Saturday, July 7, 2012

Vijana wahamasishwa kujiajiri

VIJANA wametakiwa kutobweteka kusubiri ajira za serikali na badala yake watumie juhudi na maarifa ili waweza kujiajiri kupitia kilimo na ujasiriamali.
Pia, wametakiwa kujiunga katika vikundi ili kupata fursa za kupata mikopo katika taasisi za fedha ili kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Youth Development Agency (TAYODA), Jackson Kangoye, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, jana, kuhusu masuala mbalimbali ya taasisi hiyo.
Alisema vijana nchini wamekuwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa ajira licha ya kuwa na elimu na maarifa ya kutosha na kwamba, njia pekee ya kujikwamua ni kuanzisha miradi ili kuweza kujiajiri na kujipatia kipato.
“Ulimwenguni kote kwa sasa kuna tatizo la ajira na hali ya uchumi ni mbaya, lakini hili lisiwavunje nguvu vijana wenzetu na badala yake tujipange ili kuweza kujiajiri kwa kuanzisha miradi ya ujasiriamali. Tutumie vikundi ili kupata fursa za mikopo kwenye taasisi za fedha nchini,” alisema Kangoye.
Kuhusu mikakati ya TAYODA kuanzisha benki ya vijana, Kangoye alisema mchakato unaendelea na kwa sasa wapo katika hatua nzuri kwani, wamekuwa wakipata ushirikiano kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali.
Alisema lengo la kuanzishwa kwa benki hiyo ni kuwawezesha vijana kuondokana na kero mbalimbali ikiwemo tatizo la ajira kwani, wataitumia kukopa fedha za kuanzisha miradi.
Kangoye alisema tathmini ya kina imeshafanyika na wataalamu wameridhika nayo, hivyo kwa sasa wapo katika hatua ya kufanya mchanganuo yakinifu ili kukidhi haya ya kijana wa Kitanzania.
“Taasisi imekuwa ikiwahamasisha vijana hasa walioko vyuoni kujikita kwenye ajira binafsi ikiwemo ya kilimo kupitia sera ya kilimo kwanza. Kwa sasa tunaendelea na utaratibu wa kuwawezesha vijana na tumeanza kutoa matrekta madogo kwa shughuli za kilimo,” alisema.
Kwa sasa TAYODA ina zaidi ya wanachama 8,500 wakiwemo wanafunzi wa elimu ya juu pamoja na matawi yake manane kutoka vyuo mbalimbali nchini.