Saturday, July 21, 2012

Hali tete Zanzibar

  Wabunge wazuiwa kujadili ajali ya Mv Skagit 
WAKATI Wazanzibari wakiendelea kuomboleza vifo vya ndugu zao waliofariki kwa ajali ya meli ya Mv Skagit iliyozama juzi, vurugu kubwa imezuka visiwani humo baada ya kundi la Jumuiya ya Uamsho kupigwa mabomu na polisi wakati wakisoma dua ya kuwaombea marehemu.
Vurugu hizo zilitokea jana jioni baada ya wafuasi hao wa Uamsho kumaliza swala yao ya Ijumaa na hivyo kukusanyika katika msikiti wa Malindi kwa ajili ya kusoma dua hiyo.
Hata hivyo kwa vile idadi yao ilikuwa kubwa kiasi cha kujaza msikiti huo, waumini wengine walilazimika kukaa uwanjini na wakati wakijianda kuanza dua yao, polisi walifika na kuanza kuwatawanya kwa mabomu ya machozi kwa madai kuwa hawakuwa na kibali cha kufanya mkusanyiko.
Tafrani hiyo ilidumu kwa muda kadhaa kiasi cha watu kuaza kukimbia hovyo huku na kule wakijaribu kukwepa mabomu hayo lakini baadaye hali ilitengamaa.
Wakati huohuo, zoezi la uokoji limeendelea siku nzima ya jana, ingawa hakuna maiti yoyote iliyopatikana, jambo ambalo limeifanya serikali kutangaza kuifunga kambi ya kupokelea maiti kutokana na zile zilizotolewa kuanza kuharibika.
Maiti watakaopatikana kutoka kwenye meli hiyo watazikwa na serikali moja moja bila ya kutambuliwa na jamaa zao.
Hadi kufikia juzi jioni vikosi vya uokoaji vilifanikiwa kupata maiti 68, huku 29 kati yake zikiwa zimetambuliwa majina, namba za tiketi na sehemu wanakotoka.
Katika ajali hiyo jumla ya watu 145 wakiwemo raia wa kigeni 14 wamepatikana wakiwa hai na wengine 77 hawajulikani waliko.
Wakati huo huo jeshi la polisi linaendelea kumhoji meneja wa meli ya Mv Skagit, Omari Hassan Mnkhon, baada ya kubainika kuwepo na kasoro za kumbukumbu za taarifa za safari za meli hiyo.
Wabunge wazuiwa
Nako mjini Dodoma, juhudi za wabunge kutaka ajali ya meli hiyo ijadiliwe bungeni ziligonga mwamba baada ya Naibu wa Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuitupilia mbali hoja ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), akidai hakuungwa mkono.
Mambo yalianza kwenda kombo baada ya Lissu kuomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kifungu cha 47 (1) kikiambatana na kifungu cha 47 (3) cha kutaka Bunge liahirishe shughuli zake na kujadili jambo la dharura la taifa.
Katika mwongozo wake, Lissu alisema katika kipindi cha maswali kulijitokeza swali linalohusu ajali za baharini, ambapo wabunge wengi walionyesha hisia zao hasa kutokana na ajali ya meli ya Mv Skagit iliyotokea juzi na kuua Watanzania wengi.
“Mheshimiwa Naibu Spika huu ni muda muafaka wa kulijadili suala hili hasa ikizingatiwa kuwa ni muda mfupi tu tangu itokee ajali ya Spice Islander na kuua idadi kubwa ya Watanzania, inatokea tena ajali ya meli kuzama na kupoteza maisha ya ndugu zetu, tujadili jambo hili kama dharura,” alisema.
Baada ya kauli hiyo ya Lissu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na kuliomba Bunge lisijadili jambo hilo kwa kuwa hivi sasa taifa linashughulika na uokoaji pamoja na kuhifadhi miili ya marehemu.
