Wednesday, July 18, 2012

Filikunjombe ataka Waziri, Naibu wafungwe

MBUNGE wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), ametaka uwepo utaratibu wa kifungo cha miezi sita au mwaka mmoja kwa Waziri na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani kabla ya kuanza kazi.
Filikunjombe alisema utaratibu huo utawasaidia viongozi hao kujua na kuzifanyia kazi adha, mateso na kero wanazozipata wafungwa na mahabusu kwenye magereza hapa nchini.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka 2012/2013 iliyowasilishwa jana na Waziri wa wizara hiyo Emanuel Nchimbi.
Alisema kila mwaka wabunge wamekuwa wakipiga kelele juu ya ubovu wa magereza lakini mawaziri wa wizara hiyo hawaonekani kuyatilia maanani madai hayo.
“Hali ya gereza letu la Ludewa ni mbaya sana haijulikani yupi ni mfungwa na yupi ni askari, wote wako kwenye hali mbaya, gereza hili limetelekezwa kabisa, fedha tunapitisha lakini hakuna kinachorekebishwa sasa tumechoka,” alisema.
“Ningependa Waziri na Naibu wake wafungwe kwanza japo kwa miezi sita ndipo watajua tunachokilalamikia hapa, tuweke kipaumbele katika usalama,” alisema.
Aliongeza kuwa mfungwa na mahabusu ni binadamu hivyo ni lazima waishi kwenye magereza yenye hali nzuri tofauti na ilivyo hivi.
Askari magereza na polisi wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu lakini wabunge hawaoni umuhimu wa kuweka kipaumbele katika kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi wao.
Mbunge huyo pia alichangia kuhusu polisi ambapo alisema hawana vifaa vya kisasa zaidi ya virungu ambavyo vipo kwa ajili ya kuwapiga wafuasi wa CHADEMA pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu wanaogoma kudai mikopo ya elimu ya juu.