Thursday, July 12, 2012

Kafulila aifufua Dowans.Serikali yawakatalia, Lukuvi azomewa.

SAKATA la malipo ya sh bilioni 95 zinazopaswa kulipwa kwa Kampuni ya Dowans na serikali, jana lilichukua sura mpya baada ya wabunge kung’ang’ania kulijadili.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ndiye aliyekuwa wa kwanza kulianzisha baada ya kuituhumu serikali kuwa ilihusika kuandaa mazingira ya kushindwa kesi hiyo.
Aliliomba Bunge limkubalie atoe ushahidi wa kutosha juu ya namna serikali ilivyohusika katika kushindwa kwa kesi ya Dowans kwa makusudi ya kuihujumu nchi.
Kafulila alitoa kauli hiyo jana katika swali la nyongeza ambapo alisema imekuwa ni mazoea kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendesha mipango yake kwa njia ya rushwa na ufisadi.
Kafulila alisema kuwa anao ushahidi wa kutosha na ambao hautakuwa na shaka juu ya mwenendo mbovu wa kusababisha serikali kushindwa katika kesi ya Dowans kwa masilahi ya wachache.
Alisema serikali haioni uchungu mabilioni ya fedha za walipa kodi kulipwa kwa kampuni hiyo ambayo ilirithi mkataba wa kuzalisha umeme kutoka Kampuni ya Richmond.
Baada ya kwisha kipindi cha maswali na majibu pamoja na matangazo, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), aliomba mwongozo wa Spika akitumia kanuni 68(7) akitaka Kafulila apewe nafasi kuwasilisha ushahidi huo.
Aliongeza kuwa tuhuma alizozitoa Kafulila ni kubwa na zina masilahi kwa taifa, hivyo ni vema Bunge likapata nafasi ya kupokea ushahidi huo na kujadili.
Kabla ya Machali hajamaliza, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, naye aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni 68 (1) akitaka mwongozo usitolewe kwa Machali kwa sababu ametumia kanuni isiyohusika.
Hata hivyo, Lukuvi naye hakuweza kuendelea kuisoma kanuni hiyo kwa kuwa baadhi ya wabunge walikuwa wakimzomea kwa madai anakwepesha hoja kwa kutumia kanuni nyingine 68 (1) wakati iliyotumiwa na Machali ni ya 68 (7).
Hali ya Bunge ilianza kuchafuka ambapo, Kafulila alidai kuwa Lukuvi ameingilia utaratibu na kiti cha Spika kisionyeshe upendeleo.
Kauli hiyo iliwafanya wabunge kushangilia, hali iliyomfanya Mwenyekiti wa Bunge, Sylivester Mabumba, kupata wakati mgumu huku akiwataka wabunge kutulia na kuwaahidi kuwapa nafasi ya kuzungumza wote wanaotaka mwongozo wake.
“Waheshimiwa wabunge sasa mkiendelea kupiga kelele hatutaweza kusikilizana, nawaombeni mtulie, hili ni jambo muhimu sana, ” alisema.
Baada ya wabunge kutulia, Mabumba alikataa ombi la Lukuvi na kumpa fursa Machali aendelee, jambo lililoufanya ukumbi wa Bunge hususan wapinzani kushangilia.
Machali alisema Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ni miongoni mwa watu waliopinga malipo yaliyofanywa au yanayotaka kufanywa kwa Dowans.
Aliongeza kuna utata mkubwa wa ushindwaji wa kesi hiyo, hivyo ni vema kiti cha Spika kikapokea ushahidi wa Kafulila na wabunge waujadili.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema alipewa nafasi kuzungumzia jambo hilo ambapo alitumia kanuni ya 64 (1) c, ambayo inazuia Bunge kujadili kesi iliyopo mahakamani kwa sababu Mahakama na Bunge ni mihimili tofauti na haingiliani.
“Mbunge awe makini katika kujua mambo, sakata hili lipo mahakamani…nashauri mwongozo wa Machali ukataliwe, hauna tija kwa taifa,” alisema.
Werema alisema kama mbunge ana ushahidi aitumie fursa hiyo kuupeleka mahakamani ambako inaweza kuutumia.
“Mheshimiwa Mwenyekiti usimbembeleze mtu wala kutumia kauli ya kuudhi…mwambie mbunge jambo hili halijadiliwi humu ndani…ushahidi wake aupeleke mahakamani,” alisema.
Baada ya kauli ya Werema, Mwenyekiti huyo wa Bunge alitumia kanuni iliyosemwa na Mwanasheria wa Serikali kuwa Bunge halina mamlaka ya kulijadili sakata la Dowans.
Septemba 28, mwaka 2011, Jaji Emilian Mushi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam aliamua tuzo ya Dowans ya sh bilioni 94 iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), isajiliwe na kuwa hukumu halali ya mahakama hiyo.
Hata hivyo, TANESCO haikukubaliana na hukumu hiyo, ambapo iliwasilisha mahakamani hapo maombi ya ruhusa ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu hiyo ya Mahakama Kuu.