kwa mchanganuo huo, abiria watu wazima walikuwa 250, watoto 31 na mabaharia 9.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa meli hiyo wakati ikiwa inasafiri baharini kwa saa kama mbili na zaidi ikikaribia maili saba kufikia kisiwa cha Chumbe, ilikumbana na dhoruba kali iliyopelekea kuyumba sana na hivyo abiria kuanza kukimbilia sehemu ya juu ya meli, kitendo ambacho kilichangia kupoteza utulivu na hivyo kuanza kuingiza maji pembeni.
Kitendo hicho kilifanya meli hiyo kuanza kuzama kati ya saa 7:30 hadi 8:00 mchana na ndipo serikali kupitia vyombo vyake vya bandari na ulinzi na usalama, vilianza kuchukua hatua za uokoaji.
“Mnamo majira ya saa 9:15 chombo cha mwanzo Kilimanjaro 3, kilifika katika eneo la tukio kikifuatiwa na tagi ya Bandari na baadaye helikopta ya jeshi na vyombo vingine,” ilisisitiza taarifa hiyo.
Hadi juzi jioni giza linaingia na kupelekea zoezi hilo kushindwa kuendelea, jumla ya watu 146 walikuwa wameokolewa wakiwa hai, maiti 31 kati ya hao wakiwa watoto 9 na mmoja raia wa kigeni ziliopolewa.
“Leo zoezi hili la uokoaji linaendelea ambapo vikosi vya ulinzi na usalama, makampuni binafsi ya shughuli za uzamiaji, pamoja na taasisi za bandari zitashiriki kikamilifu katika kufanikisha zoezi hilo,” alisema.
Wananchi waishioa kwenye maeneo na vijiji vya mwambao wameombwa pale watakapoona miili au watu wanaosadikiwa kuwa wametokana na kuzama kwa meli hiyo, watoe taarifa serikalini kupitia simu namba 0777- 429269.
Serikali imewataka wananchi waliopotelewa na jamaa zao kufuatia ajali hiyo wapeleke orodha ya majina hayo kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa upande wa Tanzania Bara na kwa Masheha kwa upande wa Visiwa vya Unguja na Pemba.
Serikali kununua meli
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud, amesema serikali inamaliza hatua za matayarisho ili kuona Zanzibar inapata meli mpya za abiria zitakazofanya safari zake katika visiwa hivyo.
Alisema hatua hiyo ni kwa sababu hivi sasa kumekuwa kukitokea matukio mengi ya ajali kwa kukosekana kwa usafiri wa uhakika katika visiwa hivyo hali inayotia wasiwasi miongoni mwa wasafiri.
Alisema taarifa ya meli hiyo itatolewa si muda mrefu kuhusu wapi inapotengenezwa na ubora wake na lini itaanza kazi ya usafirishaji ili kuondoa usumbufu uliokuwepo.
Akizungumza na waandishi katika uwanja wa Maisara jana, alisema pamoja na hilo serikali inajipanga kujitayarisha na vifaa vya uokoaji kwa majanga kama hayo.
“Ajali ya meli ya Mv Skagit ni ya Mungu; huwezi kuzuia kudra ya Mungu, ule haukuwa uzembe bali ni ajali iliyosababishwa na kuchafuka kwa bahari,” alisema Masoud.
Naye mmoja wa waokoaji binafsi waliofika katika tukio hilo, alisema meli hiyo imebinuka ikiwa mgongo juu huku vyombo kadhaa vya uokoaji vikiwa katika eneo la tukio.
Mmoja wa manusura, Hassan Khatib, alisema tangu walipoondoka Dar es Salaam saa sita hali ya bahari haikuwa nzuri, wimbi lilikuwa kubwa na baada ya kufika Chumbe meli ilizidiwa na wimbi na kukosa mwelekeo.
“Baada ya hapo ililala upande na muda mfupi ilibinuka nikaanguka majini nikiwa sina kitu cha kushika kisha nilianza kuogelea na baadaye nilishika ubao na kuogelea nao,” alisema.
Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema kuwa serikali zote mbili zinafanya jitihada za kuhakikisha zinazungumza na nchi husika ili wageni waliokuwemo katika ajali ya meli hiyo wanasafirishwa kurudi makwao.
Alisema mbali ya wageni hao 15 ambao wameokoka kufanyiwa juhudi za kurudi makwao, wanaendelea kufuatilia taarifa za raia mmoja wa kigeni ambaye amefariki ili kuweza kutambuliwa anakotoka.
Wabunge waachia posho
Bunge limeamua kukata posho ya siku moja (70,000) kwa kila mmoja ili zitumike kwa ajili ya rambirambi kwa watu waliofikwa na janga la kuzama kwa meli ya Mv Skagit visiwani Zanzibar.
