Tuesday, July 31, 2012

Gazeti la Mwanahalisi lafungiwa

• Kubenea atoa kauli, wadau wa habari waja juu

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelifungia gazeti la Mwanahalisi kwa muda usiojulikana, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na mwenendo wake wa kuandika habari na makala za uchozezi.

Kwa mujibu wa serikali, sababu nyingine ya kufungiwa kwa gazeti hilo ni pamoja na kujenga uhasama na uzushi, likiwa na nia ya kusababisha wananchi wakose imani na vyombo vya dola, hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa nchi.

Akisoma tamko la serikali lililotolewa na Msajili wa Magazeti jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (MAELEZO), Phabian Lugaikamu, alisema kuwa katika toleo la gazeti hilo namba 302, 303 na 304 ya mwaka 2012 na mengine yaliyotangulia yalichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.

“Mhariri wa gazeti la Mwanahalisi ameitwa na kuonywa mara nyingi lakini hataki kukiri kuwa maudhui ya makala zake hazina tija kwa jamii, pia hazifuati weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari,” alisema.

Aidha, alisema kuwa mhariri huyo mara zote katika utetezi wake amekuwa akinukuu kifungu cha 18 cha Katiba ya nchi kinachotoa uhuru wa kutoa maoni na kwa makusudi kutokunukuu kifungu cha 30 cha Katiba hiyo hiyo kinachoweka ukomo wa uhuru wa kutoa maoni.

“Serikali imeamua kulifungia gazeti hilo kutochapishwa kwa muda usiojulikana kwa mujibu wa sheria ya magazeti ya mwaka 1976, kifungu namba 25(i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai, 2012 kwa mujibu wa tangazo la serikali namba 258 lililochapishwa katika gazeti la Serikali na kutolewa jijini Dar es Salaam Julai 27, 2012,” alisema.

Aidha, serikali imewataka wamiliki, wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ili kutekeleza wajibu wa kuhabarisha, kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.

Aidha, Lugaikamu alisema kuwa serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo vitatoa taarifa za uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu.

Saed Kubenea atoa kauli


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwanahalisi Communications inayochapisha gazeti la Mwanahalisi na gazeti dada la michezo la Mseto, Saed Kubenea, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha kwani kisheria mashitaka ya uchozezi ni ya jinai, hivyo serikali kama ilikuwa na ushahidi ilitakiwa ilipeleke Mwanahalisi mahakamani.

Kubenea alisema hakuna haja ya kuogopa serikali, kwani kama ina hoja ni vema iende mahakamani ili aamuliwe mshindi nani, na kuachana na tabia ya kuendesha shughuli zake kwa kuvizia.

“Serikali ikae kimya iandikwe, kulifungia Mwanahalisi kwa habari iliyoandikwa itaonekana inakiri na inaogopa kusemwa ukweli,” alisema.

CUF yatoa tamko, Lissu awaka bungeni

Wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya afya mjini Dodoma jana, Mnadhimu Mkuu wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alitumia nafasi hiyo kuishambulia serikali na kutaka iachane na sheria kandamizi dhidi ya vyombo vya habari.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema serikali isije kudhani kutumia mabavu kwa vyombo vya habari kutasaidia kuficha maovu yake na kutaka uhuru wa vyombo vya habari upewe kipaumbele.

Jukwaa la Wahariri waja juu

Baadhi ya wadau wa habari akiwamo Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Neville Meena, alisema kuwa kitendo cha kulifungia gazeti la Mwanahalisi hakikubaliki, huku akihoji aliyelifungia ni nani na kwa utaratibu upi, kwa kipi na waziri anatoa wapi maamuzi ya kulifungia.

Meena pia alisema mfumo mzima una matatizo kwani mtu mmoja hawezi kutoa maamuzi na mahali pekee penye haki ni mahakamani, kwani ndipo sehemu watu wanapopambana na kupatikana aliyesimama kwenye haki.

“Hakuna haki wala uhuru wa habari, tunataka haki itendeke kwa wanaoandikiwa na wanaoandika, tutajuaje kama makosa waliyofungiwa yana ukweli na unasema tunalifungia muda usiojulikana ndiyo nini? Ungefuatwa utaratibu wa mahakama,” alisema.

Meena pia alisema TEF wanatarajia kutoa tamko leo kuhusiana na jambo hilo.

Mhariri Tanzania Daima aguswa

Naye Mhariri Mtendaji wa gazeti hili, Absalom Kibanda, alisema taarifa za serikali kulifungia gazeti hilo zilivuja na jambo hilo haliingii akilini kwani taifa limekuwa likizungumzia uhuru wa kujieleza.

Kibanda pia alisema kuwa sheria zilizopo ni kandamizi na kulifungia gazeti hilo ni hatua nyingine ya kukandamiza na kutishia, ikiwamo kuwanyima wanahabari haki yao na maelfu ya wananchi kupata habari kupitia Mwanahalisi.

“Kwanini wasitoe maelezo kuhusu Mwanahalisi lilifanya nini kuhusiana na kile kilichokuwa kikiandikwa? Mimi naona hata serikali haikuzingatia weledi, ikiwamo kutoa ufafanuzi na kwa stahili hii nasema Mwanahalisi iliigusa serikali pabaya,” alisema Kibanda.

Pia aliitaka serikali kutoingilia uhuru wa habari, ikiwamo kutambua gharama za demokrasia, isiinyime mawazo na kutambua kuwa ukinzani wa mawazo ndipo kwenye maendeleo.

TAMWA nao wacharuka

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake, Ananilea Nkya, alieleza kupitia mtandao wa mabadiliko kuwa hatua hiyo ya serikali ya kulifungia gazeti la Mwanahalisi badala ya kwenda mahakamani ni ishara kwamba yaliyoandikwa na gazeti hilo ni ukweli mtupu.

“Labda niulize swali moja tu, hivi mfalme akiambiwa yuko uchi, kama hajawa uchi ni kwa nini aamue kumuua/kumwadhibu aliyemwambia yuko uchi kabla ya yeye mfalme kuthibitisha kuwa hajawa uchi?,” alihoji.



Source: Tanzania Daima.