Friday, July 20, 2012

JWTZ kutotumia nguvu, viboko mafunzoni





JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeweka wazi kuwa suala la kutumia nguvu na viboko wakati wa mafunzo kwa maofisa na askari, halikubaliki.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano Makao Makuu ya JWTZ, ilieleza kuwa kanuni za Jeshi na Sheria za Ulinzi wa Taifa, ofisa au askari akitumia viboko ni kosa la jinai.

“Suala la Jeshi kutumia nguvu na viboko wakati wa mafunzo kwa maofisa na askari, halikubaliki. Kanuni za Jeshi na Sheria za Ulinzi wa Taifa zinakataza kutumia viboko kwani ni kosa la jinai,” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ofisa atakayefanya hivyo atashitakiwa chini ya kifungu C.32 na akipatikana na hatia anaweza kufungwa kwa kipindi kisichopungua miaka miwili jela.

Taarifa hiyo inasema kuwa adhabu hiyo si mila na desturi za Jeshi na kuwa kazi ya Jeshi ni ya kitaalamu na mafunzo ya zama hizi ya kijeshi yameendelea kuboreshwa kila wakati na huendeshwa kisayansi, ili kutoa elimu inayoendana na karne hii.

“Ushauri wa kutumia nguvu katika mafunzo ya JWTZ kama ulivyotolewa na baadhi ya magazeti haukubaliki kwa vile unaenda kinyume na maadili ya kijeshi, Kanuni na Sheria za Ulinzi wa Taifa na pia haki za binadamu.

Msimamo wa JWTZ ni kuendelea kutumia mbinu za kisayansi katika kuwafunza maofisa na askari wake,” ilieleza taarifa hiyo. Wakati huo huo, JWTZ leo itaaga maofisa wake wakuu wenye vyeo vya Meja Jenerali na Brigedia Jenerali ambao wamestaafu utumishi kwa umri na hafla yao itafanyika Kambi ya Twalipo iliyopo Mgulani jijini Dar es Salaam.

Majenerali wastaafu watakaoagwa ni Meja Jenerali Said Said Kalembo, Meja Jenerali Samwel Kitundu, Meja Jenerali Festo Ulomi, Meja Jenerali Nicolaus Mitti, wengine ni Brigedia Jenerali Idinga, Brigedia Jenerali Kilama na Brigedia Jenerali Mangwamba.

Taarifa hiyo inasema kuwa sherehe hizo zitahudhuriwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi Luteni Jenerali Abdurahman Shimbo, maofisa wakuu, maofisa wadogo pamoja na askari.