MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imesema
ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa kupitia maoni ya
wadau wa usafiri kuhusu mapendekezo ya kuongezeka kwa nauli mpya za
daladala.
Hayo yalibainishwa jana na Ofisa Mawasiliano wa
Sumatra, David Mziray alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi
kwa njia ya simu kuhusu hatua ambazo Sumatra imefikia baada ya wamiliki
wa daladala (Dacoboa), kupendekeza kuanza kutumika kwa nauli mpya za
daladala kutoka Sh350 hadi 870.
Alisema kazi ya kupitia maoni na
mapendekezo ya wadau wa usafiri kuhusu kuanza kutumika kwa nauli mpya za
daladala unaendelea na kwamba upo katika hatua za mwisho kukamilika.
“Kwa
sasa Sumatra haiwezi kusema chochote kuhusu lini nauli mpya za daladala
zitaanza kutumika kwani mchakato wa kupitia maoni na mapendekezo ya
wadau unaendelea lakini ninachoweza kusema umefikia katika hatua nzuri,”
alisema Mziray.
Alifafanua kuwa wakati mchakato huo utakapo
kamilika bodi ya Sumatra itakutana na kuamua nini kifanyike kwa kupitia
mambo yote yaliopendekezwa kwani wao ndio watakuwa waamuzi wa mwisho
katika suala hili kama nauli mpya za daladala zitaanza kutumika au nauli
za awali zitaendelea kutumika.
Mei 24 mwaka huu wadau wa usafili
walikutana jijini Dar es Salaam na kujadili mapendekezo yaliowasilishwa
na Dacoboa ya kutaka kuongezeka kwa nauli za daladala kutoka Sh 350
hadi 870.