Spika wa Bunge Anne Makinda, alitangaza uamuzi huo jana bungeni alipokuwa akiahirisha kikao cha Bunge kwa siku ya jana ili kutoa nafasi kwa wabunge kushiriki kwenye maombolezo.
Makinda alisema Kamati ya Uongozi, ilikutana jana asubuhi na kukubaliana posho za siku moja kwa wabunge zikatwe na zipelekwe kwa waliokumbwa na ajali hiyo.
Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa sasa lina idadi ya wabunge 352, hivyo kiasi cha sh 24,640,000 kinatarajiwa kukusanywa kama rambirambi za wawakilishi hao wa wananchi.
Akifafanua sababu za kuahirishwa kwa Bunge, Spika alisema kuwa walikubaliana kufanya hivyo kwa siku moja kwa ajili ya maombolezo.
“Jambo hili ni la kitaifa hivyo tumepeleka wabunge 14 kwa ajili ya kuwakilisha katika msiba huo, tayari maofisa wengine wamekwenda Zanzibar kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo uokoaji,” alisema.
Alibainisha kuwa huo ni msiba mkubwa wa taifa na mambo yako tete, hivyo wabunge hawawezi kuendelea na shughuli za Bunge katika kipindi hiki.
Spika Makinda alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema hakutakuwa na mazishi ya halaiki kwa sababu maiti 31 waliopatikana walishatambuliwa na ndugu zao.
“Maiti zote zilizowekwa katika Uwanja wa Maisela tayari zimeshatambuliwa na ndugu zao, hivyo kwa sasa wanaendelea na shughuli za mazishi leo,” alisema.
Makinda aliongeza kuwa watu waliopatikana wakiwa hai na maiti idadi yao ni ndogo kuliko wale waliokosekana, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo mazishi ya halaiki hasa baada ya kukamilika kwa shughuli za uokoaji.
Wabunge wanena
Akizungumza na Tanzania Daima, mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamis (CCM), alisema kuwa hivi sasa serikali inapaswa iweke nguvu katika kuboresha vifaa vya uokoaji.
Sadifa alisema ni vizuri eneo la Chumbe kukawekwa kituo cha uokoaji chenye vifaa vya kisasi ili ajali itakapotokea kitoe msaada wa haraka unaohitajika.
“Tuna kila sababu ya kujiimarisha kwa vifaa vya kisasa pamoja na watu wenye uwezo wa kuogelea, haya ni mambo ambayo serikali inapawa kuyapa kipaumbele,” alisema.
Naye mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alisema serikali imeshindwa kuboresha sekta ya usafiri wa majini pamoja na kikosi cha uokoaji ndiyo maana kila zinapotokea ajali za meli maafa yanakuwa makubwa zaidi.
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema chanzo cha ajali za majini zinazoendelea kutokea kuwa zinasababishwa na serikali kutokuwa makini.
Alisema kuwa pamoja na kwamba katika Ofisi ya Waziri Mkuu kuna kitengo cha maafa, kitengo hicho hakijaimarishwa badala yake kwa muda mrefu kimekuwa kikitoa vyakula na magodoro kwa waathirika badala ya kupambana na majanga makubwa.
“Matatizo haya yanatokea kwa sababu ya uzembe wetu, viongozi wetu hawako makini kwa sababu hata hawaoni umuhimu wa kuimarisha kitengo cha maafa.
“Kama kweli tungekuwa makini, hiyo meli isingesafiri kwani zingetolewa taarifa mapema kwamba bahari imechafuka ili meli zisisafiri lakini kwa kuwa viongozi hawako makini meli zinasafiri bila taarifa,” alisema.
CCM yatoa tamko
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka serikali kuchukua hatua za haraka dhidi ya wale watakaobainika kusababisha kwa uzembe kutokea ajali ya meli ya Mv Skagit iliyotokea visiwani Zanzibar.
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alitoa tamko hilo jana mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu janga hilo na kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka ikibainika kuwepo uzembe.
Nape alisema kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuipitia upya taarifa hiyo kwani inawezekana kuna baadhi ya mambo ambayo hayakufuatiliwa.
Alisema inatakiwa watu waliochangia kutokea kwa ajali hiyo wawajibike wenyewe kwani haiwezekani watumie fedha za wananchi lakini hakuna linalofanyika.
Nape aliongeza kuwa lazima vyombo vinavyohusika viwe makini kwani mara nyingi tukio la kuzama kwa meli au ajali linapotokea mambo mbalimbali hujitokeza kama vile kuwepo kwa uzito mkubwa melini au uchakavu.
Alishangazwa na namna meli hiyo ilivyoondoka bandarini ikiwa na abiria na mizigo zaidi ya uwezo wake wakati kuna watu wanaohusika na kazi hiyo.
Pia alisema inavyoonekana hivi karibuni usafiri wa ndege umekuwa ni wa uhakika zaidi lakini hilo linatokana na ukweli kuwa watendaji wake wamekuwa makini kila wakati.