Friday, July 13, 2012

Nchi inaelekea vitani

Uporaji wa ardhi wawatisha wabunge
WABUNGE wamesema serikali inaiandaa nchi kuingia vitani na umwagaji mkubwa wa damu kwa kuendekeza migogoro na uporaji wa ardhi unaofanyika sehemu mbalimbali hapa nchini.
Onyo hilo limetolewa bungeni jana na wabunge mbalimbali walipokuwa wakichangia bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2012/2013 ambapo walisema serikali inawanyang’anya ardhi wananchi na kuwapa wawekezaji.
Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, alisema serikali imejigeuza wakala, dalali na kuwadi wa wawekezaji kwa kutumia nguvu kuwanyang’anya ardhi wananchi.
Lissu alisema kitendo hicho ni hatari kwa taifa kwa kuwa kinaandaa mazingira ya vita na kutengeneza harakati za ukombozi na mapinduzi ya umwagaji damu siku zijazo.
Alibainisha kuwa kesi za migogoro ya ardhi hapa ni nyingi ambapo mpaka sasa zipo 6,000 katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi.
“Kuna migogoro mingi kwenye ardhi ambapo mingine haipelekwi mahakamani kwa sababu chombo hicho kimekuwa mithili ya gulio la kununulia haki,” alisema Lissu.
Lissu alisema wananchi hivi sasa wamekosa imani na mahakama inayoshughulikia masuala ya ardhi na matokeo yake wameamua kujichukulia sheria mkononi.
“Migogoro ambayo imekuwa ikisababisha mapinduzi na vita vya kutafuta ukombozi katika baadhi ya nchi barani Afrika mingi ni ile inayosababishwa na ardhi,” alisema.
Aliongeza kuwa serikali inafuata ubepari uchwara kwa kujigeuza kuwadi, dalali wa kuuza ardhi ya wananchi na kuwapa wawekezaji, ambao ni kampuni za Magharibi.
“Tunatengeneza mapinduzi ya umwagaji damu siku zijazo, mimi sipendi niwe sehemu ya historia hiyo, nitawaambia wajukuu wangu kuwa tulikemea lakini tulizidiwa nguvu,” alisema Lissu.
Lissu alitolea mfano kuwa serikali ilivyotumia nguvu kupora ardhi ya wananchi katika Jimbo la Singida Mashariki eneo la Shanta Mining, huku Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa serikali wakipinga kimya kwa madai kwamba, wamekuwa makuwadi wa soko huria na wawekezaji.
“Na namna zote zilifanyika ni wananchi kuchukua silaha. Waziri akifanya majumuisho aeleze vinginevyo wananchi wa Singida Mashariki wanasema ama zao ama za Shanta Mining,” alisema Lissu.
Alisema kuna baadhi ya vitu vinatia aibu na kutolea mfano wa namna kampuni moja ya Kitanzania ya uwindaji wanyama kuingia mkataba na kampuni za uchimbaji wa madini ya uranium, kinyume cha sheria ya matumizi ya ardhi.
“Kama si ukuwadi ni nini? Tunatengeneza mazingira ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na hawatakuwa wamekosea,” alisema Lissu.
Naye mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alisema serikali inawalinda maofisa ardhi wanaopora ardhi za wananchi na kuvigawa kwa mtu zaidi ya mmoja.
“Waziri wa Ardhi nilishakwambia kuwa Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Kasulu, anauza maeneo ya wazi lakini hutaki kuchukua hatua, hivi kuna nini hapa, sasa nakwambia siungi mkono bajeti yako.
“Siungi mkono na kama serikali itashindwa kuchukua hatua dhidi ya huyu Ofisa Ardhi, basi mimi nitawaambia wananchi wangu wachukue sheria mkononi maana nyie mmeshindwa kuchukua hatua.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), alisema atawahamasisha wananchi wake wachukue sheria mikononi ili wapate haki zao kwa sababu serikali imeshindwa kuitatua migogoro ya ardhi.
“Polisi, serikali wameshindwa kuwasaidia wananchi wangu ambao kila wanapoipeleka migogoro ya ardhi kituo cha Polisi Kawe, askari hawachukui hatua kwa sababu wanapewa rushwa na wenye fedha.
“Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba uchukue hatua kumaliza migogoro hii, najua kuna mtu mmoja anamiliki Kituo cha Mafuta kiitwacho Tegeta Petrol Station, huyu amepora ardhi ya watu kwa kisingizio kuwa anafahamiana na watu wa Ikulu.
“Mheshimiwa waziri hebu chukua hatua, kama umeweza kubomoa majengo fulani fulani pale Dar es Salaam, basi naomba ukavunje na yale majengo ambayo mimi na wewe tulifukuzwa na mlinzi siku tulipoyatembelea,” alisema Mdee.
Mbunge wa Kisarawe, Selaman Jafo (CCM), pamoja na kutoridhishwa na migogoro ya ardhi jimboni kwake na Tanzania kwa ujumla, aliwatahadharisha watu waliopora ardhi kwenye mashamba pori jimboni kwake, kwamba ardhi hiyo itarudishwa serikalini kwa kuwa wameichukua bila kufuata utaratibu.
Katika hatua nyingine, aliilalamikia serikali kwa kushindwa kuwachukulia hatua watendaji wasiokuwa waadilifu kwa kuwa ndiyo wanaosababisha migogoro hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.