Alisema serikali itaunda tume ya kuchunguza jambo hilo na matokeo yake yatawekwa hadharani pamoja na kama itabainika kuna uzembe wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.
“Meli ile ina usajili wa Zanzibar, kuna mambo mengi inabidi yafuatwe lakini la msingi ni lazima uchunguzi wa kina utafanyika, naliomba Bunge lisijadili jambo hili,” alisema.
Akitoa mwongozo dhidi wa hoja ya Lissu, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliikataa hoja yake kwa madai hoja yake haikuungwa mkono na wabunge licha ya kuitumia vizuri kanuni.
CUF yataka uwajibikaji
Cha cha Wananchi (CUF), kimeitaka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, kuwajibika kutokana na kujirudia kwa ajali za majini.
Akizungumza na waandishi jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema mara baada ya kutokea kwa ajali ya Mv Spice Islander, Balozi Idd, aliwaahidi Wazanzibari na Watanzania kuwa yaliyotokea katika ajali hiyo yasingelirudiwa tena.
Alisema cha kushangaza hadi sasa serikali haijajipanga kuwa na utaratibu unaoeleweka wa uokoaji pindi ajali inapotokea, hivyo ni bora ofisi hiyo ambayo ndiyo inaratibu masuala ya maafa na uokoaji kuwajibika.
Kuhusu kutowajibika kwa Waziri wa Bandari, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Hamad Masoud Hamad, aliyetokana na chama hicho, Prof. Lipumba alisema suala hilo ni jukumu la waziri mwenyewe.
“Sisi hatujawahi kumkingia kifua kwa kuwa tayari ajali ya kwanza kuna jitihada zilifanyika na tukapewa ufafanuzi, hata hivyo nina uhakika waziri wetu atachukua maamuzi ya kisiasa, siwezi nikamsemea ana busara zake ataamua afanye nini,” alisema.
Alisema CUF imepokea kwa masikitiko taarifa ya kuzama kwa meli ya Mv Skagit iliyotokea Julai 18 na kuwapa pole wafiwa, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na tukio linalofanana na lile la Septemba 10 mwaka jana.
Hata hivyo, Prof. Lipumba alivitupia lawama vyombo husika ikiwa ni pamoja na vikosi vya ulinzi kwa kukosa kutimiza wajibu wake kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuchelewa kufika eneo la tukio.
Alisema kutokana na kasoro zote zilizojitokeza, CUF ina wasiwasi na uwezo wa manahodha na mabaharia katika kujua uwezo wa chombo chao kama kinaweza kukubaliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa siku husika pamoja na uzembe wa Sumatra na Wakala wa Meli Zanzibar (ZMA).
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetuma salamu za rambirambi kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kufuatia ajali ya meli ya Mv Skagit iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 100.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.Willibrod Slaa, alisema msiba huo umekuwa ni zaidi ya msiba wa kitaifa kwa kuwa miongoni mwa waliokufa ni raia kutoka nchi za nje.
Alisema kunahitajika mikakati ya wazi na makini kwa serikali kukabiliana na majanga mbalimbali huku akitaka viongozi wanaohusika na masuala ya usafirishaji kwa upande wa serikali wawajibike.
“Haiwezekani ndani ya mwaka mmoja kutokee ajali kubwa za kufuatana huku kukiwa hakuna hatua madhubuti ya kukabiliana na hali hiyo,” alisema.
Kuhusu Bunge kushindwa kujadili suala hilo la dharura kwa sababu ya kanuni, Dk. Slaa alisema ameshtushwa na hali hiyo na kueleza kuwa kuna haja ya kanuni hizo kuangaliwa upya kama zinakidhi matakwa ya Watanzania.
Aidha, Dk. Slaa alitaka taarifa za ajali zilizotangulia awali na kuundiwa tume ziwekwe hadharani ili wananchi wajue ni hatua gani zilizochukuliwa kwa wale waliozembea.