Friday, July 13, 2012

Madaktari kuandamana

Upande wa kulia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Rodrick Kabangila
Baada ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuwafutia leseni pamoja na kuwasimamisha kazi madaktari 400 waliopo kwenye mafunzo ya vitendo, madaktari kote nchini wanatarajia kufanya maandamano jijini Dar es Salaam kupinga dhuluma na uonevu dhidi yao.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Rodrick Kabangila, alisema wiki ijayo madaktari kote nchini wataungana kwa kufanya maandamano yatakayoanzia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) hadi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Dk. Kabangila, alisema, lengo ni kuishinikiza serikali kuunda tume huru itakayochunguza suala la kupigwa, kuteswa na kutupwa katika msitu wa Mabwepande Dk. Stephen Ulimboka, pamoja na kupinga dhuluma na uonevu unaoendelea dhidi ya madaktari.

Aliongeza kuwa maandamano hayo ni ya amani na kwamba madaktari wote watavaa makoti meupe na wale wasio madaktari watatakiwa wawe na vitambaa vyeupe.

Alisema leo kutakuwa na mkutano wa dharura wa wanachana wote wa MAT utakaojadili mustakabali, changamoto na mwenendo wa taaluma ya udaktari nchini.

Kuhusu kupata kibali kufanya maandamano hayo kutoka Jeshi la Polisi, Dk. Kabangila, alisema watakachokifanya ni kuomba ulinzi kutoka jeshi hilo na siyo kibali kutokana na kwamba maandamano siyo ya fujo bali ni ya amani.

Alisema MAT imeshangazwa na hatua ya kuwafukuza madaktari 400 wakati Tanzania inakabiliwa na upungufu mkubwa wa kada hiyo na kwamba uwiano ni kuwa daktari mmoja anahudumia wagonjwa 30,000; idadi aliyoeleza kuwa ni kubwa sana.

Naye mwakilishi wa madaktari waliopo kwenye mafunzo, Dk. Frank Kagoro, alisema kitendo walichofanyiwa madaktari 400 walioko kwenye mafunzo ni uonevu na hakikustahili dhidi yao.

Alisema madaktari waliopo kwenye mafunzo (Interns) wanafanya kazi chini ya usimamizi wa madaktari bingwa waliotangaza kugoma Julai 2, mwaka huu hivyo wasingeweza kufanya kazi pasipo kuwepo kwa madaktari hao.

Alisema shitaka wanalopewa madaktari hao wa vitendo la kuhatarisha maisha ya wagonjwa ni uonevu na anayestahili kupewa adhabu hiyo ni madaktari bingwa waliotangaza katika vyombo vya habari kuwa wanagoma.

Dk. Kagoro alisema awali, waliambiwa waandike barua kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii lakini kabla ya kuandika barua hizo hukumu ikatolewa dhidi yao pasipo kuwasikiliza.

Aliongeza kuwa gharama za kumsomesha daktari mmoja ni Sh. milioni 30 hadi milioni 40 hivyo kuwafukuza madaktari 400 ni upotevu mkubwa wa fedha za umma.

ILO NA BARUA YA MAT

Shirika la Kazi Duniani (ILO), limesema kuwa barua waliyoletewa na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Dk. Alberic Kacou, kuhusu maombi ya madaktari bado wanaishughulikia.

Akizumgumza na NIPASHE, Ofisa Habari wa ILO Tanzania, Magness Minja, alisema barua hiyo waliipokea juzi kutoka makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) na bado wanaishughulikia.

Alisema maombi ya madaktari yanahitaji kushughulikiwa kwa kushirikisha sekta kadhaa za haki za binadamu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na sheria ya kazi katika kutoa maamuzi, hivyo siyo jambo la kutoa maamuzi haraka.

Juni 26, mwaka huu madaktari kote nchini walitangaza kusitisha kutoa huduma  kwa wagonjwa kwa madai ya kutokuwepo kwa vitendea kazi katika hospitali na kudai kuboreshwa kwa huduma ya afya nchini pamoja na maslahi bora jambo ambalo limeibua mgogoro baina yao na serikali.

Wakati mgogoro huo ukiendelea, Dk. Ulimboka aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari,  alitekwa, kupigwa na kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana na hivi sasa anatibiwa nchini Afrika Kusini.