Friday, July 20, 2012

Kikwete ataka wananchi wawe wavumilivu ajali ya Zanzibar



RAIS Jakaya Kikwete amesema, wananchi wanapaswa kuwa wavumilivu na moyo wa subira wakati huu baada ya kuzama kwa meli ya mv Skagit visiwani Zanzibar kuwa kuwa, kazi ya uokoaji inaendelea.

Meli hiyo iliyoondoka Dar es Salaam saa sita mchana ilipinduka na kuanza kuzama jana alasiri katika eneo la Chumbe, Zanzibar.

“Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kueleka Zanzibar ilikuwa imebeba watu 290. Kati yao watu wazima 250, watoto 31 na wafanyakazi wa meli 9” imesema taarifa ya Ikulu na kubainisha kuwa, Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Kikwete aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Muungano yaani JWTZ na Polisi waanze kazi ya uokoaji mara moja.

Ikulu imesema, hadi jana usiku zilipositishwa shughuli za uokoaji hadi leo, watu 136 walikuwa wameokolewa na maiti 31 zilikuwa zimepatikana lakini mali zilizokuwa kwenye meli hiyo hazikuweza kuokolewa.

Rais Kikwete ametoa salamu za rambirambi kwa waliopotelewa na jamaa zao na kuwapa pole waliopata majeraha na kwamba, huu ni msiba wa Watanzania wote, na majonzi ni ya Watanzania wote.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein na viongozi wote wa ngazi mbalimbali kwa uongozi wao thabiti tangu taarifa ya kutokea kwa ajali mpaka sasa.” imesema taarifa ya Ikulu.

“Kama ilivyofanyika katika ajali ya MV Spice Islander miezi 10 iliyopita, uchunguzi wa kina utafanyika kubaini chanzo cha ajali. Kutokana na ajali hiyo na msiba huu mkubwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ametangaza maombolezo ya taifa ya siku tatu ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo, tarehe 19 Julai, 2012” imesema taarifa hiyo.