Saturday, July 14, 2012

Hili la Dk. Ulimboka si la kufumbia macho

JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, jana lilitangaza kunaswa kwa mtuhumiwa Joshua Gitu Mhindi, raia wa Kenya mwenye kitambulisho cha utaifa Na.29166938 na hati ya kusafiria ya dharura Na.0123431, akidaiwa kuhusika katika tukio la kutekwa, kupigwa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
Juni 27, mwaka huu, Dk. Ulimboka aliokotwa na msamalia mwema katika msitu huo wa Mwabepande akiwa amejeruhiwa vibaya na kisha akafikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa na maumivu makali na kuanza kutibiwa.
Lakini hata hivyo, siku chache baadaye madaktari waliokuwa wakimtibu walisema wameshindwa kumtibu katika hospitali hiyo kwa sababu hakuna vifaa, hivyo wakamsafirisha kwenda nchini Afrika Kusini ambako hadi sasa anaendelea na matibabu.
Kamanda wa polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema kuwa vitambulisho hivyo vilitolewa Nyeri na Namanga nchini Kenya.
Katika mahojiano na polisi, mtu huyo alieza kwamba yeye ni mwanachama wa kikundi cha kihalifu kinachojulikana kama Gun Star chenye makao yake eneo la Ruiru Wilaya ya Thika nchini Kenya.
Kova aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo aliwaeleza kuwa kikundi hicho kinaongozwa na mtu mwenye jina la utani Silence akisaidiwa na Past, ambao wamekuwa wakifanya matukio mengi ya kihalifu nchini Kenya.
Alisema kuwa mtu huyo alipohojiwa zaidi alisema alikuja Tanzania na wenzake 12 kwa lengo la kumdhuru Dk. Stephen Ulimboka baaada ya kukodiwa na mtu ambaye hakumtaja jina, ambaye anaamini kuwa ni mtumishi wa serikali.
Tunapenda kuweka bayana kuwa tumeshtushwa na taarifa hizo na hivyo tungependa kulishauri jeshi la polisi na vyombo vyote vya usalama kuchunguza kwa undani madai haya yaliyotolewa na mtuhumiwa.
Ni wazi kuwa mtuhumiwa amefikishwa mahakamani wakati upelezi zaidi kuhusu tukio hilo la kutekwa Dk. Ulimboka ukiendelea, lakini madai hayo ya uwepo wa wahalifu wengine 12 toka Kenya hayapaswi kupuuzwa kamwe.
Tunasema hivyo, kutokana na ukweli kwamba tukio la kikatili kama hilo ni la aina yake linaloashiria kuwa kuna nguvu kubwa nyuma yake, hivyo iko haja ya kujipanga zaidi kwa vyombo vyetu vya usalama kubaini kundi hilo la Gun Star na nwenendo wake.
Tangu kutekwa kwa Dk. Ulimboka kumekuwa na maneno mengi ambayo yanaleta mkorogano wa tukio zima, hivyo katika kuweka nchi yetu kwenye sura nzuri ya dunia, vyombo vyetu vinapaswa kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo halisi.