Monday, July 23, 2012
Kesi ya Lulu leo Mahakama Kuu
KESI ya mauaji inayomkabili mwigizaji wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, leo inatarajiwa kutajwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutokana na maombi yake yaliyopo mahakamani hapo ya kutaka umri wake halisi uchunguzwe.
Julai 9 mwaka huu kesi hiyo ilitajwa mahakamani hapo ambapo Jaji anayesikiliza maombi ya Lulu, Fauz Twaib aliiahirisha na kupanga kutajwa leo baada ya kusema jalada halisi la kesi hiyo limeitwa Mahakama ya Rufaa.
Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam Lulu anakabiliwa na kesi hiyo ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba yanayodaiwa kufanyika Sinza jijini Dar es Salaam, Aprili 7 mwaka huu.
Maombi ya Lulu ya kutaka uchunguzi kwa umri wake, pamoja na kesi ya msingi ya mauaji iliyoko mahakama ya Kisutu zinaendelea kutajwa bila kusikilizwa baada ya Mahakama ya Rufani kuliomba jalada la kesi hiyo kufanya mapitio ya uamuzi wa Jaji Twaib baada ya upande wa mashitaka kuwasilisha maombi katika mahakama hiyo ya juu.
Umri wa Lulu umezua utata baada ya mawakili wanaomtetea, Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe kuomba mahakama ya Kisutu kesi ya mteja wao itajwe katika Mahakama ya Watoto .
Mawakili hao wakidai kuwa mshitakiwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka inavyoonesha. Mahakama ya Kisutu ilisema haina mamlaka kusikiliza maombi hayo na hivyo mawakili hao wakayawasilisha Mahakama Kuu.