Friday, July 13, 2012

Mzimu wa Dowans waitesa serikali

Hoja ya ama kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans ilipwe au isilipwe fidia, jana iliibuka tena na kutishia kuchafua hali ya hewa bungeni.

Hoja hiyo iliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, wakati wa kipindi cha maswali na majibu.

Kafulila aliliomba Bunge limkubalie kutoa ushahidi wa kutosha juu ya namna serikali ilivyohusika katika kushindwa kwa kesi ya Dowans kwa makusudi ya kuihujumu nchi.

Aliomba kufanya hivyo alipokuwa akiuliza swali la nyongeza na kusema kwamba imekuwa ni mazoea kwa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kuendesha mipango yake kwa njia ya rushwa na ufisadi.

Alisema ana ushahidi wa kutosha juu ya mwenendo mbovu ambao umesababisha serikali kushindwa katika kesi ya Dowans kwa ajili ya maslahi ya watu wachache.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua ni kiwango gani cha umeme kinatakiwa kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Aidha, alihoji ni kiasi gani cha nishati ya umeme kilichoongezeka na kilichozalishwa ikilinganishwa na hali ilivyokuwa awali.

Akijibu, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema ili kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, kiasi cha MW 4,117 kitahitajika.

Simbachawene alisema katika mpango wa muda mfupi ni kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka MW 1,375.74 za sasa mpaka MW 2,500 ifikapo mwaka 2015.

Alisema ongezeko hilo litahusisha mchango jadidifu kama vile umeme wa jua, upepo na jotoardhi (geothermal) kwenye uwiano wa uzalishaji.

Alisema Serikali kupitia Tanesco iliandaa mpango kabambe wa kuendeleza sekta ya ndogo ya umeme ambapo tangu kuanza kwa utekelezaji wa mpango wa Dira ya Taifa mwaka 2000, uwezo wa kuzalisha umeme umeongezeka kwa kiasi cha MW 575.74 ikilinganisha na MW 800 zilizokuwepo mwaka 2000.

Kuhusu tuhuma za rushwa na ufisadi ndani yaTanesco, alisema hana taarifa hizo na kueleza kuwa swali la nyongeza halihusiani na swali la msingi hivyo akamuomba Mbunge kutafuta njia maalum ya kuliwasilisha.

Hata hivyo, suala la Dowans liliibuka baada ya kipindi cha maswali na majibu, ambapo Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, aliomba Mwongozo wa Spika kwa Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba, na aliporuhusiwa alitaka Kafulila apewe nafasi ya kutoa maelezo kamili na ushahidi kuhusu kampuni hiyo.

Wakati Machali akiendelea kutoa maelezo hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na Mabumba alipomuona, alimkatiza Machali na kumpa Lukuvi fursa ya kuzungumza.

Lukuvi alisimama ili kutoa taarifa kwa kutumia kanuni ya Bunge kukosoa mwongozo ulioombwa na Machali, lakini wakati akiendelea kuzungumza, baadhi ya wabunge waliguna kwa nguvu kuashiria kumpinga.

Mbali na miguno hiyo, pia Kafulila alisimama na kupinga kitendo cha Mabumba kumkatiza Machali na kumruhusu Lukuvi kuzungumza.

Kafulila alisema kikanuni, Lukuvi, hakupaswa kuomba mwongozo wakati tayari kulikuwa na maombi mengine ya mwongozo wa Spika, ambayo muombaji (Machali) alikuwa bado anaendelea kuyatolea maelezo.

Kutokana na hilo, alimtaka Mabumba amruhusu Machali kuendelea kuzungumza hadi mwisho, akisema Lukuvi siyo mpiga ramli, kwani hajui, ambacho Machali alitaka kukizungumza.

Baada ya Kafulila kueleza hivyo, Machali naye alisimama na kuomba kutoa taarifa, huku Lukuvi naye akishikilia kutaka kuendelea kuzungumza.

