Thursday, July 19, 2012

Kova atakiwa kurudia filamu ya Dk. Ulimboka

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama ‘Sugu’ (CHADEMA), amempiga kijembe Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Suleiman Kova, akimtaka arudi studio atengeneze vizuri filamu ya utekwaji wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
Sugu alisema filamu iliyopo hivi sasa haileweki kwenye jamii, kwa kuwa tukio hilo limegubikwa na utata, hasa baada ya Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kuibuka na kudai kuwa mtuhumiwa aliyekamatwa na jeshi hilo ni mwendawazimu.
Kijembe hicho alikitoa juzi jioni bungeni alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2012/2013.
Alibainisha kuwa licha ya serikali na Bunge kufunga mjadala juu ya kutekwa kwa Dk. Ulimboka, kwa madai kwamba suala hilo liko mahakamani, ukweli utabaki kuwa filamu hiyo haikuchezwa vizuri.
“Jambo hili lina utata sana, hivi sasa wanajaribu kuliingiza katika mambo ya kidini, Kamanda Kova filamu yako haieleweki….katengeneze nyingine,” alisema.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimzuia Sugu kuendelea kugusia jambo hilo, kwa kuwa tayari Bunge lilikwisha kubaliana kutolijadili suala hilo kwa sababu lipo mahakamani.
Wiki iliyopita Kamanda Kova alitangaza kukamatwa raia wa Kenya, Joshua Mulundi (21), akihusishwa na utekaji huo, na kwamba mtuhumiwa huyo ni muumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe.
Kova alidai raia huyo mwenye kitambulisho cha utaifa namba 29166938 kilichotolewa Oktoba 11, 2010 katika Wilaya ya Nyeri nchini Kenya, pia anamiliki hati ya dharura ya kusafiria yenye namba 0123431 iliyotolewa Juni 14 mwaka huu huko Namanga, Kenya.
Alisema mtuhumiwa huyo na wenzake 12 wako kwenye kikundi kijulikanacho kama Gun Star, chenye makao yake Iwiru, Wilaya ya Thika nchini Kenya na kwamba kinaongozwa na mtu mmoja ajulikanaye kama Silencer, akisaidiwa na Paft.
Alisema pia mtuhumiwa huyo alidai kuwa wamekuwa wakijihusisha na matumizi ya silaha na kwamba wamekuwa wakifanya matukio mengi ya uhalifu nchini Kenya.
Alisema baada ya utekaji huo, Juni 29 mwaka huu raia huyo alikwenda katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko Kawe kwa nia ya kutaka kuonana na kiongozi wa kanisa hilo, Mchungaji Gwajima, lakini hakufanikiwa badala yake alionana na msaidizi wake ajulikanaye kama Joseph Marwa Kiriba.
Siku mbili baada ya polisi kutoa taarifa hizo, Mchungaji Gwajima alikana mtu huyo kwenda kutubu kanisani kwake, bali alikamatwa nje ya viwanja vya kanisa hilo na walinzi.
Alisema mtu huyo alionekana kurukwa na akili, kwani alikuwa akipiga kelele, jambo lililowafanya walinzi kumchukua  na kumpeleka polisi.
Katika hatua nyingine, Sugu aliitaka serikali kuunda tume huru kuchunguza vurugu zilizotokea Novemba 11 mwaka jana mkoani Mbeya, ambazo ziliwahusisha polisi na wafanyabiashara ndogondogo.