SAKATA la kusimamishwa kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Marko Ntunga, limewagawa wabunge hususan wanaotoka katika mikoa inayolima zao la Pamba.
Wakati Bunge likikaa kama kamati kupitia kifungu kwa kifungu, Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), aliomba ufafanuzi wa Waziri wa Kilimo, akitaka kujua ni kwa nini mkurugenzi huyo anaendelea na kazi wakati amesimamishwa kupisha uchunguzi.
Cheyo ambaye pia ni mwenyekiti wa wabunge wanaotoka mikoa inayolima pamba, alisema kuwa mkurugenzi huyo bado anaendelea na kazi kwani hata hivi karibuni alikuwa mjini hapa ingawa kwenye kikao hakutambulishwa.
Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Christopher Chiza, alisema kuwa suala la mkurugenzi huyo limekuwa na utata kutokana na wabunge wanaotoka mikoa inayolima pamba kutokuwa na msimamo wa pamoja katika tuhuma zao kwake.
“Mheshimiwa mwenyekiti hili suala la Ntunga kwa kweli hata sisi limetupa utata sana kwani wabunge hawa ni kama wanapishana kwenye msimamo wao.
“Mtakumbuka kuwa baada ya kutuhumiwa humu bungeni na baadhi yao, mwenzao John Shibuda (Maswa Mashariki), alimtetea akidai kuwa anabebeshwa madhambi ya wengine kwani uovu ulioko sasa kwenye bodi hiyo aliukuta,” alisema.
Chiza alifafanua kuwa ni katika utata huo wamejikuta wakienda kwa umakini lakini akasisitiza kuwa bado msimamo wao uko pale pale kuwa Ntunga atasimamishwa kwa muda kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na kama hatakutwa na hatia atarudishwa kazini.
Mapema mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alitaka kuibua tafrani pale alipoomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya 112 (1) akitaka mjadala wa Kamati ya Bunge zima kwa wizara ya kilimo uanze upya kwani hadi wanaahirisha mwishoni mwa wiki idadi ya wabunge ilikuwa haitimii hatua iliyofanya mchakato mzima kuwa batili.
Hata hivyo, Spika wa Bunge Anne Makinda, alikataa hoja hiyo akisema kuwa wataendelea pale walipoishia kwani walikuwa sahihi maana hawakufikia maamuzi.
Spika Makinda pia alizima hoja ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), ambaye alitaka waziri alieleze Bunge ni kiasi gani cha posho wanapaswa kulipwa wajumbe wanaohudhuria vikao husika ambapo alitolea mfano wa Bodi ya Korosho chini ya mwenyekiti wake, Anna Abdallah, na wajumbe Jerome Bwanausi, Mudhihir Mudhihir na mkewe waliolipana sh milioni 7.3 kwenye kikao.
Kuhusu ugonjwa wa migomba mkoni Kagera maarufu kama mnyauko, Waziri Chiza alikubaliana na hoja ya mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage ya kutumia utaalam wake aliopendekeza na kuongeza kuwa serikali inakusudia kuwapeleka wataalamu wake na baadhi ya wakulima nchini Uganda ili kujifunza zaidi.
Alisema nchi hiyo imepiga hatua kubwa ya mafanikio katika kuutokomeza ugonjwa huo, hivyo wameona ni bora wakulima wa Tanzania nao waende kujifunza mbinu hizo.
Waziri Chiza pia alikubaliana na hoja ya mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora, akisema anawasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuweka utaratibu wa muda maalumu kwa Mufilisi wa Mali za Serikali kwani imebakia kuwa baadhi wanatumia ujanja kwa kukaa na mali hizo muda mrefu wakijinufaisha.