Hata hivyo, Mabumba alimzuia Machali kuzungumza na kumweleza pia Kafulila kuwa alikiuka kanuni ya Bunge, ambayo inataka Mbunge kusimama na kuzungumza baada ya kuwa ameruhusiwa na kiti.

Baada ya kueleza hayo, Mabumba, alimruhusu Lukuvi kuendelea kuzungumza, ambaye alisisitiza kuwa kikanuni, Machali alikosea kwani alitakiwa kuomba mwongozo huo wakati ule ule, baada ya mtoa hoja (Kafulila) kukaa chini na kwamba Machali hakufanya.

Hata hivyo, hoja hiyo ya Lukuvi ilipingwa na Mabumba, hivyo akamruhusu Machali kuendelea kuutolea maelezo mwongozo aliouomba.

Machali alisema hoja iliyotolewa na Kafulila inaonyesha kuwa Mbunge huyo anayo maelezo kamili na ushahidi kuhusu Dowans, hivyo akaomba aruhusiwe kuviwasilisha bungeni ili kuliepusha taifa kuendelea kupoteza pesa.

Hata hivyo, hoja hiyo ilizimwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na kuungwa mkono na maamuzi ya Mabumba.

Jaji Werema alisema licha ya kuwa kila mtu ana haki ya kupata taarifa, serikali siyo sehemu ya kesi ya Dowans iliyoko mahakamani, hivyo akasema kama Kafulila ana ushahidi, basi akautolee mahakamani na siyo bungeni.

“Kwa hiyo mwongozo hauna manufaa, unavunja kanuni na naomba ukataliwe,” alisema Jaji Werema na kuungwa mkono na Mabumba, ambaye naye alisisitiza kumtaka Kafulila kupeleka ushahidi alionao kuhusu Dowans mahakamani.


Oktoba 14, 2006 kampuni ya Richmond Development L.L.C ya Texas, Marekani ilitiliana saini mkataba na kampuni ya Dowans Holdings S.A ya Costa Rica ili kuhamisha mkataba kati yake na Tanesco kuendesha, kuzalisha na kuuza umeme wa dharura kutokana na ukame uliokuwa unalikabili taifa wakati huo.

Richmond ambao walikuwa wameingia mkataba na Tanesco mkataba wake ulidaiwa ni batili kwa kuwa ilikuwa siyo kampuni halali, hali iliyotikisha serikali baada ya kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela (Sasa Waziri wa Uchukuzi), Dk. Harrison Mwakyembe, kueleza kuwa Richmond ilikuwa kampuni ya mfukoni.

Kutokana na ripoti hiyo, aliyekuwa Waziri wa Mkuu, Edward Lowassa, alijiuzulu na kusababisha Baraza la Mawaziri kuvunjika kutokana na sakata hilo.

Pia walijiuzulu mawaziri walihudumu kwenye Wizara ya Nishati na Madini, Bazir Karamagi na Mtangulizi wake, Dk. Ibrahim Msabaha wakati huo akiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mkataba kati ya Tanesco na Dowans ulisainiwa Juni 23, mwaka 2006 kwa ajili ya kuzalisha umeme wa dharura, mkataba huo ulijulikana kama ‘Power Off – Take Aggreement (POA)” chini ya kifungu cha 14 (e) cha POA.

Tangu wakati huo, Dowans iliendelea kutambuliwa kuwa ndiyo iliyokuwa inatekeleza majukumu ya Richmond na hata baada ya mkataba wake kusitishwa na serikali, ndiyo ilikwenda Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) dhidi ya Tanesco na kudai fidia, hatua ambayo ilisababisha shirika hilo la umeme kuamuriwa kulipa Sh. bilioni 94.

Dowans nayo iliuzwa kwa Symbion ambayo ndiyo inaendesha mitambo hiyo yenye uwezo wa kuzalisha megawatui 120 za umeme.

Suala la Richmond, Dowans na baadaye Symbion limekuwa tata kiasi cha kuacha maswali mengi ya kiutendaji na ya kisiasa.