Wednesday, July 11, 2012

Dk. Slaa, Mnyika, Lema wabanwa.Nchimbi adai CHADEMA ni wazee wa tuhuma

SIKU moja baada ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kudai kimebaini mikakati ya makusudi ya usalama wa taifa kutaka kuwadhuru baadhi ya viongozi wake, Waziri wa Mambo ya Ndani, Emanuel Nchimbi, ameliagiza Jeshi la Polisi liwahoji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Waziri Nchimbi alisema licha ya jeshi la polisi kusita kuwahoji viongozi hao kwa madai ya kutoaminika, lakini sasa ameliagiza liwahoji na kuzifanyia uchunguzi tuhuma zao.
Alisema kama tuhuma hizo zitathibika si za kweli watachukuliwa hatua kulingana na sheria za nchi.
Juzi, CHADEMA kupitia kwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, ilieleza kubaini mkakati wa makusudi wa kuwadhuru viongozi wakuu wa chama hicho, na kudai kuwa mpango unaratibiwa na baadhi ya vigogo katika idara ya usalama wa taifa, kwa lengo la kudhoofisha harakati za kufichua ufisadi na kudhoofisha serikali na chama kinachotawala.
Viongozi wanaolengwa katika mkakati huo ni Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa, Mbunge wa Ubungo John Mnyika na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbles Lema.
Freeman Mbowe, alisema taarifa za uhakika zilizoangukia mikononi mwa intelijensia ya chama hicho zinathibitisha dhamira ya vigogo hao kuwadhuru viongozi wao na kuwataka wananchi wasisite kupigania haki yao, hata kama dhamira hiyo chafu itafanikiwa.
Alisema mpango huo unaratibiwa na mmoja wa viongozi wa juu kutoka Idara ya Usalama wa Taifa (jina linahifadhiwa). Vile vile, alimtaja mmoja wa watu wanaofuatilia nyendo za Mnyika na kwamba mkakati wa kwanza wa kumdhuru mbunge huyo ni kumuwekea sumu au kuvamiwa na watu watakaodhaniwa kuwa ni majambazi.
Hata hivyo katika hilo, Nchimbi alisema viongozi wa CHADEMA kwa muda mrefu wamekuwa na tabia ya kuvichonganisha vyombo vya dola na wananchi ili visiaminike.
Alisema suala la kuwalinda raia limesemwa kwenye Katiba na sheria kuwa ni jukumu la jeshi la polisi, hivyo mtu yeyote anayesema hana imani na jeshi hilo ana matatizo.
Alibainisha kuwa ingawa viongozi wa polisi walimuambia hawawezi kuwahoji viongozi wa CHADEMA waliosema hawana imani na jeshi hilo, amewaagiza wahojiwe bila kujali walichokisema.
“Ninyi CHADEMA …wazee wa tuhuma kwa miaka minne mmekuwa mkitoa tuhuma kwa JWTZ, polisi na usalama wa taifa, sasa tukiwachagua kuongoza nchi itakuwaje?” aliuliza Nchimbi.
Alisema iwapo itatokea siku moja jeshi la polisi likatangaza kupumzika kwa muda wa saa nne bila kukamata wala kuhoji jambo lolote nchi itakuwa kwenye hali mbaya hivyo ni vema wanasiasa wakajiepusha na kauli zenye lengo la kubomoa.
“Hawa viongozi wa CHADEMA wanajitafutia umaarufu wa kisiasa, wao wanajua sehemu za kupeleka taarifa zao na zinavyofanyiwa kazi, sasa kwa nini wanatumia njia zisizostahili?” alihoji.
Nchimbi aliongeza kuwa CHADEMA imeshajenga tabia ya kuvituhumu vyombo vya dola na imeshafanya hivyo kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), usalama wa taifa na sasa polisi.
Alibainisha kuwa tabia hiyo inaonyesha namna viongozi wa chama hicho wasivyo makini katika kupigania matatizo ya wananchi na kugeuka kuwa walalamikaji wa mambo yao binafsi.
Nchimbi pia alitumia fursa hiyo kukemea tabia ya viongozi wa kisiasa kuvishutumu vyombo vya dola hadharani bila kufikisha malalamiko yao ndani ya utaratibu unaostahili na kusema kuwa unavivunja moyo.
Waziri huyo alisema serikali haifanyi kazi kwa fitna, visasi au majungu kwani kama ingekuwa inafanya hivyo ingewakamata viongozi wa CHADEMA waliokuwa wakihusishwa na kifo cha kada mwenzao marehemu Chacha Wangwe.
Alisema pamoja na viongozi wa CHADEMA kutajwa sana kwenye ajali hiyo serikali iliyapuuza madai hayo na dereva wa marehemu Wangwe alifikishwa mahakani na kushtakiwa.
“Tutafute majukwaa ya kunufaika kisiasa kwa njia zilizo bora si hili linalofanywa na CHADEMA, wanachokifanya ni kulibomoa taifa badala ya kulijenga.
Nchimbi aliwataka wananchi na wanasiasa waondoe hofu iliyoanza kujengwa kuwa polisi haiaminiki na badala yake washirikiane na jeshi hilo kikamilifu.